Rais Samia kurejea nchini kufuatia zaidi ya vifo 50, Katesh

December 4, 2023 10:54 am · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Kaya zilizoathirika mpaka sasa ni 1,150 huku idadi ya watu ikiwa 5,600.
  • Rais Samia aagiza Serikali kusimamia mazishi, gharama za matibabu.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kurejea nchini leo kufuatia vifo vya zaidi ya watu 50 na majeruhi zaidi ya 80 vilivyotokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua za El Nino.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, Zuhura Yunus,  imebainisha kuwa Rais Samia amefupisha safari yake Umoja wa Falme za Kiarabu (U.A.E) ambako alihudhuria Mkutano wa 28 wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP 28).

“Rais Samia ambaye amekuwepo Dubai kwa ajili ya Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP28) ameamua kufupisha safari hiyo na kurejea nchini haraka iwezekanavyo ili kushughulikia kwa karibu janga hilo,” imebainisha taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Yunus, idadi za kaya zilizoathirika na mvua kubwa zilizoanza kunyesha (juzi) Disemba 02, 2023  ni 1,150, huku idadi ya watu walioathirika hadi sasa ni 5,600 na ikikadiriwa takriban ekari 750 za mashamba zimeharibika.

Maafa hayo yaliyochochewa na kuporomoka kwa sehemu ya mlima Hanang, yametajwa kuathiri zaidi  mji wa Katesh hususan vijiji vya Jorodom, Ganana, Katesh na Dumbeta na vijiji vya Gendabi, Sarijandu, Arukushay, na Sebasi.

Serikali kugharamia matibabu, mazishi

Aidha, Rais Samia amemuagiza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye yuko mkoani Manyara, kuhakikisha Serikali inagharamia mazishi ya waliofariki pamoja na gharama za matibabu kwa majeruhi.

“…Rais Samia ameelekeza Serikali ya Mkoa na Kitengo cha Maafa cha Ofisi ya Waziri Mkuu kuhakikisha wananchi wote ambao makazi yao yamesombwa na maji wapate makazi ya muda kwa ajili ya kuwastiri wananchi hao,” imebainisha taarifa kutoka Ikulu.

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks