Miaka 22 bila Mwalimu Nyerere, wazee watoa ya moyoni
- Washauri Watanzania kuogopa rushwa na ufisadi.
- Mitaala ya elimu iwaandae vijana kuwa wazalendo kama Mwalimu Nyerere.
Mwanza. Wakati Watanzania wakiadhimisha miaka 22 ya kifo cha Baba wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, baadhi ya wazee wa Mkoa wa Mwanza wameshauri kumuenzi kwa kuboresha mitaala ya elimu na kuwaandaa vijana kuwa wazalendo kwa nchi yao.
Baadhi ya wazee maarufu jijini Mwanza wakizungumza na Nukta Habari (www.nukta.co.tz), wamesema kukua kwa teknolojia kumesababisha changamoto kwa vijana kutopata elimu stahiki inayowaandaa katika kukuza na kulinda rasilimali za Taifa.
Wameiomba Serikali iboreshe mitaala ya elimu mashuleni na ilenge katika uzalendo na maadili yatakayomwandaa kijana kuwa mzalendo anayejali maslahi ya Taifa.
Fellician Freemary, mkazi wa mtaa wa Nyegezi jijini Mwanza anasema katika utawala wa mwalimu Nyerere aliweka misingi ya elimu huku lengo lake likiwa ni kufuta ujinga.
“Alipenda watu wote wapate elimu, na alichukia rushwa, ni vema Serikali ikaweka mikakati ambayo itasaidia katika kuboresha mitaala ya elimu mashuleni ili watoto wajifunze maadili na kuchukia rushwa, somo hili likifundishwa toka mashuleni litasaidia kupunguza tatizo la rushwa nchini,” amesema Freemary.
Amesema mwalimu aliyefariki siku kama ya leo mwaka 1999 alichukia rushwa na alikuwa mkali kwa mtu ambaye alibainika kula rushwa huku akiwataka Watanzania kuiga mfano huo.
Freemary ametaja matabaka, ukabila na udini umeanza kurudi katika nyakati hizi kitendo ambacho huko nyuma kilikemewa vikali na mwalimu na viongozi waliopita katika mikono yake.
“Kutoka na hayo ndiyo maana tunashuhudia siasa za kurithishana pamoja na madaraka, hakuna ulazima wa kiongozi mkubwa kwenye nchi kumrithisha mtoto au mke wake uongozi wakati katika eneo hilo kuna vijana wamehitimu elimu miaka mingi na hawana kazi,” amesema Raphael Lwamba, mzee a makamo wa jijini hapa.
Lwamba ameeleza kwa sasa watu wamekuwa na tamaa ya mali na madaraka na wapo tayari kutoa gharama yoyote ili kupata vitu hivyo.
“Viongozi wawe madhubuti wawajibishe watu wanaooneka kwenda kinyume na sheria na taratibu za nchi, tuenzi misingi ya mwalimu kwa maendeleo endelevu ya Taifa letu,” amesema Lwamba.
Kifo cha Baba wa Taifa Julius Nyerere kilitokea Oktoba 14, 1999 katika hospitali ya Mtakatifu Thomas nchini Ungereza alipokuwa akipatiwa matibabu. Hata hivyo, falsafa na hotuba zake zimeendelea kuishi ndani na nje ya Tanzania.
Latest
