Dk Mpango azitaka nchi za EAC kuwekeza zaidi katika rasilimali watu
- Ni kutokana na kiwango cha uwekezaji wa rasilimali watu katika nchi za EAC kuendelea kuwa chini.
- Asema Nchi kuunganisha nguvu kunaweza kusaidia kupata muarobaini wa tatizo hilo.
Arusha. Makamu wa Rais wa Tanzania Dk Philip Mpango amezitaka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuongeza nguvu katika uwekezaji wa rasilimali watu kupitia elimu ili kuchochea maendeleo.
Agizo la Dk Mpango linakuja wakati nchi za Afrika zikitajwa kuwa na kiwango kidogo cha uwekezaji katika rasilimali watu jambo linalofanya shughuli nyingi za maendeleo kusuasua.
Takwimu za Benki ya Dunia (WB) zinabainisha kuwa uwekezaji wa rasilimali watu kwa nchi za Afrika ni chini ya asilimia 0.4 kikiwa ni kiwango kidogo kulinganisha na kiwango cha dunia cha asilimia 0.57 kinachohitajika.
Dk Mpango aliyekuwa akizungumza katika mkutano wa kwanza wa elimu uliofanyika jijini Arusha leo Agosti 13, 2024 amebainisha kuwa kauli mbiu ya mkutano huo ilipaswa kubeba dhima ya rasilimali watu kutokana na umuhimu wa sekta hiyo.
“Kongamano hili la Agosti linatoa fursa ya kutafakari maendeleo na changamoto za EAC katika elimu kwa kuhusiana na bara zima, nimeona mada ya kongamano hili ila ingepaswa kubadilishwa kidogo kutoka ‘elimu kwa waafrika’ hadi ‘kuendeleza rasilimali watu kwa ajili ya Karne ya 21,” amesema Dk Mpango.
Katika hatua nyingine Dk Mpango amezitaka nchi hizo kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya elimu katika jumuiya hiyo ikiwemo kiwango na ubora wa elimu inayotolewa, ubora na kiwango cha walimu, pamoja na matumizi ya Tehama na teknolojia.
Ili kutatua changamoto hizo Dk Mpango amezitaka nchi wanachama wa EAC kuunganisha nguvu za pamoja kwa sababu changamoto hizo zinafanana katika nchi zote.
Hata hivyo, Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof Adolf Mkenda amesema kuwa nchi za Afrika Mashariki zinafanya vizuri kiasi kulinganisha na nchi nyingine za Afrika.
“Ninavyofahamu nchi ambazo zimesogea mbele kidogo ni Kenya na Tanzania inafuata ya pili katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki,” amesema Prof Mkenda.