Mfumuko wa bei wang’ang’ania kiwango cha Julai

September 8, 2021 2:03 pm · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Mfumuko wa bei umefikia asilimia 3.8 mwaka unaoishia Agosti 2021.
  • Mfumo wa bei katika huduma za usafiri wavuka asilimia 100.
  • Kiwango hicho ni cha juu kuliko miezi 19 iliyopita.

Dar es Salaam. Kasi ya mfumuko wa bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia Agosti 2021 imeendelea kubaki kama ilivyokuwa Julai mwaka huu jambo linaloonyesha mwenendo imara wa mabadiliko ya bei katika kipindi hicho.

Mfumuko wa bei wa Taifa hupima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na zinazotumiwa na kaya binafsi nchini. 

Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imebainisha kuwa mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwaka ulioishia Agosti  2021 ulikuwa asilimia 3.8 ikiwa ni sawa kabisa na kiwango kilichorekodiwa katika mwaka ulioishia Julai 2021.

Taarifa ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali iliyotolewa  leo Septemba 9, 2021 imeeleza kuwa hali hiyo imechangiwa na kuongezeka na kupungua kwa bei za baadhi bidhaa zisizo za vyakula na vinywaji visivyo na vileo (vinywaji baridi) kwa kipindi kilichoishia Agosti 2021.

Licha ya mfumuko wa jumla kubaki tambalale, taarifa hiyo inaeleza kuwa mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwezi Agosti 2021 umepungua hadi asilimi 3.6 kutoka asilimia 5.1 mwezi Julai.

Kwa upande wa huduma ambazo mfumuko wa bei umepanda ni pamoja na umeme, malazi, tumbaku, vinywaji vyenye vileo pamoja na usafiri.

Mfumuko wa huduma za usafiri ndiyo umepanda zaidi kuliko bidhaa na huduma nyingine ambapo umefikia asilimia 104.1 mwaka unaoishi Agosti kutoka asilimia 103.5 mwaka unaoishia Julai.

Licha ya mfumuko wa bei kubaki pale pale, bado rekodi hiyo inakuwa ni ya juu zaidi kuwahi  kurekodiwa ndani ya miezi 19 iliyopita ambapo mara ya mwisho mfumuko wa bei umeripotiwa kuwa na kiwango kama hicho Desemba 2019.

Tangu hapo mfumuko wa bei umekuwa ukiangukia kati ya asilimia 3 na asilimia 3.6.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW