Matokeo kidato cha nne 2023 haya hapa

January 25, 2024 11:49 am · admin
Share
Tweet
Copy Link


Dar es Salaam. Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) limetangaza matokeo ya mitihani ya kidato cha nne yaliyofanyika Novemba 13 hadi 30, 2023, Tanzania Bara na Visiwani ambapo ufaulu umeongezeka kiduchu.

Matokeo hayo yametangazwa leo , Januari 25, 2024, makao makuu ya Necta jijini Dar es Salaam na Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Dk. Said Mohamed amewaambia wanahabari kuwa jumla ya watahiniwa 484,823 sawa na asilimia 87.65 ya watahiniwa waliofanya Mtihani wa Kidato cha Nne 2023 wamefaulu.

“Mwaka 2022 watahiniwa waliofaulu walikuwa 476,450 sawa na asilimia 86.78, hivyo ufaulu umeongezeka kwa asilimia 0.87 ikilinganishwa na mwaka 2022,” amesema Dk. Said.

Kwa mwaka 2023 watahiniwa 572,359 walisajiliwa  kufanya mtihani huo wa kidato cha nne  ambapo watahiniwa wa Shule walikuwa 543,332 na watahiniwa wa kujitegemea walikuwa 29,027.

Kati  ya watahiniwa hao Wasichana walikuwa 310,248  sawa na asilimia 54.21 na Wavulana walikuwa 262,111.

Ubora wa ufaulu waongezeka kiduchu

Kwa mujibu wa Necta mwaka 2023 ubora wa ufaulu kwa watahiniwa wa shule katika mitihani hiyo iliyofanyika Novemba mwaka jana umeongezeka kiduchu kwa asilimia 0.47.

Mwaka 2022 watahiniwa waliopata ufaulu wa daraja la kwanza hadi la tatu walikuwa 192,348 sawa na asilimia 36.95, kulinganisha na watahiniwa 197,426 waliopata madaraja hayo mwaka 2023.

Aidha, Dk Mohamed amewaambia wanahabari kuwa ubora wa ufaulu ni mzuri zaidi kwa wavulana ikilinganishwa na wasichana ambapo Wavulana  waliofaulu katika madaraja hayoo ni 108,368 sawa na asilimia 44.47 na Wasichana ni 89,058 ikiwa ni sawa na 31.37.

Idadi  hiyo ni sawa na kusema wavulana wanne na wasichana watatu kati ya 10 ndio waliofaulu mtihani huo katika daraja la kwanza hadi la tatu.

Bofya hapa kuona matokeo kidato cha nne 2023 

Enable Notifications OK No thanks