Dk. Mpango atoa mapendekezo matatu kuboresha rasilimali watu Afrika

July 25, 2023 11:03 am · David
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na kutoa mafunzo na elimu ya kutatua changamoto za Afrika
  • Sekta binafsi yatakiwa kuja na ubunifu kuongeza ushiriki wake kwenye kuimarisha rasilimali watu

Dar es Salaam.  Makamu wa Rais wa Tanzania Dk. Philip Isdor Mpango ametoa mapendekezo matatu yatayosaidia kuimarisha uwezo wa rasilimali watu barani Afrika ikiwemo taasisi za elimu kutoa mafunzo yenye suluhu za kukabiliana na changamoto za Afrika.

Kwa muda sasa wadau wa elimu, wamekuwa wakishauri kufanya maboresho ya mitaala ya elimu itakayowawezesha wahitimu kuajirika au kuwa na uwezo wa kujiajiri tofauti na sasa ambapo wahitimu wengi hutegemea zaidi kuajiriwa.

Kwa mujibu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) vijana milioni 10 hadi 12 huingia katika soko la ajira kila mwaka huku vijana milioni tatu pekee wakifanikiwa kupata ajira.

Makamu wa Rais Dk.Mpango aliyekuwa akizungumza kwenye ufunguzi wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Rasilimali Watu leo Julai 25,2023 amewaambia washiriki kuwa taasisi za mafunzo na elimu zina mchango mkubwa katika kukuza matumizi ya rasilimali watu.

Mpango ameongeza kuwa mchango wa taasisi hizo unapaswa kujielekeza  katika kusaidia Afrika kusimamia na kunufaika na rasilimali asilia zinazopatika katika bara hilo.

“Afrika imekuwa ikitoa rasilimali fedha kwa ajili kukuza ujuzi ili kutumia katika kunufaika na rasilimali zetu, hivyo taasisi za mafunzo Afrika zinapaswa kushirikana ili kuja na suluhu mbalimbali kwa changamoto zinazoikumba Afrika”, amebainisha Dk. Mpango jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, Kwa mujibu wa Ripoti ya Mwelekeo wa Ajira kwa Vijana Ulimwenguni ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) ya mwaka 2022, kijana mmoja kati ya watano barani Afrika, hajaajiriwa, hajapata elimu wala hana mafunzo.


Soma zaidi:


Taasisi za fedha na sekta binafsi ziunge mkono

Mpango amesisitiza kuwa taasisi za fedha za kikanda na kimataifa zinapaswa kuja na mipango yenye ubunifu katika masuala ya fedha ili kusaidia ukuaji wa matumizi ya rasilimali watu katika bara la Afrika.

“Tunapaswa kufahamu kuwa matumizi ya rasilimali watu kwa uhalisia ni mpango wa muda mrefu na hivyo inahitaji taasisi za fedha za ndani ambazo zinatoa masharti nafuu”, amesema Dk Mpango.

Ili kuwakwamua vijana kiuchumi Tanzania imekuwa ikitoa mikopo kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kupitia asilimia 10 ya mapato ya halmashauri zao, utaratibu ambao utaenda kubadilishwa kutokana na ubadhirifu pamoja na mikopo kutorejeshwa kwa wakati.

Kwa mujibu wa Dk. Mpango, sekta binafsi inamchango mkubwa katika la ukuaji na matumizi ya rasilimali watu hasa wakishirikiana pamoja Serikali, hivyo mkutano huu utumike kama nyenzo ya kujadiliana njia bora ya sekta binafsi kushiriki kuimarisha rasilimali watu.Washiriki na viongozi mbalimbali wakifuatilia hotuba ya Makamu wa Rais wa Tanzania Philip Mpango katika ufunguzi wa Mkutano wa Rasilimali Watu jijini Dar es Salaam. Picha|World Bank Tanzania

Takwimu za Kamisheni ya Uchumi Barani Afrika (UNECA) za mwaka 2023 zinaonesha kuwa sekta binafsi inamiliki zaidi ya asilimia 80 ya uzalishaji barani Afrika, theluthi mbili ya uwekezaji, robo tatu ya mitaji pamoja na kutoa ajira kwa asilimia 90 ya watu walio katika umri wa kuajirika.

Kwa upande wake Waziri wa Fedha Dk. Mwigulu Nchemba amesema Tanzania imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali katika kufanikisha dhima ya matumizi mazuri ya rasilimali watu ikiwemo kutoa elimu bure kuanzia elimu ya msingi hadi sekondari na hivyo kutoa mchango katika kuwapa ujuzi vijana mbalimbali nchini.

Mkutano wa huo ambao ni wa kwanza kufanyika nchini Tanzania umewakutanisha wakuu wa nchi mbalimbali pamoja na waziri wa kisekta kujadili uwekezaji katika rasilimali watu barani Afrika na unatarajiwa kutatamatika kesho Julai 26,2023.

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Nukta TV

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

Nukta TV

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Nukta TV