Shule 10 bora matokeo kidato cha sita 2023 Tanzania

July 22, 2023 10:04 am · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na Ahmes, Tabora Boys pamoja na Mzumbe ya Morogoro.
  • Ni shule nne za umma zilizopenyeza katika orodha hiyo ya dhahabu.
  • Wavulana wang’ara zaidi ya wasichana.
  • Marian Boys imepanda hadi nafasi ya sita kutoka nafasi ya 44 mwaka jana. 

Dar es Salaam. Mchana wa Julai 13, 2023, Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) lilitangaza matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Sita mwaka 2023, matokeo yanayoonesha takriban watahiniwa wote walifaulu.

Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji  wa Necta, Dk. Said Ally Mohamed watahiniwa  96, 010 wa shule sawa na asilimia 99.9 ya waliosajiliwa wamefaulu mtihani wa kidato cha sita (ACSEE) mwaka 2023 ikiwa ni ongezeko la asilimia 0.06 ikilinganishwa na mwaka 2022.

Tofauti na miaka ya nyuma wengi walikosa ladha ya kufahamu shule zilizofanya vyema pamoja na watahiniwa waliofanya vizuri zaidi kama ilivyozoeleka hapo awali. 

Itakumbukwa kuwa Necta iliondoa utaratibu wa kutangaza shule zilizofanya vizuri pamoja na wanafunzi waliofanya vizuri mapema Januari 29, mwaka huu ikieleza kuwa utaratibu huo hauna tija katika ukuaji wa elimu nchini.  

Baadhi ya wadau wa elimu wanasema orodha ya shule 10 au wanafunzi 10 bora husaidia wazazi na walezi kufanya maamuzi sahihi wakati wa kuchagua shule na kisha huchochea ushindani chanya katika sekta ya elimu pamoja na kuchochea uwajibikaji.

Licha ya Necta kutotoa orodha ya shule 10 bora, uchambuzi wa takwimu za matokeo ya kidato cha sita mwaka 2023 uliofanywa na Nukta Habari umebaini kuwa kuna shule sita zimeendelea kusalia kwenye orodha hiyo ya dhahabu zikiwemo tatu za umma za Kisimiri, Tabora Boys na Mzumbe.

Uchambuzi huu umezingatia wastani wa ufaulu wa shule husika yaani (GPA) ambao kwa mujibu wa Necta hukokotolewa kwa kugawanya jumla ya uzito wa gredi za masomo na idadi ya masomo. Uchambuzi huu haujazingatia vigezo vingine vya ziada nje ya wastani wa GPA wa shule iwapo mamlaka zilikuwa zikitumia hapo awali.


Zinazohusiana


10. Mwandet – Arusha 

Shule ya Mwandet iliyopo mkoani Arusha ndio imeshika nafasi ya 10 kwenye orodha ya shule 10 zilizofanya vema katika mtihani wa kidato cha sita. Hii si mara ya kwanza kwa shule hii ya kaskazini mwa Tanzania kuingia katika orodha ya 10 bora baada ya kufanya miaka iliyopita ikiwemo mwaka 2020. 

Mwaka 2022 shule hii ilishika nafasi ya 32 kitaifa baada ya kuambulia GPA ya 1.96 hivyo tunaweza kusema wamejitafuta na kujipata tena.

Wanafunzi 77 waliofanya mtihani kwenye shule hiyo wote wamepata daraja la kwanza ambapo 11 wamepata daraja la kwanza la pointi tano huku 21 wakifaulu kwa pointi sita. Wanafunzi wengine 21 wamefaulu kwa daraja la kwanza la pointi saba, 20 la pointi nane na wanne la pointi tisa.

Kwa matokeo hayo Mwandet imepata wastani wa GPA ya 1.63 na kushika nafasi ya 10 kwa mujibu wa uchambuzi wa takwimu hizo za Necta. Mwaka 2022 nafasi hiyo ilishikiliwa na Shule ya Sekondari Ziba iliyopo mkoani Tabora.

9. Agape Lutheran Junior Seminary – Kilimanjaro

Nafasi ya tisa imeshikiliwa na Shule ya Seminari ya Agape iliyopo mkoani Kilimanjaro ikiwa na GPA ya shule ya 1.62. 

Mwaka 2023 jumla ya watahiniwa 30 walifanya mtihani wa kidato cha sita katika shule hiyo inayomilikiwa na Kanisa la Kiiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) ambapo 29 wamepata daraja la kwanza huku mmoja akipata daraja la pili.

Wanafunzi wawili wamepata daraja la kwanza la juu la pointi tatu, wengine wakifaulu kati ya daraja la kwanza la pointi nne hadi tisa na mmoja amepata daraja la pili la pointi 11. Mwaka jana nafasi hiyo ilishikwa na Shule ya Sekondari Mkindi ambapo mwaka huu haipo kwenye orodha ya kumi bora kitaifa.

8. Uwata – Mbeya

Shule ya wavulana ya Uwata kutoka mkoani Mbeya imeshika nafasi ya nane baada ya kupata GPA ya 1.55 ambapo kati ya wanafunzi 84 waliofanya mtihani mmoja pekee ndiye kapata daraja la pili.

Wanafunzi watatu wamepata daraja la kwanza la pointi tatu, sita wakipata la pointi nne, 18 la pointi tano, 15 la pointi sita, 25 la pointi saba, 14 la pointi nane, wawili la pointi tisa na mmoja amepata daraja la pili la pointi 10.

7. Nyaishozi – Kagera

Wastani wa GPA ya 1.54 umeifanya Shule ya Sekondari ya Nyaishozi kutoka mkoani Kagera kushika nafasi ya saba miongoni mwa shule 10 zilizofanya vizuri katika matokeo ya kidato cha sita mwaka 2023.

Hata hivyo, shule hii imesalia kwenye nafasi ambayo iliishika mwaka 2022 baada ya wanafunzi 62 waliofanya mtihani wa kidato cha sita katika shule hiyo Mei 2023 kupata daraja la kwanza la pointi tatu, hadi tisa na mmoja akipata daraja la pili la pointi 11.

6. Mzumbe – Morogoro

Baada ya kushika nafasi ya nane kwenye matokeo ya kidato cha sita mwaka 2022, sasa mzumbe imepanda mpaka nafasi ya sita mwaka 2023 baada ya kupata GPA ya 1.47.

GPA hiyo imepatikana baada ya watahiniwa 130 kupata daraja la kwanza na watahiniwa watatu kupata daraja la pili ambapo hakuna daraja la tatu, la nne au waliopata sifuri.

Mzumbe iliyopo mkoani Morogoro ni miongoni mwa shule nne za umma zilizotoboa kuingia kwenye orodha ya 10 bora.

5. Kisimiri– Arusha

Katika nafasi ya tano, shule nyingine ya umma ya Kisimiri imeendelea kubaki katika orodha hiyo baada ya kuweka kibindoni wastani wa GPA ya 1.42 baada ya wanafunzi wake wote 124 kupata daraja la kwanza. 

Hata hivyo, Kisimiri iliyopo mkoani Arusha, imeporomoka kutoka nafasi ya pili iliyoshika mwaka 2022 wakati huo ikiwa na wastani wa GPA ya 1.38. Ni miongoni mwa shule chache za umma ambazo zimekuwa zikizibwaga zile za binafsi ndani ya miaka mitano sasa. 

4. Kemebos– Kagera 

Kama ilivyo kwa Arusha, Mkoa wa Kagera nao umeingiza shule nyingine katika orodha ya 10 bora kitaifa katika matokeo ya kidato cha sita 2023 ambayo ni Kemebos.

Kama ilivyo kwa Kisimiri, Kemebos nayo imeporomoka kutoka nafasi ya kwanza mwaka 2022 ambapo ilikuwa na GPA ya 1.37 hadi nafasi ya nne mwaka huu kwa kuwa na GPA ya 1.42

Hata hivyo, wanafunzi wote 35 waliofanya mtihani shuleni hapo wamepata daraja la kwanza wakitofautiana kwa pointi pekee ambapo ni wanafunzi watatu tu ndio wamepata daraja la kwanza la pointi nane.

3. Marian Boys – Pwani

Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Marian Boys kutoka mkoani Pwani imeshika nafasi ya tatu katika orodha ya shule 10 bora. 

Marian imepanda kutoka nafasi ya 44 kitaifa iliyoshika mwaka 2022 kwa kupata GPA ya 1.42 ambapo wanafunzi wote 96 waliofanya mtihani shuleni hapo wamepata daraja la kwanza pekee.

Mwaka 2022 nafasi ya tatu ilishikiliwa na Tabora Boys ambayo imepanda hadi nafasi ya pili

2. Tabora Boys – Tabora 

Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Tabora inakamilisha idadi ya shule tatu za Serikali zilizopenya kwenye 10 bora kitaifa katika matokeo kidato cha sita mwaka 2023 kwa kushika nafasi ya pili.

Tabora Boys imepanda kutoka nafasi ya tatu iliyoshika mwaka 2022 baada ya kupta wastani wa GPA ya 1.41 ni kutokana na wanafunzi wote 109 waliofanya mtihani shuleni hapo kupata daraja la kwanza.

Wanafunzi 13 wamepata daraja la kwanza la pointi tatu, ufaulu ambao ndio wa juu zaidi. Wengine 17 wamepata daraja la kwanza la pointi nne, 23 la pointi tano, 31 ambao ndio wengi zaidi wamepata daraja la kwanza la pointi sita na wengine wakipata la pointi saba hadi tisa. 

Tofauti na matokeo ya kidato cha nne, shule za umma zimekuwa zikifanya vizuri zaidi katika matokeo ya mtihani wa kidato cha sita ndani ya miaka 10 iliyopita. 

1. Ahmes – Pwani 

Shule bora kwa ufaulu katika matokeo ya mtihani wa kidato cha sita mwaka 2023 ni Ahmes iliyopo mkoani Pwani baada ya kushika nafasi kwa mujibu wa uchambuzi wetu wa matokeo hayo yaliyotolewa na Necta Julai 13. Hii ni shule ya pili kutoka mkoa huo kuingia katika shule 10 bora baada ya Marian Boys. 

Nafasi ya kwanza imeenda kwa shule ya Sekondari Ahmes iliyopo mkoani Pwani, mkoa ambao umeingiza shule mbili kwenye 10 bora taifa mwaka 2023.

Ahmess imepanda kutoka nafasi ya tano iliyoshika mwaka 2022 kwa kuiondoa Kisimiri ambayo ndiyo iliyoshika nafasi ya kwanza mwaka jana baada ya kupata wastani wa GPA ya 1.29.

Wanafunzi wote 132 waliofanya mtihani wa kidato cha sita mwaka 2023 katika shule hii ya Ahmess wamepata daraja la kwanza kati ya pointi tatu hadi nane jambo lililowawezesha kuwa bora zaidi kitaifa.

Wavulana wang’ara

Tathmini zaidi iliyofanywa na Nukta Habari imebaini kuwa shule za wavulana zimefanya vizuri zaidi kulinganisha na shule za wasichana katika matokeo ya kidato cha sita mwaka 2023.

Kwa mujibu wa Dk. Mohamed ubora wa ufaulu kwa daraja la kwanza hadi la tatu ni mzuri zaidi kwa wavulana kwa asilimia 0.12 

Kwa daraja la kwanza pekee wavulana wamefaulu kwa asilimia 41 huku wasichana wakifaulu kwa asilimia 35.

Ufaulu huu unazidi kuwaacha nyuma wasichana kifursa ambao idadi yao hupungua zaidi katika mtihani wa kidato cha nne licha ya kuwa wengi zaidi katika elimu ya msingi na Sekondari hasa kidato cha kwanza hadi cha nne kwa mujibu wa takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).

Enable Notifications OK No thanks