Tutarajie nini ujio wa simu mpya ya iPhone 13?

September 1, 2021 6:54 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Zitakuwa na betri bora zaidi kuliko matoleo yaliyopo.
  • Inaweza kuja na rangi ya pinki.
  • Pia kamera yake itakuwa bomba na uwezo mkubwa wa betri.

Dar es Salaam. Kwa wadau wa mitandao ya kijamii, bila shaka wameshaona picha ambayo inasambaa kwenye majukwaa hayo ya muonekano wa simu mpya ya iPhone 13 ambayo kwa mujibu wa duru za teknolojia, inaweza kutoka mwanzoni mwa mwezi Septemba 2021.

Mwaka jana, Apple ambayo ndiyo kampuni inayotengeneza simu hizo, iliingiza sokoni simu za iPhone 12 ambazo zilikuwa na matoleo manne: iPhone 12, iPhone 12 mini, iphone 12 Pro na iPhone 12 Pro Max.

Kwa mwaka huu, Apple inatarajia kuingiza sokoni iPhone 13 na haya ndiyo yanayozungumzwa kwenye midomo na maandishi ya wadau wa teknolojia kuhusu simu hiyo ambayo bado Apple hawajaweka wazi.

Muonekano mpya wa kamera na uhifadhi wa kutosha mamilioni ya picha unatarajiwa kwenye simu mpya za iPhone13. Picha| GSM Arena.

Ubora wa betri juu kwa takriban asilimia 20

Kati ya vitu vinavyoongelewa kwa simu ya iPhone 13 ni kuwa na betri imara zaidi ikilinganishwa na matoleo mengine.

Kwa simu ya iPhone 13, mwandishi wa habari za teknolojia Gordon Kelly kutoka jarida la Forbes amesema simu toleo la Pro Max linatarajia ongezeko la uwezo wa betri kwa asilimia 18 ikilinganishwa na matoleo yaliyopita.

Kelly  amesema betri itafikia hadi “mAh4352” na kuifanya simu hiyo kujumuika na simu zingine kama simu janja inayokaa na chaji kwa muda mrefu zaidi.

Kwa toleo la 13 na 13 Pro, inatagemewa uwezo wake kuongezeka kwa asilimia 10 ikilinganishwa na matoleo dada ya iPhone12 na 12Pro.

Pia, toleo la Mini, litaongezeka uwezo kwa asilimia nane kutoka mAh2,227 ya 12 Mini.

Uhifadhi mara mbili zadi

Kama mdau wa mauudhui, simu inayokuhakikishia uhifadhi wa video, picha, muziki na maudhui mengine ni muhimu. 

Apple inaainisha kuwa Uhifadhi wa 12 Pro na Pro Max ulikuwa ni wa hadi GB512, kwa matoleo ya iPhone 13 Pro na Pro Max, yanatarajiwa kuwa na uwezo wa hadi Terabaiti (TB) moja, uhifadhi unaotosha mtu kuweka hadi picha milioni 4 na filamu 250 zenye ukubwa wa GB nne.

Hata hivyo, huenda Apple wamechelewa kuwa na simu yenye uhifadhi huo kwani Samsung Galaxy S 10+ ilishavunja rekodi hiyo. 

Kwa mujibu wa duru za teknolojia, inaweza kutoka mwanzoni mwa mwezi Septemba. Picha| Forbes.

Kamera ya kutulia

Mbali na wadau wa teknolojia kusema kuwa kamera za iPhone 13 zitaongezeka kwenye kila simu ikilinganishwa na 12, kuna lingine. Kamera za iPhone 13 zinaambatana na uwezo wa kuskani vitu, kurekodi video zilizotulia na kupiga ppicha zenye ubora.

Kamera ya simu hiyo ina uwezo wa kurekodi video zilizotulia hata kama ukiwa unakimbia. Chukulia mfano huu, kama unarekodi video ya kumkimbiza mtoto, huenda video ikaonyesha kuwa na wewe ulikuwa unakimbia. Kamera za toleo la iPhone 13, zitatoa video zilizotulia kana kwamba ulikuwa umesimama.

Uwezo huo upo kwenye kamera kubwa aina ya DSLR (soma hapa) na unatumika kwa mara ya kwanza kwenye simu za Apple.

Hayo ni makubwa matatu, lakini sambamba na hayo, Forbes imeandika kuwa simu hizi zinakuja na maiki nzuri zaidi hivyo kwa wale wanaorekodi sauti kwa simu huenda zikawapendeza huku rangi ya pinki ikiongezwa kwenye orodha ya rangi zitakazotumika.

Uzuri ni kuwa, Septemba siyo mbali, Tusubiri tuone kama yaliyomo yamo.

Enable Notifications OK No thanks