Halmashauri 161 zashindwa kuvuka lengo la kupanda miti milioni 1.5 kwa mwaka

April 24, 2023 12:32 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni halmashauri 23 tu ikiwemo ya Iringa ndiyo zilifanikiwa kuvuka lengo la kupanda miti milioni 1.5 mwaka 2022/23. 
  • Miti milioni 185.6 ilipandwa 2022/23 na iliyostawi ni milioni 154.9. 
  • Kampeni ya upandaji miti inatekelezwa nchini kwa kila halmashauri kupanda miti milioni 1.5 kila mwaka. 

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikihamasisha upandaji miti kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, ni halmashauri 23 tu ikiwemo ya Iringa ndiyo zilifanikiwa kuvuka lengo la kupanda miti milioni 1.5 mwaka 2022/23. 

Kampeni ya upandaji miti inatekelezwa nchini kwa kila halmashauri kutakiwa kupanda miti milioni 1.5 kila mwaka.

Upandaji huo unalenga kupunguza kasi ya ukataji miti hasa kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kibinadamu ikiwemo kuni na mkaa, ujenzi na kilimo. 

Hata hivyo, vitendo hivyo vimekuwa vikichangia ukame, mabadiliko ya unyeshaji wa mvua, mafuriko na kuongezeka kwa kina cha bahari na joto nchini.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Dk Sulemani Jafo aliyekuwa akiwasilisha makadirio ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2023/24 bungeni leo Aprili 24, 2023 amesema katika kipindi cha mwaka 2022/23, idadi ya miti iliyopandwa ni milioni 185.6 na iliyostawi ni milioni 154.9 sawa na asilimia 83.5.

Hiyo ni sawa na kusema kwa kila miti 10 iliyopandwa ni nane ndiyo iliyofanikiwa kustawi.

Dk Jafo amesema licha ya kufanikiwa kupanda miti hiyo, bado muitikio wa halmashauri kuotesha mimea hiyo siyo wa kuridhisha.

Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Philip Mpango akipanda mti kuashiria kuzindua rasmi kampeni ya kitaifa ya upandaji miti rafiki wa maji kwenye vyanzo vya maji, zoezi lililofanyika katika chanzo cha maji cha Nzovwe 1 kata ya Mwakibete Jijini Mbeya Novemba 16,  2022. Picha | Michuzi Blog.

Amesema ni halmashauri 23 tu kati ya 184 sawa na asilimia 12.5 ndiyo zilifanikiwa kutekeleza kikamilifu lengo la kupanda miti milioni 1.5 kwa kila halmashauri mwaka huu wa 2022/23.

Halmashauri hizo ni Iringa, Kilolo, Mufindi, Bukoba, Muleba, Ngara, Korogwe, Kibondo, Butiama, Chunya, Rungwe, Mlimba, Njombe.

Nyingine ni Halmashauri ya Mji wa Makambako, Njombe, Kibiti, Mbinga, Nyasa, Madaba, Tunduru, Ushetu, Kaliua na Lushoto.

“Hivyo, ninazihimiza Halmashauri zote ambazo hazikufikia lengo kuchukua hatua za makusudi za kupanda miti ili kunusuru nchi na athari zitokanazo na uharibifu wa misitu na ukataji miti,” amesema Dk Jafo ambaye ameliomba Bunge liidhinishe Sh54.1 bilioni kwa ajili ya wizara yake kwa mwaka 2023/24.

Kati ya fedha hizo zinazoombwa, Sh35.4 bilioni sawa na asilimia 65 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida zikijumuisha matumizi ya ofisi binafsi ya Makamu wa Rais. 

Bajeti hiyo endapo itapitishwa na Bunge itakuwa imeongezeka kwa asilimia 1.8 kutoka Sh53.1 bilioni ya mwaka 2022/23.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Edward Ole Lekaita ameishauri Serikali kuhakikisha kua fedha zilizoombwa na wizara hiyo zinatumika vizuri, miradi inatekelezwa ipasavyo na kuhakikisha inawasilisha mbele ya kamati taarifa mbalimbali za utekelezaji wa bajeti kwa mujibu wa sheria.

“Serikali ihakikishe fedha inayoidhinishwa na Bunge kwa ajili ya Ofisi hii (ya Makamu wa Rais) inapatikana kwa ukamilifu ili kufanikisha utekelezaji wa majukumu yaliyopangwa,” amesema Ole Lekaita wakati akisoma maoni ya kamati yake kwa bajeti hiyo.  


Soma zaidi:


Nini kinafanyika kuokoa ukataji miti?

Waziri Jafo amesema wizara yake na wadau wanaendelea kushirikiana katika nyanja mbalimbali kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ikiwemo kutekeleza mradi wa kupunguza hewa ukaa inayosababishwa na ukataji na uharibifu wa misitu nchini. 

Lengo la mradi ni kuiwezesha Tanzania kuwa tayari katika utekelezaji wa makubaliano ya Paris chini ya Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi na kunufaika na biashara ya kaboni.

 
“Ofisi itaendelea kusimamia utekelezaji wa Mpango Kabambe wa Hifadhi ya Mazingira kwa kutekeleza shughuli zifuatazo: Kuratibu utekelezaji wa shughuli za hifadhi na usimamizi wa mazingira katika miji na majiji ikiwemo udhibiti wa taka na upandaji miti,” amesema Jafo.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW