Ujumbe wa Rais Samia kwa Watanzania baada ya kutoka Marekani
- Amesema Tanzania itatekeleza yote waliyokubaliana katika mkutano wa UN.
- Awataka Watanzani kushikamana kujenga nchi yao.
Dar es Salaam. Rais Samia amesema mambo yote ambayo Tanzania iliahidi katika mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA76) ikiwemo kuboresha utawala bora itayatekeleza kivitendo huku akiwataka Watanzania kushikamana ili kujenga Taifa lao.
Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Septemba 25, 2021 katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam akitokea nchini Marekani alipokuwa akishiriki mkutano huo.
Rais Samia amesema katika mkutano huo wakuu wa nchi wanachama wa UN wamejadiliana mambo makuu manne ambayo yanatakiwa kuwekwa katika utekelezaji ikiwemo namna dunia inavyoweza kuimarisha uchumi wake na kukabiliana na athari za Uviko-19.
Jambo lingine ni namna ya kuishinda Uviko-19, utawala bora na mabadiliko ya tabianchi.
“Niliahidi kwamba Tanzania tutayafanya yote haya, tuende nasi kama dunia inavyokwenda,” amesema Rais Samia na kuongeza kuwa, “kuzungumza katika taasisi kama ile ni jambo moja lakini kinachotakiwa ni utekelezaji wa yale tuliyoyazungumza.”
Kiongozi huyo mkuu wa nchi amesema akiwa katika mkutano huo aliuhakikishia ulimwengu kuwa Tanzania iko imara na itaendelea kufanya kazi na dunia katika masuala yote muhimu.
Aidha, amewaomba Watanzania kusimama pamoja na kushikamana kuijenga nchi yao ili kujiletea maendelea na kuendelea kushirikiana na jumuiya za kimataifa.
“Kwa hiyo niwaombe sana Watanzania wote tuungane, tushirikiane tufanye kazi pamoja kujenga Taifa letu ambalo kwa miaka 60 limekuwa likijengwa awamu na hatua mbalimbali,” amesema Rais Samia.
Ziara hiyo ya Samia inatajwa kuwa ni ya kihistoria kwa sababu kwa miaka sita Tanzania ilikuwa inawakilishwa na ngazi ya mawaziri katika mikutano hiyo ya kimataifa.
Pembeni ya mkutano huo, Rais Samia alikutana na viongozi mbalimbali wa nchi na taasisi za kimataifa akiwemo Rais wa Benki ya Dunia, David Malpass aliyekubali kuisaidia Tanzania kupata chanjo dhidi ya Uviko-19.
Latest
