Mwongozo ulipaji kodi kwa mashirika yasiyo ya kiserikali waja

September 30, 2021 8:37 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Imesema iko katika hatua za mwisho kuukamilisha.
  • Utasaidia kupunguza changamoto za kodi kwa mashirika hayo.
  • Rais Samia ayataka mashirika hayo kupunguza utegemezi.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali iko katika hatua za mwisho za kukamilisha mwongozo wa misamaha ya kodi kwa mashirika yasiyo ya kiserikali huku akiyataka mashirika hayo kupunguza utegemezi wa fedha kutoka kwa wahisani.

Rais Samia amesema zipo changamoto kwenye mifumo ya kodi kwa baadhi ya taasisi zinazostahili kupata msamaha wa kodi na tayari Serikali imeanza kufanyia kazi masuala yote hayo.

“Kuhusu msamaha wa kodi kwa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali ambayo yanafanya kazi kwa hisani tayari tumeshakamilisha kuandaa kitini kinachotoa mwongozo wa namna mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yatanufaika na misamaha ya kodi,” amesema Rais Samia.

“Tuko katika hatua za mwisho za kumalizia,” amesema kiongozi huyo mkuu wa nchi leo Septemba 30, 2021 aliposhiriki mkutano wa mwaka wa jukwaa la mashirika yasiyo ya kiserikali jijini Dodoma.

Huenda mwongozo huo utapunguza malalamiko ya baadhi ya mashirika yasiyo ya kiserikali kudaiwa kutozwa kodi wakati hayaingizi faida na yanategemea misaada ya washirika wa maendeleo.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, mwaka 2020 ulifanyika uchambuzi wa mapato na matumizi ya mashirika 803 na ilibainika kuwa mapato yalikuwa Sh1.2  trilioni na matumizi ni Sh1 trilioni.

Aidha, Rais ameyataka mashirika hayo kupunguza utegemezi na kubaki katika malengo ya kuanzishwa kwao ili kutimiza kwa ukamilifu ajenda za maendeleo.

“Nayahimiza mashirika yasiyo ya Serikali hususan ya ndani, kupunguza utegemezi. Ajenda za kidunia zinavyobadilika, wahisani wanabadilisha sera zao za kutoa fedha, unajikuta lile uliloanzishia taasisi, si kipaumbele kwao, mnajikuta hamna fedha za kujiendesha,” amesema Rais.

Pia ameyataka mashirika hayo kufanya kazi zinazoendana na tamaduni, mila, desturi na maadili ya Kitanzania.

Ameziagiza sekretarieti za mikoa na mamlaka za serikali za mitaa kutoa ushirikiano wa kutosha kwa mashirika hayo katika kutoa kwa wakati vibali vya utekelezaji wa miradi wanayoibuni ili kujenga Taifa kwa pamoja.

Kwa upande wa Tanzania bara, mashirika yasiyo ya kiserikali yaliyosajiliwa ni 11,603 na yametoa ajira za moja kwa moja 17,836.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW