Kutana na kijana anayeyapa thamani mazingira kwa taka za plastiki

April 29, 2023 10:18 am · Abdushakur
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni Emmanuel Mbelwa, muhitimu wa kidato cha nne.
  • Kwa siku anakusanya chupa kilo 100 ili kuokoa uharibifu wa mazingira.
  • Wadau waungana naye kuokoa mazingira.

Mwanza. Wakati dunia ikiendelea kuhamasisha utunzaji wa mazingira, vijana nchini Tanzania wanashiriki kuanzisha vituo vya ukusanyaji wa chupa za plastiki kusaidia jitihada hizo na kujipatia kipato.

Kazi hiyo ni miongoni mwa hatua za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwemo mafuriko na uchafuzi wa vyanzo vya maji.

Huu ni mwaka wa tatu kwa Emmanuel Mbelwa, mkazi wa Mtaa wa Magorofani, Kata ya Mkuyuni wilayani Nyamagana jijini Mwanza, tangu kuanzisha kituo cha ukusanyaji chupa za plastiki ili kulifanya jiji hilo kuwa safi na salama. 

Kwa siku hukusanya wastani wa kilo 100 za chupa za plastiki.  Mbali na kumpatia pesa, amechangia kwa sehemu kuwa kupunguza uchafu kwenye mtaa wake.

“Wanadharau kazi hii ila inasaidia jamii,”  anasema Mbelwa huku akionyesha kuifurahia kazi yake.

“Wanaookota chupa wanapewa majina mabaya, wanadharaulika wanaitwa wezi mtaani japo wanasaidia mazingira,” anaongeza ambaye ofisi yake iko Kata ya Luchelele karibu na Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino Tanzania (SAUT).

Anaamini kuwa eneo hili lina watumiaji wengi wa bidhaa zilizofungashwa kwenye chupa za plastiki ikiwemo maji na juisi, hivyo kituo chake kinasaidia pia kutunza mazingira. 

Mbelwa anasema kilichomsukuma kufungua kituo cha ukusanyaji wa chupa za plastiki ni baada ya kuona ongezeko la chupa huzo hususan maeneo jirani na chuo cha SAUT.

“Wanachuo wanakunywa sana maji, juisi na wakitupa chupa mimi ndiyo napata faida,” anasema kijana huyo. 

Emmanuel Mbelwa, muokota chupa za plastiki mkoani Mwanza ambaye anachangia kuokoa mazingira ya jiji hilo. Picha | Abdushakur Mrisho. 

Changamoto za kazi

Kudaiwa kuwa mwizi, umetokwa na akili ama mtumiaji wa dawa za kulevya ni miongoni mwa dhana potofu wanazotuhumiwa waokotaji na wamiliki wa vituo vya ukusanyaji wa chupa za plastiki mbali na mchango wao kwenye mazingira.

Mbelwa amesema hili hutokea kutokana na baadhi yao kutokuwa wasafi wa mwili na kutoishi vyema na jamii.

Yeye huzingatia utanashati wake pindi anapokuja kazini pia huwa na kauli njema kwa jamii inayomzunguka.

Ombi lake kwa serikali na asasi za kiraia ni kuzidi kuwapa elimu na msaada kifedha ili wafike mbali zaidi.

“Tangu nimeanzisha kituo sijaona Serikali au mashirika kuja kunisaidia chochote,  japo nasaidia utunzaji wa mazingira. Watusupport (watusaidie) kwani tuna mengi ya kufanya, ila uwezo bado haujaruhusu,” anasema Mbelwa. 


Soma zaidi:


Afisa Mazingira wa Shirika la Usimamizi wa Mazingira na Maendeleo (EMEDO-Mwanza) Kitogo Lawrence, anasema wametoa elimu kwa kaya zaidi ya 20 mitaa ya Sweya na Silivini kuhusu fursa iliyopo kwenye ukusanyaji wa chupa za plastiki ili kutunza mazingira. 

EMEDO hununua kila chupa tatu za plastiki kwa shilingi 100 na kutengeneza vitu mbalimbali ikiwemo hereni, vifaa vya kutunzia peni,  vibanda vya kupumzika na vitalu vya bustani za  nyumbani.

“Kwetu chupa ni malighafi siyo takataka unaweza kutuletea na sisi tunazinunua, hii pia inayaweka mazingira yetu salama,” anasema Lawrence. 

Kwa miaka miwili EMEDO imekusanya vitu vya plastiki wastani wa tani 6  huku chupa za plastiki pekee ni tani 1, kwa mujibu wa Lawrence. 

Hii ni sawa na wastani wa chupa za plastiki 17 katika kila vitu vya plastiki 100.

Lawrence amesema ukusanyaji wa chupa za plastiki husaidia utunzaji wa mazingira na kudhibiti plastiki kuingia kwenye Ziwa Victoria.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Silivini, Ramadhan Malugu, mbali na kukiri kuwa kituo cha Mbelwa kinasaidia utunzaji wa mazingira ya mtaa wake, ameitaka jamii kuwaheshimu waokotaji wa chupa za plastiki ili waendelee kutunza mazingira.

Pia ametoa rai kwa asasi za kiraia kuzidi kuwaelimisha wamiliki wa vituo vya ukusanyaji wa chupa za plastiki ili waifanye vyema kazi yao na kulinda ikolojia ya Ziwa Victoria.

Afisa Mazingira wa Shirika la Usimamizi wa Mazingira na Maendeleo (EMEDO-Mwanza) Kitogo Lawrence akionyesha namna wanavyotumia chupa za plastiki kuboresha mazingira ya ofisi yao. Picha | Abdushakur Mrisho. 

Kila baada ya dakika 60 dunia inakadiriwa kuzalisha zaidi ya tani 46,000 za plastiki sawa na wastani wa zaidi ya tani milioni 400 kila mwaka. Hii ni kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa mwezi Juni 2022 na taasisi ya The World Economic Forum ya mjini Geneva uswizi.

Takwimu zilizochapishwa na tovuti ya Giga Africa juu ya utafiti uliofanyika jijini Mwanza, zimeonesha kuwa samaki na viumbe wengine katika Ziwa Victoria wana asilimia 20 ya plastiki kwenye miili yao.

Pia inakadiriwa kuwa kufikia mwaka 2050 huenda chupa za plastiki zikawa nyingi kuliko idadi ya samaki katika ziwa hilo.

Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (OECD) linasema matumizi ya vifaa vya plastiki yanatarajia kuongezeka mara tatu zaidi hadi tani bilioni 1.3 mwaka 2060.

Dunia imepanga kubadili matumizi ya vifaa vya plastiki kwa asilimia 60 ya plastiki zote duniani.

Miongoni mwa malengo ni kuongeza ubadilishaji wa chupa za plastiki kutoka asilimia 6 kwa sasa hadi kufikia asilimia 41 na kuimarisha mifumo ya udhibiti taka.

OECD imesema ifikapo mwaka 2060 dunia itatumia asilimia 1 ya mapato yake kudhibiti matumizi ya plastiki.

Pia imesisitiza kuheshimu mchango wa ngazi za chini (ikiwemo vituo vidogo vya ukusanyaji wa chupa za plastiki mitaani) ili kutunza mazingira dhidi ya taka za plastiki.


/
No matches found for this filter
26 May, 2026 · TZS
No forex gainers today
No forex losers today
26 May, 2026 · TZS
No gainers today
No losers today
26 May, 2026
No active movers today
Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
MIKOA 5 YA KIPOLISI INAYOONGOZA KWA MAKOSA BARABARANI

MIKOA 5 YA KIPOLISI INAYOONGOZA KWA MAKOSA BARABARANI

Nukta TV

SERIKALI YAKAMILISHA MAZUNGUMZO MRADI WA LIGANGA NA MCHUCHUMA

SERIKALI YAKAMILISHA MAZUNGUMZO MRADI WA LIGANGA NA MCHUCHUMA

Nukta TV

🔴LIVE: KAPINGA AKIWASILISHA HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA 2026/2027 BUNGENI.

🔴LIVE: KAPINGA AKIWASILISHA HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA 2026/2027 BUNGENI.

Nukta TV