Ugonjwa wa kipindupindu waripotiwa Kagera, wanne wafariki

December 4, 2023 1:48 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni kutoka Wilayani Misenyi Mkoani Kagera.
  • Wananchi watakiwa kuchukua tahadhari.

Dar es Salaam. Mkuu wa mkoa wa Kagera Fatma Mwassa ametangaza mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu katika mkoa huo ambapo tayari watu wanne wamepoteza maisha wilayani Misenyi.

Mwassa aliyekuwa akizungumza na wanahabari leo Disemba 4, 2023 mkoani Kagera, amewaambia kuwa tayari Serikali imeanza kufanya uchunguzi wa sampuli za watu waliochangamana na wagonjwa hao kabla ya kupoteza maisha.

“Tunaendelea na uchunguzi tunafuatilia watu wote waliochagamana na wagonjwa wakati wakiugua au wakati wa mazishi lakini tayari tumechukua sampuli 18 kwa ajili ya upimaji…,” amesema Mwassa.

Kwa mujibu wa Mwassa, ugonjwa huo umegundulika Novemba 29, 2023 katika Kijiji cha Buchurago wilayani Misenyi huku wageni kutoka nchi jirani walioingia nchini hivi karibuni wakitajwa kuwa chanzo cha ugonjwa huo uliosababisha vifo vya watu watatu wa familia moja miongoni mwa waliofariki.

Mpaka sasa watu wanne wamepoteza maisha kutokana na ugonjwa huo, wanne wamelazwa na watatu tayari wametibiwa na kuruhusiwa kurudi nyumbani.


Soma zaidi:Tanzania yasema hakuna maambukizi mapya ya Marburg


Wananchi chukueni tahadhari

Aidha, Mwassa amewataka wananchi wa Mkoa wa Kagera na maeneo jirani Kuchukua tahadhari ili kuepuka ugonjwa huo ikiwemo kusafisha matunda kabla ya kula na kunywa maji yaliyochemshwa.

“Tunasisitiza tuchemshe maji ya kunywa lakini haswa haswa tusafishe vitu ambavyo tunakula…tusinywe maji bila kuchemsha hiki ni kipindi cha mvua ni rahisi vimelea vya magonjwa mbalimbali  kusambaa kupitia maji,” amesema Mwassa

Mbali na maagizo hayo amewataka wananchi kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima, kunawa mikono kila mara na kutoa taarifa za wagonjwa wa kipindupindu kwa haraka ili kuepusha kusambaa kwa ugonjwa huo zaidi.

Hii ni mara ya pili kwwa mkoa wa Kagera kuripoti magonjwa ya mlipuko ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.

Itakumbukwa tarehe 21 mwezi March 2023, Serikali ilitangaza uwepo wa mlipuko wa Marburg katika Kata mbili za Maruku na Kanyangereko zilizopo wilayani Bukoba katika mkoa wa Kagera ikiwa imepita siku tano tangu mlipuko huo utokee.

Siku 10 baadae Waziri wa Afya Umy Mwalimu alitangaza kutokuwepo kwa maambukizi mapya ya ugonjwa wa Marburg huku watu 35 kati ya 212 waliokuwa chini ya uangalizi maalumu wakiruhusiwa kurejea makwao.

Enable Notifications OK No thanks