Ulega: Halmashauri itafute suluhu mgogoro wa Tan Green na Wananchi Magu, Mwanza
- Ni mgogoro uliodumu kwa muda wa miezi nane.
- Ulega asema amani na ushirikiano ndio njia ya kufikia muafaka.
Mwanza. Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega ameiagiza Halmashauri ya wilaya ya Magu mkoani Mwanza, kutafuta suluhu ya mgogoro baina ya wananchi na mwekezaji kampuni ya Tan Green ili kurejesha hali ya amani na kuepusha hasara zinazoweza kujitokeza.
Kwa muda wa miezi nane sasa kamuni ya Tan Green inayojihusisha na ufugaji wa samaki wa vizimba katika Ziwa Victoria imekuwa na mgogoro na wakazi wa kijiji cha Nyambiro, ikiwashutumu wakazi wanaofanya shughuli za uvuvi eneo hilo, kuharibu vizimba vya samaki na kusababisha hasara jambo ambalo wananchi wamelikanusha.
Kwa mujibu wa baadhi ya wakazi waliokuwa wakiwasilisha kero za mwekezaji kwa Waziri Ulega, watu watano wanahofiwa kupoteza maisha kutokana na kushambuliwa na walinzi wa kampuni hiyo kwa kuhisiwa kufanya uharibifu wa vizimba.
Soma zaidi : Bei ya mafuta yaendelea kung’ata watumiaji, wamiliki vyombo vya moto Tanzania
Ulega aliyekuwa ziarani wilayani Magu, ameshauri pande zote mbili kukutana na kukubaliana njia bora ya kila upande kutekeleza shughuli zake bila kuathiri mtu mwingine ili kuepusha vitendo vya uvunjifu wa amani na hasara kwa Serikali au mwekezaji.
“Rai yangu kwenu, wote muishi kwa amani na utulivu, mwekezaji awe tayari kufanya kazi zilizomleta na wananchi wawe huru kufanya shughuli zao bila kuvunja taratibu na kumwingilia mwekezaji,” amesema Ulega.
Ulega ameongeza kuwa mgogoro huo unaweza kutatuliwa kwa kuweka ulinzi shirikishi utakaoratibiwa na halmashauri ya wilaya hiyo, ambao utakuwa na jukumu la kuhakikisha kila mmoja anafanya shughuli zake bila kuingiliana.
“wawekezaji lazima watengeneze urafiki mkubwa sana na kijiji ili kinufaike na uwekezaji wake, na kama hiyo itashindikana basi waanzishe polisi jamii ambapo watakuwa pia chanzo cha kupata taarifa kutoka huko kijijini na hawa watakuwa wanalipwa aidha na kampuni ili wawasaidie kulinda,” amesema Ulega.
Soma zaidi : Dk. Mpango atoa maagizo mazito kwa ATCL akipokea ndege mpya
Kwa mujibu wa Justine Methusela, msimamizi wa mradi wa ufugaji samaki wa Tan Green, mradi huo unaoadiriwa kuwa na gharama ya zaidi ya Sh15.2 bilioni ukiwa na jumla ya vizimba vya samaki 52, ambavyo vina vifaraga zaidi ya milioni 10 vya sato.
Methusela amebainisha kuwa miongoni mwa changamoto inazowakabili ni wananchi kuvamia vizimba hvya samaki na kukata nyavu kwa kisu jambo lililosababisha upotevu wa zaidi ya tani 90 za samaki.
Hata hivyo, Mkuu wa wilaya ya Magu, Rachel Kasanda amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo na kueleza kuwa wameshughulikia changamoto hiyo kwa kuweka mpaka utakasaidia pande zote mbili kufanya kazi bila kuingiliana.