Zifahamu aina za kamera na matumizi yake

Rodgers George 0616Hrs   Agosti 11, 2021 Teknolojia
  • Kamera zinatofautiana kulingana na maumbo, matumizi na hata gharama.
  • Kuna aina kuu tano za kamera na zote zina matumizi yake.
  • Kabla ya kununua kamera, fahamu mahitaji yako kabla ya kwenda dukani.

Dar es Salaam. Nini huja kichwani kwako unapowaza kununua kamera kwa ajili ya kazi au kuhifadhi kumbukumbu zako? Huenda ni njia panda ya gharama, kampuni iliyotengeneza na uwezo wa lensi hasa kama ni mgeni wa mambo haya.

Kifaa hicho cha kielektroniki kinachotumika kupigia picha kinakuja kwa maumbo, uwezo na gharama tofauti. 

Licha ya kujiuliza swali la matumizi ya kamera unayonunua kabla ya kutoa fedha yako kuichukua dukani, ni muhimu kufahamu matumizi ya kamera kulingana na aina zake.

Kampuni inayojishughulisha na masuala ya upigaji picha na video pamoja na uuzaji wa bidhaa za kielektroniki ya Adorama ya Marekani,, imeandika katika tovuti yake kuwa kuna aina nyingi za kamera lakini zinazotumika zaidi ni aina sita. Zifahamu kamera hizo sita:

Kamera ndogo za kidijitali 

Kamera za kidijitali zinahitaji mtu kuelekeza kamera sehemu anapohitaji kupiga picha na kisha kubonyeza batani ya kupigia picha. Kitaalamu zinaitwa “compact digital camera”. 

Hizi hazihitaji ufundi mkubwa kutumia na udogo wake unazipatia uwezo wa kubebeka mfukoni huku zikisifika kukaa kwa muda mrefu kulingana na utunzaji. Kamera hizi hazina gharama kubwa za manunuzi.

Hata hivyo, kamera hizi zina kikomo cha kuvuta picha (zoom), hazimpatii mtumiaji wake uwezo wa kubadilisha lensi na ubora wa picha zake ni mdogo kwa mahitaji ya picha za matumizi ya kibiashara ikiwemo matangazo.

Kamera aina ya compact ni rahisi kubeba. Picha| Canon South Africa.


Kamera za kidijitali za “Digital SLR”

Aina nyingine ya kamera ni “Digital SLR Cameras”. Hizi ni bora zaidi kuliko Compact. Kamera hizi ni kubwa kwa umbo na pia zinatumika katika matukio mbalimbali ikiwemo kurekodi video na kupiga picha zinazoweza kufaa hata kwa matangazo

Tofauti na Compact, mtu ana uwezo wa kuchagua lensi anayoitaka huku matokeo ya kazi zake yakiwa ni ya kufurahisha zaidi.

Hata hivyo, kamera hizi zinahitaji mtumiaji wake kujua mambo mengi ili kupata matokeo mazuri kwani kabla ya kupiga picha, itabidi ufanye matengenezo ya kitaalamu kupata matokeo ya picha unayohitaji. 

Hilo lisikufikirishe sana baadhi ya kamera hizi zina chaguo la kiautomatiki, kwa mtu ambaye siyo mbobeizi wa masuala ya kamera kutumia.

Unahitaji walau Sh600,000 lakini bila lensi kuipata kamera hii.

Kamera za “Mirorless”

Kamera hizi ni za kisasa zaidi kwenye tasnia ya upigaji picha. Kwa mujibu wa Adorma, kamera hizi zina sifa ya kamera za DSLR na kamera za Compact kutokana na udogo wake na uwezo wa lensi yake.

Zinafaa kwa matumizi binafsi na hata ya kibiashara kwani picha zake ni nzuri japo siyo kama zilivyo kwa DSLR.

Uzuri ni kuwa, kamera hizi ni rahisi kutumia, nyepesi, zina kasi kwenye kurekodi video na ubora wa video zake ni mzuri hata kwa kamera za bei poa.

Changamoto yake ni kuwa, betri zake hazikai na chaji kwa muda mrefu ikilinganishwa na DSLR. Pia lensi zake ni chache sokoni hivyo hazina mawanda mapana ya uchaguzi wa aina ya lensi.

Kamera za DSLR zinauwezo wa kubadilishwa lenzi  hivyo hufaazaidi kwa wapiga picha mashughuli. Picha| TechRadar.


Aina nyingi ya kamera 

Kamera zingine ni pamoja na zinazoweza kuchukua picha kwa nyuzi 360 (360 Cameras). Hizi ni kwa ambao wanahitaji video na picha za kibunifu zaidi. Na hata bei yake siyo ya kitoto.

Kwa kawaida, utahitaji walau Sh200,000 lakini matokeo yake siyo ya ubora mzuri. Ukitaka matokeo mzuri, utahitaji walau kuanzia Sh2.3 milioni.

Kamera zingine ni zile zinazotumia mkanda (film) ambazo kwa sasa zimepitwa na wakati. Gharama yake ni kuanzia Sh600,000.

Hata hivyo, uchaguzi mzuri unayoweza kufanya katika manunuzi ya kamera ni DSLR na Mirorless kwani ndiyo kamera za kisasa ambazo pia matokeo yake ni mazuri.

Makala hii imefanyiwa uthibitishaji na mpiga picha wa Nukta Habari, Gift Mijoe.

Related Post