Si kweli: Vidonge vya paracetamol vina Virusi vya Machupo

January 24, 2024 4:44 am · Daniel Mwingira
Share
Tweet
Copy Link
  • TMDA ilishakanusha uwezekano wa virusi hivyo kukaa kwenye vidonge.
  • Aidha dawa hiyo haijasajiliwa kuuzwa hapa nchini Tanzania.

Dar es Salaam. Huenda umeshakutana na picha inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii kama Whatsapp na X ikitoa tahadhari kwa watu kutotumia  vidonge vya paracetamol vyenye lebo ya “P/500” au “P-500” kwa kuwa vina virusi vya Machupo, jambo hilo ni la uongo na halipaswi kutiliwa maanani.

Ujumbe huo ulioandikwa kwa lugha ya Kiingereza, unasomeka “ONYO LA HARAKA! Jihadhari usichukue paracetamol iliyoandikwa P/500. Ni paracetamol mpya, nyeupe sana na yenye kung’aa, madaktari wanashauri ina virusi vya ‘Machupo,’ vinavyochukuliwa kuwa mojawapo ya virusi hatari zaidi duniani, na kiwango kikubwa cha vifo,” unasomeka ujumbe huo unaomtaka msomaji kuusambaza kwa watu wengine zaidi.

Picha inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii ambayo Nukta Fakti imethibitisha ujumbe uliowekwa ni wa uongo. Pichal Mtandao

Soma zaidi : Si kweli: Mtu ajirusha ghorofa ya nne hoteli ya bondeni Magomeni Tanzania

Ukweli huu hapa!

Nukta Fakti imefanya uchunguzi ili kujiridhisha na kuthibitisha madai hayo na kugundua yafuatayo;

Ukweli ni kwamba ujumbe huo umekuwa ukisambaa katika makundi sogozi ya WhatsApp, na sio mpya kama wengi wanavyodhani kwa kuwa imeshatokea katika nchi mbalimbali barani Afrika, ikiwemo hapa Tanzania, pamoja na Afrika Kusini. 

Aidha, Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA) ilitoa taarifa kwa umma tarehe 21 Agosti 2019 ikikanusha taarifa hiyo ya upotoshaji. Taarifa hiyo ilibainisha kuwa hakuna virusi vyovyote vinavyoitwa Machupo, na hakuna uwezekano wa virusi kuishi kwenye vidonge vya paracetamol. 

Pia, bidhaa ya P-500® (Paracetamol) iliyotengenezwa na Apex Laboratories Private Limited, India, haijasajiliwa nchini Tanzania, na TMDA haijawahi kutoa kibali cha uingizaji wa bidhaa hiyo.

Hata hivyo, taasisi kadhaa duniani kama vile Taasisi ya Serikali ya Singapore (Singapore’s Health Sciences Authority) na Mamlaka ya Udhibiti wa Dawa ya Zambia (Zambia Medicines Regulatory Authority), pamoja na taasisi za ukaguzi wa habari kama Africa Check, Snopes, zote zimekanusha habari kuhusu Virusi vya Machupo kuwepo kwenye dawa hizo.

Enable Notifications OK No thanks