Rais Samia amteua Badru kuongoza PSSSF, HESLB ikipata bosi mpya
- Uteuzi wa Abdul-Razaq Badru kwenda PSSF unakamilisha safari ya zaidi ya miaka saba katika Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Tanzania (HESLB)Â
- Dk Bill Kiwia kuchukua nafasi ya Badru HESLB.Â
Dar es Salaam. Wakati muda wa kazi unamalizika jana jioni Abdul-Razaq Badru alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Tanzania (HESLB) lakini leo hii njia ya ofisi ya bosi huyo imebadilika baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kumteua kuuongoza Mfuko wa Hifadhi za Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF).
Uteuzi huo uliotangazwa na Ikulu jana (Februari 6, 2024) unakamilisha safari ya miaka zaidi ya saba ya Badru katika taasisi hiyo muhimu katika utoaji huduma za mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu nchini.Â
Kwa mara ya kwanza Badru aliteuliwa kushika wadhifa huo Agosti 11, 2016 na hayati Rais Dk John Magufuli akitokea Taasisi ya Afya ya Ifakara ambako alikuwa akihudumu kama makamu mkurugenzi wa taasisi hiyo.
Katika mabadiliko hayo ya jana jioni, Badru anachukua nafasi ya Hosea Kashimba ambaye taarifa ya Ikulu imebainisha kuwa “atapangiwa kazi nyingine.
Soma zaidi : Deni la Tanroads kitendawili kingine Serikali ya Rais Samia
Badru atakumbukwa kwa mageuzi aliyoyafanya ndani ya HESLB ikiwemo kufanikisha urahisi wa kukusanya madeni ya mikopo kwa wanufaika ambapo mwaka 2022 taasisi hiyo ilizindua mfumo utaowawezesha waajiri kuwasilisha makato ya wafanyakazi wanufaika wa HESLB popote nchini.
Katika uteuzi huo, Badru anatazamiwa kuboresha utoaji wa huduma kwa wateja wa PSSSF ambao umekuwa ukilalamikiwa kuchelewesha malipo ya wastaafu.Â
Nafasi ya Badru pale HESLB sasa inashikiliwa na Dk. Bill Kiwia ambaye kabla ya uteuzi huo amewahi kuhudumu katika nyadhifa mbalimbali ikiwemo Mkuu wa Benki na Huduma za Fedha wa Taasisi ya Usimamizi wa Taaluma ya Benki (TIOB).
Pia bosi huyo mpya wa HESLB aliwahi kuwa mhadhiri katika Chuo Cha Usimamizi wa Fedha (IFM) pamoja na Kamishna wa Ushirikiano wa Sekta binafsi katika Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji visiwani Zanzibar.
Rais Samia pia alimteua  Dk. Thomas Nestory Bwana kuwa Mkurugenzi  TARI) ambapo kabla ya uteuzi huu Dk. Bwana alikuwa Mkurugenzi Msaidizi Mazingira (Biodiversity Conservation) Ofisi ya Makamu wa Rais akichukua nafasi ya Dk. Geofrey Mkamilo ambaye amemaliza muda wake.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Ikulu uteuzi wa Badru na Kiwia umeanza rasmi jana Februali 6,2024 wakati uteuzi wa Dk.Bwana ulianza tangu Februali 3, 2024.