Njia zitakazokomesha uchafuzi wa bahari Tanzania

March 23, 2022 5:45 am · Nuzulack Dausen
Share
Tweet
Copy Link
  • Serikali yatakiwa kupiga marufuku matumizi ya plastiki.
  • Viongozi wa BMU wataka elimu zaidi itolewe kudhibiti uchafu baharini.
  • Serikali yawataka wenye viwanda kudhibiti plastiki zisiingie kwenye mazingira.

Bagamoyo/Dar es Salaam. Pembezoni mwa ufukwe wa moja ya visiwa vidogo vya Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani, makundi madogo madogo ya taka za nyumbani yametapakaa.

Katika taka hizi, zilizotupwa na maji ya bahari kuna chupa za plastiki, viatu chakavu, vidumu vya lita vyenye mabaki ya petroli, visodo au taulo za kike zilizotumika na barakoa.

Baadhi ya watu waliokuja katika kisiwa hiki kidogo kwa ajili ya utalii wanapita pembezoni huku wengine wakikanyaga bila hofu.

Kwa sehemu ya wakazi wa pwani, takataka hizi huenda ni jambo la kawaida ila ambacho hawafahamu ni kuwa ni hatari zaidi kwa mazingira ulimwenguni na kwa viumbe bahari ambavyo baadhi ni sehemu ya chakula muhimu kwa binadamu.

Ripoti ya Muungano wa Kimataifa wa Kuhifadhi Mali Asili (IUCN) inaeeleza kuwa tani milioni 14 za taka za plastiki hutupwa baharini kila mwaka kati ya tani milioni 300 zinazozalishwa ulimwenguni. Taka hizi hujumuisha plastiki zinazotumika mara moja tu kama vifungashio, birauli za kunywea vinywaji na mirija na kufanya asilimia 80 ya taka zote zinazotupwa baharini.

Baadhi ya wavuvi na wakazi wa pwani wanaeleza kuwa sehemu kubwa ya taka hatarishi baharini zinatupwa kutoka mitaani na maji ya mvua kutokana na kutokuwepo mfumo madhubuti wa udhibiti wa taka hizo.

Mmoja wa watalii katika moja ya visiwa vidogo vya Bagamoyo mkoani Pwani akiwa katika fukwe za eneo hilo hivi karibuni. Visiwa hivi licha ya kuwa havikaliwi na watu fukwe zake zimetapakaa uchafu unaotoka baharini. Picha|Nuzulack Dausen.

“Uchafuzi wa bahari unatokana na matumizi yetu wenyewe kwa sababu mvua zinapokuja zinakusanya uchafu wote na kuleta baharini. Kila mvua inaponyesha uchafu unajaa sana baharini hasa plastiki,” anasema Lulenga Chitanda, mmoja ya watu wanaofanya shughuli zao katika ufukwe wa Kawe jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa IUCN plastiki hizo hupatikana karibu kila ukingo wa bahari duniani hasa kwenye maeneo yenye watu wengi na vivutio vya utalii kama Bagamoyo.

Hata hivyo, kiwango cha plastiki kinachotupwa baharini huenda kikaongezeka zaidi siku zijazo.

Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) linabainisha kuwa kiwango cha taka kinachotupwa baharini kinatarajiwa kuongezeka mara mbili ifikapo mwaka 2030 kutoka wastani wa tani milioni 11 kwa mwaka na kinaweza hata kuzidi mara tatu mwaka 2040.

Hatari kwa viumbe bahari

Katika mchakato wa kikemikali unaotokana na kupigwa jua, upepo, na mawimbi, plastiki hizo huvunjika vunjika katika vipande vidogo vidogo vinavyowezwa kuliwa na viumbe vya bahari na kuwaletea madhara yanayofikia binadamu pia.

“Uchafuzi wa bahari wa plastiki unahatarisha afya ya bahari yenyewe, viumbe vyake, usalama wa chakula, afya za binadamu, utalii wa pwani na inachochea mabadiliko ya tabianchi,” inaeleza IUCN katika moja ripoti yake kuhusu udhibiti wa taka za plastiki baharini.

UNEP inakadiria kuwa mwaka 2018 pekee athari za uchafuzi wa mazingira baharini  ulimwenguni hususan huu wa plastiki katika sekta ya utalii, uvuvi na kilimo cha samaki zikijumuishwa na gharama nyingine za kusafisha taka hizo zilikadiriwa kuwa Dola za Marekani kati ya 16 hadi 19 bilioni duniani sawa na zaidi ya Sh43.5 trilioni.

Hasara ama gharama hizo zilizorekodiwa miaka mitatu iliyopita ni zaidi ya jumla ya bajeti yote ya Serikali ya Tanzania mwaka 2021/22 ambayo ni Sh37.98 trilioni.

Katika eneo la Forodhani visiwani Zanzibar kuna baadhi ya miradi ya kukabiliana na plastiki baharini kama huu ambao watu hurusha taka ili kuilinda bahari. Taka ni hatari kwa viumbe bahari wakiwemo samaki. Picha|Nuzulack Dausen. 

Kasi ya kuongezeka kwa taka za plastiki na nyinginezo inazidi kuongezeka duniani, licha ya kuwepo kwa sheria na sera mbalimbali za kuzidhibiti.

Hadi sasa kuna mikataba mikubwa ya kimataifa ya kudhibiti taka bahari ikiwemo mkataba wa kuzuia utupaji wa taka baharini wa mwaka 1972 mashuhuri kama the “London Convention,” Itifaki ya mwaka 1996  iliyoboresha mkataba wa utupaji taka baharini na mkataba wa kimataifa wa kuzuia uchafuzi wa mazingira kutoka kwenye meli (MARPOL).

Hata hivyo, siyo nchi zote zimeridhia mikataba hiyo, jambo linalozidisha ugumu katika kudhibiti taka hizo.

BMU nguzo kuu ulinzi wa bahari

Baadhi ya fukwe zenye shughuli za kijamii na kiuchumi kama masoko ya samaki, vituo vya wavuvi na vikundi vya kijamii husafisha lakini hujikuta wakizidiwa pale mvua zinaponyesha mfululizo.

Humud Mbegu, Mwenyekiti wa kikundi cha usimamizi wa fukwe cha Kawe (BMU) jijini Dar es Salaam anasema wana utaratibu wa kusafisha ukanda wote wa fukwe kila mwisho wa mwezi ili kupunguza taka ila changamoto imesalia kwa baadhi ya chupa za rangi na chupa za kioo.

“Halmashauri zinapaswa kuongea na kampuni za kuzalisha chupa ili walete fedha kwenye BMU ili kuongeza nguvu za kudhibiti taka hizo vinginevyo fukwe zitakuwa mahali hatari sana,” anasema Mbegu.

Mbegu anasema baadhi ya nyasi bahari zimeng’oka au zinapatikana mbali sana tofauti na miaka ya nyuma kwa sababu ya uchafuzi wa bahari.

“Siku hizi nyasi bahari huzipati kirahisi kwa sababu ya hizi taka na muingiliano wa maji yenye taka kutoka mtaani,” anasema Mbegu.

Hata hivyo, si fukwe zote ni chafu Tanzania. Baadhi ya maeneo wakazi wa maeneo hayo wamejiwekea taratibu zinazosaidia kukabiliana na taka baharini ikiwemo kusafisha fukwe mara kwa mara na kuwapiga faini wachafuzi.

Sehemu kubwa ya fukwe za Pangani mkoani Tanga ni safi kutokana na jitihada za wakazi wa eneo hili kufanya usafi mara kwa mara.

Wakazi wa Pangani wanasema sheria kali na faini vimefanya wakazi wa mji huu kutotupa sana taka baharini kiasi cha kusaidia kupunguza uchafuzi baharini.

Faini zapunguza uchafuzi bahari Pangani

“Ufukwe wetu huwa hauweki uchafu na kila mtu hapa anawajibika kusimamia hili. Kama mtu atatupa taka atatozwa Sh50,000 na BMU zinajitahidi sana kupanda mikoko kuzuia mmonyoko,” anasema Daud Hamis, mkazi wa Pangani.

Hamis anasema Serikali na BMU huwaelimisha wakazi wa mji huo ikiwemo umuhimu wa kutokata mikoko kwa kuwa inasaidia kuzuia bahari isingiingie mtaani.

Vikundi vya usimamizi wa fukwe (Beach Management Units) hapa vina ushawishi mkubwa katika jamii hii, licha ya changamoto zinazowakabili.

Mwenyekiti wa kikundi cha usimamizi wa fukwe (Beach Management Unit) ya Pangani Mashariki, Ally Ally anasema kiwango cha takataka katika eneo lao kinapungua japo anashahudia ongezeko kubwa la taka za plastiki baharini.

“Hizi chupa kuna wakati zinazama chini na kumomonyoka zikikaa muda mrefu na baadhi ya samaki wakila wanakufa, ‘tukidive’ (tukizamia) huwa tunaziona chupa hizi,” anasema Ally.Mamlaka wilayani Pangani katika mkoa wa Tanga zimejenga ukuta kuzuia mmonyoko wa kingo za bahari na kuzuia maafa kwa wakazi wa mji huo. Wakazi wa eneo hilo wanasema sasa hawatupi taka eneo hilo kwa sababu wanaelewa athari zake na wanaogopa kupigwa faini. Picha|Nuzulack Dausen. 

Elimu, marufuku ya plastiki kuokoa jahazi

Katika harakati zake za uvuvi, Ally anasema ameshawahi kuvua samaki mara mbili wakiwa wamemeza vipande vya chupa za plastiki, jambo linalompa hofu kuwa huenda wakaathirika zaidi siku zijazo.

“Tulifanya semina namna ya kuwaelimisha wananchi ili kudhibiti taka halisia kama magogo na majani ya minazi lakini tunaona taka za plastiki zinaongezeka. Tunaandaa mkakati wa kudhibiti taka hizi kwenye vijiji vyetu,” anasema.

Ili kudhibiti zaidi chupa baharini, Ally anashauri vifungashio vingi viwe vya karatasi kama maboksi ya juisi kwa kuwa huoza haraka baharini tofauti na plastiki na anataka elimu itolewe zaidi.

“Serikali inapaswa kupiga marufuku kabisa matumizi ya plastiki, isisitize matumizi ya chupa za kioo zinazorudishika,” anasema Ally.

Serikali yawakalia kooni wenye viwanda

Hadi sasa Serikali ya Tanzania imeanza taratibu za udhibiti wa taka za plastiki ikiwemo kuondoa mifuko ya plastiki maarufu kama rambo na hivi karibuni walizuia watengenezaji wa chupa za plastiki kuweka plastiki laini (Plastic seal) juu ya mifuniko ya chupa hizo.

Mwishoni mwa Februari mwaka huu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Dk Selemani Jafo aliwaambia wanahabari baada ya kukagua viwanda vya kuzalisha vinywaji kuwa vimeanza kutii maagizo ya Serikali yakiwemo ya kutoweka plastiki laini kwenye vifuniko.

Katika kudhibiti taka hizo, Dk Jafo aliviagiza viwanda kuimarisha mfumo udhibiti wa taka ziingie kwenye mazingira ikiwemo kuimarisha mifumo ya urejelezaji wa taka hizo.

Makala hii imedhaminiwa na WAN-IFRA-Press Freedom. WAN-IFRA haihusiki kwa namna yeyote na maudhui haya.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW