Inawezekana: Usawa wa kijinsia unavyoshamiri sokoni
- Wanawake wamejengewa uwezo wa kutambua haki zao.
- Ukatili dhidi yao umepungua kwa kiasi kikubwa.
- Sasa wamekuwa vinara wa kufanya biashara na kuingiza kipato.
Dar es Salaam. Miaka ya nyuma ilikuwa si rahisi kujitokeza na kuzungumza hadharani hususan na vyombo vya habari. Kwa wakati huo, aliamini kuwa muda aliyekuwa akipaswa kuongea ni mwanaume pekee kwa kuwa ndivyo alivyokuwa amezoea kuona kwenye jamii yake.
Hata hivyo, safari hii mambo ni tofauti. Akiwa kwenye harakati za kupanga mboga zake kwa ajili ya kuanza siku, alitamani kujua kinachoendelea baada ya kuona kamera ikichukua matukio katika eneo la soko.
Baada ya kusogea na kusikia mwenzake akitoa maoni juu ya jitihada na maendeleo ya wanawake katika soko la Kiwalani, haraka kwa ujasiri akaomba naye kuzungumza kiasi cha kuwashangaza wengi wakiwemo wanaume waliokuwepo sokoni hapo.
“Zamani uongozi wetu wote ulikua umeshikwa na wanaume, sasa hivi na sisi tumejua kumbe tunaweza kuongoza tukisaidiana nao,” anasema Sura Mweta mfanyabiashara wa mboga mboga katika soko la Kiwalani jijini Dar es Salaam ambaye pia ni katibu wa soko hilo.
Miaka sita iliyopita ilikuwa ni ngumu kumkuta mwanamke kama Sura katika nafasi za juu za uongozi sokoni. Hali hiyo si tu sokoni bali katika maeneo mengi hadi kwenye sekta rasmi na zisizo rasmi.
Ripoti ya Takwimu Muhimu za Tanzania ya mwaka 2017 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inabainisha kuwa pamoja na kwamba nusu ya kaya zilizopo nchini kuwa wanawake, bado ushiriki wao katika masuala ya uongozi ni mdogo kulinganisha na wanaume.
Ripoti hiyo inaonyesha kwa mwaka 2013 – 2014 nafasi za uongozi katika nyanja mbalimbali ikiwemo halmashauri za mtaa kwa wanaume ni asilimia 82 huku wanawake asilimia 18.
Hii ina maana kuwa kati ya kila viongozi wa mitaa 100, wanawake walikuwa 18 au moja ya tano ya nafasi zote, jambo linalowanyima fursa wanawake katika vyombo vya uamuzi.
Wanawake wamekuwa mstari wa mbele kufanya biashara sokoni baada ya kupewa elimu ya biashara. Picha | Gift Mijoe
Mbali na nafasi za uongozi, wanawake wamekuwa nyuma pia katika shughuli za kiuchumi kiasi cha kuwarudisha nyuma katika jitihada za kukabiliana na umaskini.
Eva Paschal (47), mfanyabiashara wa kanga na vitenge kwa takribani miaka 15 katika soko la Mchikichini lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam, anasema katika jitihada za kujitafutia riziki amekutana na maswahibu lukuki yanayokatisha tamaa baadhi ya wanawake.
Miongoni mwa matatizo ambayo amekuwa akikumbana nayo mama huyo, anayesaka pesa za kulea na kusomesha watoto wake, ni kunyang’anywa vizimba, kuambiwa lugha za matusi na mengine ambayo hakuwa tayari yaripotiwe.
Hata hivyo, angalau siku hizi yeye na wanawake wenzake kwa kiasi kikubwa wameweza kujikomboa kwa kujitambua baada ya kuanza jitihada za kutokomeza ukatili wa kijinsia uliokuwa umeshamiri sokoni na kuwakosesha fursa za kiuchumi na kijamii.
“Purukushani zipo ila kwa upande wetu elimu imetuweka imara,” anasema Eva na kubainisha kuwa wamekuwa wakipeana elimu juu ya namna ya kudhibiti ukatili huo na kuhakikisha hautokei tena.
Hali ilivyokuwa awali
Afisa Mradi kutoka Shirika la Equality for Growth (EfG), Susan Sitta anasema hali ilikuwa siyo ya kuridhisha kwa wanawake katika masoko mengi jijini Dar es Salaam kwa kuwa wengi walikuwa hawatambui haki zao za msingi na walikosa majukwaa ya kuongelea kero zao.
Susan, ambaye shirika lake ni moja ya wadau waliokuwa wakitoa elimu kwa wanawake kuhusu haki zao kupitia mradi “Sauti ya mwanamke sokoni”, anasema kwa sasa wanawake wengi wamepata mabadiliko ya kifikra na wanaweza kujipambania.
“Wakati tunaanza kufanya utafiti, hali ilikua ni mbaya hasa katika upande wa ukatili wa kijinsia maana utafiti wetu ulionyesha ni karibia asilimia 97 ya wanawake waliokua kwenye maeneo ya masoko walikua wanapitia ukatili wa kijinsia,” anasema Susan.
Ukatili uliokuwa unaongoza katika maeneo hayo ya biashara ni unyanyasaji, bugudha, lugha za matusi na rushwa ya ngono.
Baada ya kutolewa elimu hiyo kwa wafanyabiashara wa masokoni, heshima ya mwanamke imeanza kushamiri katika maeneo hayo.
Mwenyekiti wa soko la Kiwalani, Neema Charles katika shughuli zake sokoni. Picha | Gift Mijoe.
Hatua zitakazoendelea kuimarisha hali ya usawa masokoni
Mwenyekiti wa soko la Kiwalani, Neema Charles anasema licha ya mambo kubadilika kwa kiasi kikubwa, inahitajika elimu zaidi kuwafikia watu wengi ili kutokomeza kabisa ukatili dhidi ya wanawake.
“Hatutaishia hapa. Ni jukumu letu na watoa elimu kuzidi kusukuma hili gurudumu ili tufike mahali tunapotaka kufika,” anasema Neema huku akitaka nguvu zaidi ielekezwe kuwawezesha wanawake kiuchumi ikiwemo kuwapa mbinu za kufanikiwa kibiashara.
Hata hivyo, wadau ikiwemo Serikali wanasema wataendelea kufikia wajasiriamali wengi zaidi masokoni kuwapa elimu hasa wale ambao haijawafikia wawe sehemu ya kukabiliana na ukatili wa kijinsia.
“Ni matazamio yetu tutakaporudi tena kuwaongezea elimu juu ya mambo ya msingi ya kuzingatia ili kukomesha ukatili wa kijinsia, itakua ni mwanzo wa kupata jamii ya wanawake wanaojitambua,” anasema Susan.
Wanawake waliopo katika masoko ya Ilala wanasema licha ya elimu hiyo kuwafaidisha wangependa iwafikie pia wanawake wengine majumbani ili nao wajengewe uwezo wa kukabiliana na ukatili wa kijinsia.
“Nilivyomsaidia ndugu yangu kupata haki yake, alinishukuru na kushangaa iwapo haya mambo yanawezekana. Aliniambia ikiwezekana tuombe elimu kama hii isiishie masokoni tu, hata wanawake waliopo mtaani wanufaike nayo,” anasema Sura Mweta, Katibu wa soko la Kiwalani, Manispaa ya Ilala.
Kaimu Mkurugenzi Manispaa ya Ilala Tabu Shaibu ameiambia Nukta (www.nukta.co.tz) kuwa Serikali inaendelea na utekelezaji wa maboresho ya maeneo ya kazi hasa masokoni ikiwemo kuunga mkono juhudi zinazofanywa na wafanyabiashara wakiwemo wanawake kujiendeleza.
“Serikali imeweka mipango ya uendelezaji wa masoko. Moja ya mipango ni kuwezesha wanawake kupitia vikundi vyao pamoja na kuunga mkono juhudi wanazofanya kuchochea maendeleo,” anasema Shaibu.
Latest
