Umechoshwa na kazi? Fanya haya kuongeza ufanisi
- Unapoanza kuona kazi yako inakupa msongo wa mawazo, ujue unahitaji mapumziko.
- Unashauriwa kuweka mipaka ya kazi na maisha yako ya kawaida.
- Pia fanya kile unachokipenda.
Dar es Salaam. Katika uwajibikaji wako kazini, ipo siku ambayo unaona kabisa mambo hayaendi na ubongo unakuwa umechoka kufanya kazi yoyote.
Unakuwa kwenye hali ambayo usipoitilia maanani, huenda ukamaliza siku nzima bila kukamilisha lolote hasa kukiwa hamna mtu anayekusimamia.
Katika nyakati hizo ambazo raia wanaziita “ubongo kuganda”, baadhi hujikuta wakianza kazi na kushindwa kuzimaliza kwa kurukia kazi nyingine au kutoka kwenye reli ya umakini wa kazi hizo.
Na wakati mwingine mtu huacha kazi na kuzama kwenye mitandao ya mitandao ya kijamii na kujikuta akipoteza siku bila kufanya jamba la maana.
Kwa lugha ya wale waliosalimia “good morning sir” darasani, hali hiyo inaitwa”burnout” na hizi ndio dalili za hali hiyo:
Dalili za kukatia tamaa kazi yako
Mojawapo ya dalili ni kuiona kazi yako kama chanzo cha msongo wa mawazo na kwa baadhi huanza kuwaona wafanyakazi wenzao kama watu wasiofaa kufanya kazi nao.
Mara nyingi kwenye kipindi hiki wengine huanza kutuma maombi ya kazi zingine tena kwa juhudi.
Tovuti ya Very well Mind inaeleza kuwa, kwenye hali hiyo mtu anakuwa analalama juu ya mazingira ya kazi na mtu anaweza kuzizuia hisa zake za uvumilivu.
Dalili nyingine ni kukosa nguvu za kufanya kazi ambayo unajua kabisa ndiyo inayokuwekea chakula chako mezani au kukutimizia baadhi ya mahitaji yako.
Siyo kila wakati utakuwa na ufanisi mzuri katika kazi yako. Zipo nyakati ngumu ambazo unahitaji mapumziko kupata nguvu ya kuendelea kutimiza majukumu yako. Picha| Glenn Carstens-Peters/Unsplash
Pia, kwa baadhi utendaji wao wa kazi hupungua na kuwa na mtazamo hasi wa kazi.
Very well Mind imeandika “mtu anapofika kwenye hali hii ni ngumu kuwa na makini lakini pia hukosa ubunifu kwenye kazi zake.”
Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na kampuni ya Gallup, inayojihusisha na masuala ya ajira, hali hiyo kwa ofisini inaweza kusababishwa na vikwazo anavyopata mfanyakazi ikiwemo kukosa ushirikiano kutoka kwa meneja na wafanyakazi mwenzake au kuwa na kazi nyingi.
Sababu nyingine ni kukosa dira kamili ya kimajukumu na wafanyakazi kutokuridhishwa na vitendo vya wakuu wao hasa maslahi.
Njia za kujinasua na “burnout”
Funguka
Endapo hali hiyo inasababishwa na tabia za wakuu wako au wafanyakazi wenzio, unaweza kufungua moyo wako na kusema yanayokusibu.
Kukaa na jambo linalokukwaza moyoni, inaweza kukusababishia kuongeza msongo wa mawazo na tabia ya kuahirisha kazi zako.
Inashauriwa pale unapohisi kuna mtu anakukwamisha, umfuate mtu huyo na umwambie tatizo lake ili ajirekebishe.
TANGAZO:

Chukua “break”
Wakati mwingine ni kweli ubongo unakuwa umeganda na unahitaji “kubustiwa” kidogo.
Mkazi wa Dar es Salaam Edgar Buberwa, amesema anapokuwa ofisini na hali hiyo ikamkabili, huchukua maamuzi ya kutafuta sehemu ili apunge upepo kidogo kuipatia akili yake muda wa kupumua.
“Ninaweza kuchukua simu yangu nikaangalia vichekesho kwa kuda mfupi au nikaenda darini kupunga upepo,” amesema Buberwa.
Soma mafanikio ya wengine
Fahamu kuwa wewe siyo mtu wa kwanza kukutwa na hali hiyo. Wapo wengi tu waliotangulia na huenda waliweka mapito yao kwenye maandishi mtandaoni.
Kwa mwanahabari Goodluck Paul, amesema huchagua kuongea na mtu mwenye uzoefu wa kazi inayomtatiza au huingia mtandaoni kusoma jinsi watu wengine walivyofanya.
“Ninaingia mtandaoni nasoma wenzangu waliopitia hali hiyo walifanya nini au wataalamu wanasemaje,” amesema Paul.
Unahitaji muda wa kukaa pekee yako na kutafakari kuhusu maisha na mstakabali wa maisha yako. Picha| K15Photos.
Pumzika kidogo
Hata simu yako hupumzika baada ya kazi nyingi. Kama mashine inapumzika, kwanini wewe usipumzike?
Meneja rasilimali watu katika moja ya kampuni hapa jijini Dar es Salaam, Noela Mnyawa anasema akipatwa na hali hiyo hutafuta muda kwa ajili ya kupumzika ili akusanye nguvu zake tena.
“Pata muda ujichaji. Jaza kikombe chako kwani hauwezi kumhudumia mtu ukiwa na kikombe kitupu,” amesema Mnyawa kwa fumbo linalomaanisha ni muhimu kujijali ili wengine wakujali.
Weka mipaka kati ya kazi na maisha binafsi
Huenda huu ni msamiati kwa wengi kwani wapo ambao hata wakiwa nyumbani kwenye simu zao ni kazi, kazi na wao.
Kwa Wakili Neema Kibodya, yeye huweka mipaka kati yake na kazi. Akiwa kazini atafanya kazi na akiwa kwenye mapumziko atapumzika kweli.
Kwake hiyo humpatia nguvu mpya kila asubuhi.
“Wakati mwingine huwa naongea na rafiki au mama yangu au napanga safari naenda kwa ajili ya mapumziko,” amesema Kibodya.
Mambo mengine ambayo unaweza kuangazia ni pamoja na kufanya kitu unachokipenda ili urudi kwenye reli ikiwemo kusikiliza muziki huku ukitafuta suluhu ya changamoto yako.