Hatari inayowakabili wachimbaji wadogo Tanzania

October 12, 2021 11:25 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni wanaotumia kemikali ya zebaki bila tahadhari.
  • Kemikali hiyo ina madhara kiafya na mazingira.
  • Serikali yaingilia kati kwa kuweka mipango ya kudhibiti matumizi yake.

Dodoma. Ana miezi mitatu tangu aanze kazi katika mgodi wa dhahabu wa Chikoa uliopo nje kidogo ya jiji la Dodoma, lakini kazi anayofanya iwapo hatachukua tahadhari ipasavyo huenda ikaathiri maisha yake.

Mary Ndahani (51), ambaye anafanya kazi ya kuchenjua madini hayo baada ya kuchimbwa na wachimbaji wadogo katika mgodi huo, hutumia zebaki kutekeleza majukumu, jambo ambalo ni hatari kwa afya yake.

Uchenjuaji huo hufanyika kwa kutumia zebaki ili kukamatisha dhahabu na huusisha uchomaji wa mchanganyiko wa kemikali hiyo. Katika mchakato huo, dhahabu hutenganishwa kwa kuwa zebaki hugeuka mvuke na kutoweka angani.

Mary, mwenye mto mmoja na wajukuu wawili, alihamia katika mgodi wa Chikoa akitokea mgodi wa Nholi uliopo Wilaya ya Bahi mkoani hapa kwa matarajio ya kuongeza kipato.

“Hapa tunapata Sh200, Sh300 maisha yanaenda,” anasema Mary ambaye hana vifaa vya kujikinga ikiwemo kofia ngumu wala gloves mipira ya mkononi ya kujikinga na magonjwa na kemikali).

Hata wakati Mary akiendelea kupigania kesho yake katika mgodi huo wa wachimbaji wadogo wa dhahabu uliofunguliwa miezi sita iliyopita, hafahamu kuwa matumizi ya zebaki yanaweza kukatiza ndoto zake asipochukua tahadhari ya kujikinga.

“Nimeanza kufanya kazi hii mwaka 2017 na hiyo zebaki nashika tu sijaona madhara yoyote,” anasema Mary ambaye hajavaa barakoa kujikinga na vumbi.

Kwa mujibu wa uzoefu wake wa kutumia zebaki migodini, kemikali hiyo inaweza kumletea mtu madhara ikiwa ana kidonda kwenye mwili ambapo inaweza kuathiri mishipa ya damu. Uelewa wa Jane kuhusu Zebaki ni mdogo kiasi kinachoweza kumuongezea hatari ya kuathiriwa zaidi.

Hata wachimbaji wengine waliopo mgodini hapo, wamesema bado hawafahamu madhara ya zebaki kwa sababu hawajawahi kumshuhudia mtu akidhurika na kemikali hiyo. 

“Mimi kazi yangu ni kuchimba dhahabu wala sikamatishi zebaki na dhahabu, sijui madhara yake,” anasema Meshack Nathaniel, mchimbaji mdogo wa dhahabu mgodini hapo.

Matokeo mbalimbali ya utafiti yamebaini kuwa matumizi ya zebaki yana athari za muda mfupi na muda mrefu kwa mazingira na afya ya binadamu, mimea na wanyama ikiwa hakutakuwa na usimamizi mzuri.

Athari hizo hutokea wakati zebaki ikiyeyuka kwenye hewa, ikigusa ardhi au kuchangamana na maji hasa ya mtoni, ziwani na yanayotumiwa na binadamu katika shughuli mbalimbali.

Zebaki ni kimekali ambayo hutumika katika vifaa tiba kama vipima joto hospitalini, viwandani na tafiti mbalimbali zinazofanyika maabara.

Vifaa vya kuchechulia dhahabu katika mgodi wa Chikoa uliopo jijini Dodoma. Picha| Daniel Samson.

Moja ya vyanzo 10 hatarishi duniani

Zebaki inatajwa kuwa miongoni mwa vyanzo 10 hatarishi kwa afya ya binadamu duniani kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO). 

Zebaki ina athari mbalimbali za muda mfupi na mrefu kwa watu ikiwemo kusababisha saratani, kuharibu mfumo wa chakula na upumuaji na kuathiri ukuaji wa watoto tangu wakiwa tumboni.

Mkuu wa Afya Kazini kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Joseph Birago anasema hali hiyo inaweza kusababisha kuzaliwa mtoto mwenye ulemavu, uwezo mdogo wa kufikiri na kupoteza kumbukumbu.

Pia zebaki ambayo inaweza kuingia mwili kwa hewa au chakula inaathiri utendaji wa kingamwili, mapafu, ngozi, figo na moyo na kusababisha vifo.


Unaweza kupata mtindio wa ubongo

“Zebaki inaathiri mfumo wa neva wa namna gani mwili unavyoweza kujiendesha na kutenda. Neva zikiathiriwa na zebaki unaweza kushindwa kutafsiri baadhi ya vitu, hata unaweza ukapata mtindio wa ubongo ukubwani,” anasema Birago.

Anasema hakuna kipindi maalum ambacho madhara ya zebaki yanaweza kuonekana kwa mtu isipokuwa madhara mengi huwa ya muda mrefu na yanaweza kuhusisha vizazi vijavyo.

“Madhara yanaweza yasiwe kwa mtumiaji yakawa kwa kizazi chake. Kile kizazi kikiwa kimeathiriwa na zebaki kinakuwa na muendelezo kama ilivyo madhara ya mabomu ya nyuklia kwa Nagasaki na Hiroshima kule Japan,” anasema mtaalam huyo wa afya.

Madhara ya zebaki mwilini hutegemeana na namna mtu alivyo karibu na shughuli zinazohusisha kemikali hiyo na umri.

Dalili za athari za zebaki kwa mtu zinaweza kuwa kukosa usingizi, kumbukumbu, nguvu za kiume, maumivu ya kichwa na kifua.

Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 1997 inatambua athari za kimazingira na kiafya zinazotokana na matumizi ya zebaki katika shughuli za wadogo na hivyo kusisitiza usimamizi na udhibiti wa kemikali hiyo ili isilete madhara.


Ni hatari zaidi kwa mazingira

Utafiti wa Programu ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa (UNEP) wa mwaka 2018 umebaini kuwa wachimbaji wadogo wa dhahabu ni chanzo kimojawapo cha uchafuzi wa mazingira utakanao na zebaki duniani ambapo huchangia asilimia 30 ya uchafuzi wa mazingira.

Mratibu wa mradi wa kudhibiti matumizi ya zebaki kutoka Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC), Benjamini Mchwaupaka anasema kemikali hiyo husababisha uharibifu wa vyanzo vya maji, rutuba ya ardhi na uchafuzi wa hewa.

Uchafuzi huo hutokea wakati mialo ya maji yenye kemikali hiyo huelekezwa kwenye vyanzo vya maji na ardhi.

Mhandisi Mchwaupaka anasema zebaki ikiingia ardhini na majini inazoretesha ukuaji wa mimea na kusababisha vifo vya viumbe na hivyo kuharibu kabisa ikolojia ya eneo husika.

Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 inaelekeza kufanya tathmini ya athari za mazingira kwa wawekezaji na wachimbaji wa madini wakiwemo wachimbaji wadogo wa dhahabu katika maeneo ya miradi yao ili kuepuka uharibifu wa mazingira. 

Jinsi ya kujikinga dhidi ya zebaki

Wakati wadau na Serikali wakiendelea kutafuta mbadala wa zebaki, wachimbaji wadogo wa dhahabu wanatakiwa kuvaa vifaa maalum ikiwemo barakoa, gloves na viatu ambavyo vitawakinga wasiguse moja kwa moja kemikali hiyo wakati wakiendelea na shughuli za uchenjuaji wa madini.

Vifaa hivyo kusaidia zebaki isiguse ngozi au kuingia kwa njia ya hewa katika mwili wa mwanadamu na kuleta madhara.

Mtaalam wa mazingira kutoka Tume ya Madini Tanzania, Mhandisi Abel Madala anasema wachimbaji wanapopewa leseni hupewa masharti na miongozo ambayo ni pamoja na kuzingatia usalama mahali pa kazi ili kuwalinda wafanyakazi na hatari zinazoweza kuwapata.

“Uvaaji wa vifaa hivi unasisitizwa wakati wote wakiwa kazini na ukaguzi hufanyika mara kwa mara kuhakikisha vinakuwepo na wachimbaji wanavitumia kuepuka madhara kama ya zebaki,” anasema Mhandisi Madala. Eneo la mgodi wa Chikoa jijini Dodoma ambalo wachimbaji wadogo huchimba dhahabu na kisha kuichenjua na zebaki, jambo linalowaweka katika hatari ya kupata madhara ya kiafya. Picha| Daniel Samson.

Serikali inafanya nini kutomeza hatari hii? 

Kutokana na kubainika kwa madhara ya zebaki, Serikali imesema imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kusaini mikataba ya kimataifa ya kudhibiti matumizi ya kemikali hiyo. 

Tanzania imesaini Mkataba wa Minamata kuhusu Zebaki wa mwaka 2013 wenye madhumuni ya kulinda afya ya binadamu dhidi ya madhara ya uchafuzi wa mazingira unatokana na zebaki.

“Katika kutekeleza mkataba huu Tanzania ikiwa ni miongoni mwa nchi wanachama imeandaa mpango kazi kukidhi matakwa ya Mkataba wa Minamata na utakuwa ni wa miaka mitano kuanzia 2020 hadi 2025,” anasema Mkurugenzi wa Mazingira katika Ofisi ya Makamu wa Rais, Dk Andrew Komba.

Dk Komba anasema katika utekelezaji wa mpango kazi huo wanakusudia kupunguza matumizi ya zebaki katika sekta ya wachimbaji wadogo wa dhahabu kwa asilimia 30 na kukuza uelewa wa jamii ifikapo 2025.

Pamoja na kuwa na lengo kuu la kupunguza matumizi ya Zebaki vilevile unalenga kuendelea kuhamasisha matumizi ya teknolojia mbadala ili kupunguza changamoto za afya ya binadamu na mazingira kwa ujumla.

Aidha, Serikali imesema inafanya tathmini ya matumizi ya zebaki nchini ili kuweka usimamizi mzuri wa uagizaji wa kemikali hiyo nje ya nchi, jambo litakalosaidia kudhibiti matumizi holela ya kemikali hiyo kwa wachimbaji wadogo.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW