Utafanya nini kama hakuna anayekuamini tena?
- Ni filamu ya “The Last Duel”, inayohusu kufa kwa uaminifu kati ya Marguerite na watu wake wa karibu
- Mumewe anaitumia vita kama njia ya kumtetea.
Dar es Salaam. Ilikuwa ni siku asiyokuja kuisahau Marguerite, kwani katika maisha yake hajawahi kuwaza kama ipo siku, kitu atachozungumza hakuna ambaye hatomwamini kwa kuwa alikuwa anapendwa na kuaminiwa na kila mtu akiwemo mume wake kipenzi Jean de Carrouges.
Mategemeo ya Marguerite yanaenda kombo siku ambayo anasimama mbele ya umati mkubwa na kueleza kwamba amebakwa na Jacques Le Gris, rafiki wa karibu wa mume wake.
Mmmh..ni sauti ambayo kila mtu kwenye umati ule aliitoa tena kwa kuangaliana na jirani aliyesimama naye kuonyesha kwamba ni kitu ambacho hakiwezekani.
Kwa namna Carrouges na Gris walivyokuwa wakiishi kama ndugu wa damu na kufuatana kila mahali kama kumbi kumbi ukizingatia kuwa wao ni wapiganaji wakubwa wanaotegemewa katika nchi yao, ni lini sasa Gris alipata muda wa kumbaka Marguerite ni swali ambalo hata mumewe hakuwa na jibu.
Pozi lote linamuisha Marguerite pale anapomuangalia mumewe na kuona kuwa hata yeye haamini kile anachokizungumza. Kkwa ambao imewahi kuwakuta wanajua uchungu wa kueleza jambo alafu hakuna mtu anayeonyesha dalili ya kukuamini, maumivu yake ni kama msumari wa moto kwenye kidonda.
Licha ya kuwa haamini kile mkewe anachozungumza Carrouges anaamua kufanya jambo.
Maamuzi yenye fumbo
Shutuma za Marguerite kwa Gris, zinapofikishwa katika mahakama kuu, hakimu anaonekana kutokumwamini Marguerite hata kidogo na kudai kuwa anayosema hayatoshi kuthibitisha kama Gris ana hatia.
Ndipo, Carrouges anaomba mpambano na Gris, na matokeo ya mpambano huo ndiyo yatumike kuthibitisha kama Marguerite anachozungumza ni kweli au la!
Carrouges anamwambia Marguerite “naweka maisha yangu rehani kwa ajili yako,” Picha|Screenrant.com.
Mbona ni balaa!, Gris ana kibarua cha kujitetea kwamba hana hatia huku Carrouges akiambiwa na hakimu endapo atashindwa basi mkewe ataadhibiwa kifo cha mateso mno.
Cha ajabu ni kwamba mpambano huo hautahusisha wawili hao tu, bali hadi majeshi yao, na kwa mantiki hiyo hatuwezi kuita mpambano wa kawaida, hii ni vita.
“Kuna kitu hakipo sawa hapa”, ni mawazo yanayopita katika kichwa cha Marguerite, kwanini mumewe afanye maamuzi makubwa hivyo kwa kitu ambacho tangu mwanzo alionesha kutokukiamini?
Anapojaribu kumuuliza mumewe kwanini amechukua ‘risk’ kubwa hivyo, Carrouges anajibu, “naweka maisha yangu rehani kwa ajili yako”, jibu hili linamfunua akili Marguerite na kuhisi kwamba kuna jambo mumewe anataka kulifanya kwa kivuli cha kumtetea.
Maamuzi ya Carrouges ya kuomba mpambano na Gris, yanapelekea vita kubwa inayoandikwa katika historia ya Ufaransa.
Najua utakuwa na hamu ya kujua ni nini kilichomsukuma Carrouges kufanya maamuzi ya hatari hivyo kwa sababuhaamini kile mkewe anachosema.
Bila kusahau shauku yako ya kutaka kujua kuwa ni nani atashinda katika vita hii ya kukatana shoka. Oktoba15 mwaka huu ni siku yako ya kujua yote hayo kupitia filamu hii ya The Last Duel, wazungu wanasema ‘save the date’ na mimi naongezea ‘save the money’ kwa ajili ya Popcorn na tiketi katika kumbi za filamu
Latest