Ngono zembe, mashindano yachangia wanawake kuzaa watoto wengi Mwanza
- Baadhi ya wanawake wanasema ni fahari kuwa na watoto wengi.
- Umaskini wa kipato na ukosefu wa elimu nao wachangia.
- Hali hiyo inawaweka katika hatari ya vifo, kupata magonjwa ukiwemo Ukimwi.
Mwanza. Abrina Mugalura (45) ni mzaliwa wa Kyela mkoani Mbeya, alifika katika kisiwa cha Nafuba wilayani Ukerewe tangu mwaka 2000. Aliwasili katika kisiwa hicho kutafuta ridhiki ili kukidhi mahitaji yake ya kila siku.
Akiwa na miaka 24, Abrina (si jina lake halisi) aliamua kuanza shughuli ya kusafirisha samaki kutoka Ukerewe kwenda katika Mikoa ya Mbeya na Dar es Salaam.
Changamoto ya kuibiwa mtaji wake ilibadilisha historia ya maisha yake na kujikuta amezama kwenye mahusiano ya kimapenzi na wanaume mbalimbali ili tu aweze kutimiza mahitaji yake ya kila siku.
Anasema baada ya mtaji wake kuibiwa alianza kufanya vibarua vya hapa na pale ambavyo havikuweza kukidhi mahitaji ya kila siku ndipo alipoanza kutembea na wanaume hasa wavuvi kisiwani hapo.
“Unajua huku visiwani ni vema uwe na shughuli za kufanya vinginevyo utaishia kujiingiza kwenye mapenzi kwa kuwa kazi za visiwani ni kuuza samaki, kulima tofauti na hapo unaweza kushinda njaa,” anasema Abrina.
Mama huyo ni miongoni mwa baadhi ya wanawake wa kisiwa hichi ambao wamezaa watoto wengi kutokana na kuuza miili yao ili kujipatia kipato.
Katika maeneo mbalimbali ya Ukerewe ambako Nukta Habari (www.nukta.co.tz) pia imetembelea katika visiwa vya Ukara na Nakatunguru wilayani Ukerewe pamoja na kisiwa cha Mchangani wilayani Sengerema imekutana na kaya ambazo zinaongozwa na wanawake huku baadhi ya kaya zikiwa na watoto zaidi ya watano.
Sababu kubwa ni kuwa mama zao wanazaa na wanaume tofauti na kujiweka katika hatari za kiafya na kubeba mzigo mzito wa malezi ya watoto walio mbali na baba zao.
Hali hiyo huchochewa pia na kukosa ajira za kudumu ambazo zinawafanya wanawake kupata kipato cha uhakika kuendesha maisha yao, jambo linalotoa mwanya kwa baadhi ya wanaume hasa wavuvi kuwatumia kama ‘vyombo vya starehe.’
“Huku muda wote wanashiriki mapenzi, wavuvi wakitoka ziwani wakifika kazi yao ni kulala na wanawake ndani, na wanawake wengine huwa na tabia ya kuwapanga wanaume mstari akitoka huyu anaingia mwingine yaani ni uchafu,” anasema Abrina mwenye watoto sita.
Wanawake waliofika katika Kituo Cha Afya cha Kangunguli, Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza kupata matibabu. Picha| Mariam John.
Ni zaidi ya kutafuta pesa
Mkazi katika kisiwa cha Nakatunguru wilayani Ukerewe, Salome Baltazari anasema wanawake katika maeneo haya wanaamini mayai ya uzazi waliyopewa na Mungu yanatakiwa yatumike yote yaishe.
Salome mwenye watoto nane anasema wanazaa kwa mashindano na katika familia ambayo ina watoto wachache mama mwenye familia huwa na huzuni.
“Tunazaa ili kupata watu wa kutusaidia huko mbele wakati nguvu za kufanya kazi zimepungua, yaani ni kama tunazaa kwa mashindano ukiona familia ina watoto watatu unatamani na wewe uzae ifikie idadi hiyo,” anasema Salome.
Wanawake wenye watoto wachache huchekwa na kuchukuliwa kama hawatumii vizuri miili yao ili kupata watoto wengi.
Sababu nyingine zinazochangia uzazi usio na mpangilio ni pamoja na ukosefu wa elimu ya matumizi ya njia za uzazi wa mpango ambazo humsaidia mwanaume na mwanamke kupanga idadi kamili ya watoto watakaozaa.
“Yaani tunajiachia tu, sasa hizo njia zinafanya usizae watoto wengi. Tukienda hospitali wanatufundisha kuzaa kwa mpango lakini hatufuati,” anasema Mwajuma Abdallah, mkazi wa Nansio, Ukerewe.
Hatari iliyopo mbele yao
Wakati wanawake wakizaa kwa mashindano na kukosa elimu ya uzazi wa mpango visiwani humo wanajiweka katika hatari kubwa ya kupata matatizo ya kiafya, kubeba mzigo mzito wa kulea watoto na kuendelea kuogelea katika lindi la umaskini.
Kwa mujibu wa wataalam wa afya likiwemo Shirika la Afya Duniani (WHO), mama aliyejifungua mtoto anashauriwa kusubiri angalau mwaka mmoja kabla ya kupata ujauzito mwingine ili kupunguza hatari ya kupata matatizo ya uzazi na malezi
Matatizo hayo ni pamoja na kuvuja damu nyingi na vifo kwa wajawazito na watoto wachanga.
WHO inaeleza kuwa wanawake walio na miaka zaidi ya 35 waliopata ujauzito miezi sita baada ya ujauzito mwingine wanakua katika hatari ya kupoteza maisha kwa asilimia 1.2 sawa na vifo12 kwa kila mimba 1000.
Pia wastani wa vifo 562 vya uzazi katika kila vizazi hai 100,000 hutokea kila mwaka katika nchi zinazoendelea duniani ikiwemo Tanzania kutokana na sababu mbalimbali.
Licha ya madhara hayo ya uzazi, pia kushiriki ngono zembe bila kinga, kunawaweka wanawake hao katika hatari ya kuambukizwa magonjwa ya zinaa kama kaswende na hata kupata maambukizi ya virusi vya Ukimwi (VVU).
Matokeo hayo huongeza mzigo kwa Serikali na jamii kuwahudumia wagonjwa na kutumia kiasi kikubwa cha fedha ambacho kingeelekezwa katika shughuli za maendeleo.
Wavuvi katika kisiwa cha Kakukuru wilayani Ukerewe wakiendelea na shughuli mbalimbali mwambao wa Ziwa Victoria. Picha| Mariam John.
Baadhi ya wanaume ambao wanawazalisha wanawake na kuwatelekeza wanaeleza kuwa hufanya hivyo siyo kwa kupenda kwa sababu shughuli zao siyo za kutulia sehemu moja hivyo hujikuta wakilala na wanawake tofauti.
“Sisi shughuli zetu ni za kuzunguka, sasa ukipata mtu unashiriki tu tendo la ndoa na mnaachana na anaenda kwa mwingine, hata mtoto akizaliwa inakuwa ni ngumu kumjua baba,” anasema Silas Bwire, mvuvi katika kisiwa cha Ukara.
‘Kasi imepungua’
Balozi wa nyumba 10 katika kisiwa cha Nafuba wilayani Ukerewe, Charles Itemi kwa sasa matukio ya wanawake kuzaa watoto wengi bila mpangilio yamepungua kwa sababu elimu ya uzazi inawafikia katika maeneo yao.
Anasema uwepo wa watoto wengi mitaani pia huchangiwa na mimba za utotoni kwa wasichana ambao wanashindwa kuendelea na masomo ya shule za msingi na sekondari.
“Tena kwa sasa hali imepungua zamani ukifika katika eneo hili unakuta idadi kubwa ya watoto kwa kuwa wasichana wadogo waliokuwa wanatoka maeneo mengine wakifika visiwani wanabebeshwa mimba wanashindwa kufanya shughuli zilizowaleta hivyo shughuli yao kuu inabaki kuzaa tu,” anasema Itemi.
TANGAZO
Serikali, wataalam wa afya watoa kauli
Mwenyekiti wa kijiji cha Kangunguli wilayani Ukerewe, Antony Billi anasema kwa sasa wanatumia mikutano ya vijiji kutoa elimu kuhusu kujenga familia bora ambazo zinazingatia malezi mazuri ya watoto.
Anasema pia katika kijiji chake hufanya utambuzi wa watu wanaoingia na kutoka ili kudhibiti vitendo baadhi ya wanaume kuwazalisha wanawake na kushindwa kuwalea watoto wao.
Mganga Mfawidhi katika kituo cha afya Kangunguli, Paschal Peter anasema wamekuwa akitoa elimu kwa wanawake wanaofika kituoni hapo umuhimu wa kutumia njia za uzazi wa mpango na kuepuka kuzaa watoto bila mpangilio ili kuepuka madhara.
“Wataalam wa afya tunajitahidi kuhakikisha elimu inawafikia ili waweze kupanga uzazi na kupunguza matatizo yanayoweza kusababishwa na uzazi kwenye umri mdogo kama kifo,” anasema Dk Peter.
Mratibu wa huduma ya afya ya uzazi na mtoto mkoani Mwanza, Cecilia Mrema anasema msisitizo uliopo kwa sasa ni kuhimiza matumizi ya njia za uzazi wa mpango hasa kwa wanawake ili kuwaepusha na mimba zisizotarajiwa.
Anasema katika maeneo visiwa ambako kuna matukio mengi ya ngono zembe wamekuwa wakigawa kondomu ili kuwakinga watu na magonjwa ya kujamiana na hata mimba.
Pia wameweka vituo vya ushauri nasaha kwenye zahanati ili mzazi aweze kupata nasaha kabla na baada ya kujifungua.
Kutokana na jitihada hizo, Mrema anasema Ukerewe inaongoza kwa matumizi ya njia za uzazi wa mpango kwa asilimia 48 katika Mkoa wa Mwanza ikifuatiwa na jiji la Mwanza kwa asilimia 43 hadi Desemba 2020.
Mtaalam huyo wa afya anaamini kuwa hiyo itasaidia wanawake kujitambua na kupanga uzazi na kuzaa watoto kwa mpangilio huku wakilinda afya zao.
Latest



