Wachimbaji wanavyotumia ‘gloves’ kujikinga na Uviko-19 Dodoma

October 14, 2021 6:38 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Baadhi ya wachimbaji wa madini wasema ukosefu wa maji unawazuia kujikinga na Uviko-19.
  • Watumia ‘gloves’ kuepuka maradhi hayo yanayozidi kuutesa ulimwenguni.

Dodoma. Katika mgodi wa Chikoa, nje ya jiji la Dodoma, shughuli mbalimbali zinaendelea mgodini hapa huku milio ya sauti za mitambo na mashine zikisikika kiasi cha kuzuia usikivu makini baina ya mtu na mtu. 

Kwa wachimbaji waliopo hapa Saa 5 asubuhi ni muda wa kazi haswa na kila aliyepo mgodini uliopo anapilika zake zikiwemo kubeba viroba vya mchanga wa dhahabu.

Licha bidii waliyonayo wachimbaji na watu wengine wanaotoa huduma ikiwemo ya chakula katika eneo hilo, uchukuaji tahadhari dhidi ya Corona (Uviko-19) hauzingatiwi. Maisha katika mgodi huo, uliopo mwendo wa saa 1:30 kutoka Dodoma mjini, ni kama Tanzania haikabiliwi na Uviko-19.

Waliovaa barakoa ni wachache huku suala la kunawa mikono na kuepuka mikusanyiko halipewi kipaumbele kutokana na baadhi ya wachimbaji kudai kuwa shughuli hizo wanazofanya zinawapa wakati mgumu kufuata tahadhari zote.

Mfanyakazi wa mgodi huo, Stanslous Matata anasema maji yakiwepo hunawa mikono lakini siyo wakati wote kwa sababu wana shughuli nyingi ambazo huwazuia kunawa mara kwa mara.

“Kiukweli watu hawazingatii (tahadhari), shughuli zetu ni nyingi unatoka hapa unaenda pale unajikuta kunawa haipo. Kama yapo maji tunanawa ila sema ndiyo hivyo tunatingwa,” anasema Matata ambaye kazi yake ni kupia rola mgodini hapo.

Hali hii ya kutofuata tahadhari ya Uviko-19 inafanana na migodi mingi nchini ya wachimbaji wadogo ambayo Nukta imeitembelea hivi karibuni ya Chitongo-Ishokela hela mkoani Mwanza na Nyarugusu uliopo Geita.

Mapipa ya maji yaliyopo katika mgodi wa Chikoa hutumiwa zaidi kuchenjua dhahabu na hivyo kuwakosesha wachimbaji kunawa mikono mara kwa mara, jambo linalowafanya watumie gloves kujikinga. Picha| Daniel Samson.

Tanzania ni miongoni mwa mataifa ambayo wagonjwa wa Corona vimezidi kuongezeka hasa katika wimbi la tatu. Shirika la Afya Duniani (WHO) linabainisha kuwa watu 25,957 wameugua Uviko-19 nchini Tanzania huku 723 wakipoteza maisha hadi Oktoba 10 mwaka huu. 

Waziri wa Afya, Dorothy Gwajima aliwaeleza wanahabari mapema juma hili kuwa Serikali imekuwa ikipeleka takwimu hizo kwa WHO kila wiki hivyo watu wote wanaweza kuona mwenendo wa hali ya Uviko-19 katika tovuti ya shirika hilo.

Matata anasema siyo kunawa mikono ni changamoto kwao, hata uvaaji wa barakoa ni wa nadra kwa sababu hutumia nguvu nyingi, hivyo huihitaji hewa ya kutosha hasa wanapokuwa chini ya mgodi. 

“Kazi hizi zinahitaji nguvu nyingi, nikivaa barakoa nitakosa pumzi,” anasema Matata, licha ya kuwa wataalam wa afya wanashauri uvaaji wa barakoa katika maeneo yote ya kazi ili kujikinga siyo tu na Uviko-19 hata magonjwa mengine.

Maji kikwazo kujikinga

Mchimbaji mwingine aliyejitambulisha kwa jina moja tu, John Kapei anasema eneo la mgodi halina chanzo cha maji, hivyo yanayoyapatikana husimamiwa vizuri ili kukamilisha kazi ya uchenjuaji dhahabu, jambo linalowafanya wasinawe mara kwa mara.

Wakati Matata na Kapei  wakikiri kuwa wamepata elimu ya kujikinga na Uviko-19 na wako tayari kupata chanjo ikiwa wataelezwa faida yake, Shani Mlowa, mama lishe katika mgodi huo anasema unausikia tu ugonjwa huo kwa watu. 

Taasisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya maji (UN Water) inaeleza kuwa ukosefu wa maji na vifaa vya kujisafi katika maeneo mbalimbali duniani ni kikwazo kwa watu kuchukua tahadhari dhidi ya Uviko-19.

Meneja wa mgodi huo, Zebedayo Machunde anasema changamoto waliyonayo ni upatikanaji wa maji ya uhakika mgodini hapo hasa kwa ajili ya wafanyakazi zaidi ya 20 waliopo.

Anasema hawana mabomba, jambo linalowafanya wanunue maji kutoka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Dodoma (DUWASA) ambayo huwasambazia kwa magari kutoka mjini.

Mmoja wa wafanyakazi katika mgodi wa Chikoa jijini Dodoma akiwa anaelkekeza namna wanavyochejua dhahabu na wakati huo huo wakijikinga na Uviko-19 kwa kuvaa gloves. Picha| Daniel Samson.

Gharama za maji vs uhai

“Maji hayo ambayo ni lita 2,000 tunanunua kwa Sh150,000 ambayo tunatumia siku mbili hadi tatu, kuna wakati mwingine maji yanakuwa yameisha,” anasema Machunde na kubainisha kuwa ubovu wa barabara nao huo huchelewesha maji kufika kwa wakati.

Anasema kutatua changamoto hiyo, wafanyakazi wamepewa gloves (mipira ya mkononi) ambazo huwasaidia kushika vitu na kwamba namna moja hujikinga na maradhi hayo. 

Hata hivyo, Nukta Habari (www.nukta.co.tz) ilipofika mgodi hapo ilishuhudia idadi ndogo ya wachimbaji ndiyo walikuwa wamevaa gloves huku wakisema zinawasaidia katika kutimiza majukumu yao.

“Gloves tunavaa lakini siyo wote, zinasaidia kujikinga na hatari hasa mikononi lakini inapunguza kunawa mikono mara kwa mara,” anasema Mary Ndahani, mfanyakazi katika mgodi huo.


Kisima kupunguza makali

Pia mgodi huo tayari umechimba kisima cha maji ambacho kitapunguza ghara za kuagiza maji mjini na hivyo kuwezesha upatikanaji wa maji wakati wote kwa wafanyakazi kunawa. 

“Tumeshachimba kisima, tumebakiza hatua chache tu tutakifungua kianze kufanya kazi na kuleta maji huku juu mgodini,” anasema Machunde.

Makala hii imefadhiliwa na Shirika la maendeleo ya habari la International Media Support (IMS) na Umoja wa Ulaya (EU).

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW