Rais Samia apangua vigogo TTCL, Tanesco, vilio vya umeme vikiendelea Tanzania
- Amteua Gerson Msigwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo.
- Msigwa anakuwa katibu mkuu wa tatu wa wizara hiyo ndani ya miezi saba.
- Bosi wa Tanesco apelekwa TTCL huku wa TTCL akitarajiwa kupangiwa kazi nyingine.
- Amteua bosi mpya Tanesco atakayekumbana na changamoto lukuki zikiwemo mgao wa umeme unaoendelea nchini.
Dar es Salaam. Wiki tatu baada ya kufanya mabadiliko madogo katika baraza la mawaziri, Rais Samia Suluhu Hassan amepangua tena baadhi ya vigogo wa juu wa wizara na mashirika makubwa ya umma huku akimhamisha Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) katika kipindi chenye vilio lukuki vya mgao wa umeme nchini.
Katika mabadiliko yaliyofanywa leo (Septemba 23, 2023), Rais Samia amemteua aliyekuwa Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo akichukua nafasi ya Said Othman Yakubu ambaye ameteuliwa kuwa balozi.
Uteuzi wa Msigwa unaendelea kufanya mabadiliko katika uongozi wa juu wa wizara hiyo baada ya kumteua Dk Damas Ndumbaro kuwa waziri wiki tatu zilizopita akichukua nafasi ya Pindi Chana. Msigwa anakuwa katibu mkuu wa tatu wa wizara hiyo ndani miezi saba.
Nani kujaza nafasi ya Msigwa?
“Nafasi iliyoachwa wazi ya Mkurugenzi wa Habari-Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali itatangazwa hapo baadaye,” amesema Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Zuhura Yunus.
Katika mashirika ya umma, Rais Samia amemteua aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco Maharage Chande kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) ambalo nalo linakabiliwa na changamoto lukuki.
Chande anachukua nafasi ya Peter Ulanga ambaye atapangiwa kazi nyingine. Kiongozi huyo anaondoka ikiwa ni miaka miwili baada ya kuteuliwa kuongoza Tanesco na kuleta matumaini kibao ya kuboresha shirika hilo lililokuwa likitawaliwa na matatizo ya kiufanisi yakiwemo ya kukatika umeme mara kwa mara.
Ndani ya mwezi mmoja kumekuwa na malalamiko lukuki kutoka kwa watumiaji wa umeme kutokana na mgao wa umeme unaoendelea ambao Maharage alisema unatokana na upungufu wa nishati hiyo kutokana na ukame.
Kutokana na mabadiliko hayo, Rais Samia amemteua aliyewahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Boniface Gissima Nyamo-Hanga kuiongoza Tanesco.
Chande anaondoka Tanesco na Mwenyekiti wa bodi hiyo baada ya kumteua Meja Jenerali Paul Simuli kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya shirika hilo kuchukua nafasi ya Omar Issa anayeendelea na majukumu mengine ya Ofisi Rais-Tume ya Mipango.
Pamoja na kubarikiwa na gesi, maji, upepo, makaa ya mawe, jua na rasilimali asili nyingine nyingi ambazo zingeweza kutengeneza umeme, mpaka leo 2023, Tanzania bado inachechemea kwenye kutengeneza nishati ya umeme ya kutosha kuhudumia nchi nzima.
Misplaced priorities.
— Allan Lucky (@Allan_Lucky) September 23, 2023
Chande kuiboresha TTCL?
Chande, ambaye ni Mhandisi wa Elektroniki na Mawasiliano, anaelekea TTCL ambayo licha ya kuwa shirika kongwe la mawasiliano nchini bado limeshindwa kukua kwa kasi inayotarajiwa.
Hadi Juni mwaka huu, kwa mujibu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), TTCL ilikuwa na laini milioni 1.56 sawa na asilimia 3 tu ya laini milioni 64.1 zilizopo nchini. Wateja wa simu wa TTCL ni pungufu mara nne ya wale wa Halotel waliofikia milioni 8.4 Juni mwaka huu.
Soma zaidi
-
Saba wakamatwa kwa udanganyifu mitihani darasa la saba Mwanza
-
Maboresho mapya ya WhatsApp Business kurahisisha biashara za mtandaoni
Kibarua kigumu kwa Nyamo-Hanga
Nyamo-Hanga anakuwa bosi wa tatu wa Tanesco ndani ya miaka miwili huku akitarajiwa kukabiliwa na kibarua kigumu cha kupunguza makali ya mgao wa umeme unaoendelea sehemu mbalimbali nchini.
Kiongozi huyo ana uzoefu wa zaidi ya miaka 20 katika sekta ya nishati, akishika nafasi mbalimbali tangu mwaka 2008 alipoanza kufanya kazi na REA na baadaye kuteuliwa kuwa mkurugenzi mkuu kati ya mwaka 2016 na 2019.
Nyamo-Hanga mwenye Shahada ya Sayansi ya Uhandisi Umeme na Shahada ya Uzamili ya Menejimenti ya Uhandisi (Engineering Management) kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kwa mujibu wa Nikol, hivi karibuni alikuwa akifanya kazi Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) akisimamia operesheni za jengo la Bunge.
Licha ya kuwa Tanesco imeanza kupata faida, Nyamo-Hanga na timu yake watahitajika kupambana kuongeza vyanzo vya nishati ambavyo haviathiriki kwa kiasi kikubwa na mabadiliko ya tabianchi.
Julai 31, 2023 Maharage Chande aliwaambia wahudhuriaji wa kongamano la Mwananchi Jukwaa la Fikra (MTLF) kuwa faida ya Shirika hilo imeongezeka kutoka Sh77 bilioni mwaka 2021 hadi 109.4 bilioni jambo lilotajwa kuboresha huduma za shirika hilo.
Sanjari na uteuzi huo, Rais Samia amemteua Dk Erasmus Kipesha kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) akichukua nafasi ya Bahati Geuzye ambaye ameteuliwa kuwa katibu tawala wa mkoa wa Mtwara.
Ripoti ya nyongeza na Lucy Samson.