Tanzania itakavyofaidika na mfumo wa anuani za makazi
- Utaisaidia kupanga mipango ya maendeleo, kuimarisha usalama, kuongeza ajira na mapato ya Serikali.
- Utasaidia kuchochea biashara ya mtandaoni.
- Pia utatumika katika Sensa ya watu na Makazi mwaka 2022.
Dar es Salaam. Spika Mstaafu wa Bunge la Tanzania na Kamisaa wa Sensa ya watu na Makazi, Anne Makinda amesema mfumo wa anwani za makazi utaisaidia kupanga mipango ya maendeleo, kuimarisha usalama, kuongeza ajira na mapato ya Serikali.
Makinda ameyasema hayo leo Desemba 4, 2021 wakati akizindua mfumo huo katika viwanja vya shule ya msingi Buhongwa B, kata ya Mkolani Wilaya ya Nyamagana Jijini Mwanza.
“Nazipongeza Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, TAMISEMI, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na wadau wote kwa ushirikiano wao na jitihada walizoweka ili kuhakikisha mfumo wa anwani za makazi unatekelezwa katika nchi nzima,” amesema.
Aidha, amesema mfumo huo utaendana na programu tumizi (mobile application) ya mfumo wa anwani za makazi ambayo itakayorahisisha ukusanyaji taarifa za barabara, wakazi, makazi pamoja na kutoa anwani za makazi ya wananchi, kaya, ofisi na eneo la biashara.
“Nimeelezwa kwamba programu tumizi imetengenezwa na wazawa, nitumie fuarsa hii kuwapongeza wataalamu wetu walioshiriki kuunda programu hii, hongereni sana vijana wetu, hili ni jambo la kujivunia sana kwani lengo la Serikali ni kuhakikisha wanatumika katika kuleta maendeleo ya taifa letu,” amesema Makinda.
Aidha, Makinda amesema kwa kutumia utaratibu huu wa anwani za makazi utasaidia katika Sensa ya Watu na Makazi ya mwakani kufanyika vizuri kwa sababu pia itaonyesha wananchi wanapokaa na wanafanya kazi gani.
Anuani za makazi zinasaidia kurahisisha shughuli za biashara na usafirishaji na hivyo kuwawezesha vijana wawaofanya biashara mtandao kuwafikia kirahisi wateja.
Spika mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kamisaa wa Sensa ya watu na makazi, Anne Makinda akimkabidhi Mkazi wa Nyamagana, Sophia Kyabwene kibao chenye anwani za makazi jana katika uzinduzi wa matumizi ya mfumo wa anwani za makazi jijini Mwanza. Picha| Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Ashatu Kijaji amesema mfumo huu wa anwani za makati ni mfuo mama wa mifumo mingi ya utambuzi.
“Watanzania wamekuwa wakilalamika kuwa na mifumo mingi midogo midogo ambao inayowataka kujisajili na hivyo mfumo huu tumeweza kuunganisha na mifumo mingine kama ya afya, NIDA, mfumo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania kwenye TIN namba, kusajili makampuni BRELA na mfumo wa usimamizi wa viwanja,” amesema Dk Kijaji na kuongeza kuwa,
“Kama Wizara inayosimamia mifumo yote ya Mawasiliano tumekuja na mfumo huu ili turahisishe maisha ya watanzania kwenye kuyaendea maendeleo ya mapinduzi ya nne ya viwanda, lengo kuu ni kuondoa usumbufu na malalamiko ya watanzania.”
Ameongeza kuwa mwaka huu ni dhamira ya Wizara kila mwananchi anakuwa na anwani yake ya makazi katika eneo analoishi, eneo la ajira au eneo la biashara.
Aidha, ametoa wito kwa watendaji, viongozi na wataalamu hususani wa kata na mitaa kujengewa uwezo wa kutosha ili waweze kuwa na uelewa wa pamoja, waweze kuratibu, kusimamia na kutekeleza mfumo huu.
Naye Naibu Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula amesema katika utekelezaji wa mfumo huu wa anwani za makazi Wizara yake ni mdau mkubwa katika kuandaa ramani za kidijitali ambazo hutumika kama ramami za msingi katika utekelezaji wa anwani za makazi.
“Bila kuwa na anwani hizi za kidijitali utekelezaji wake unaweza usiwe rahisi sana kwa sababu tunawatambua watu wetu na maeneo yao kwa kufuata mfumo huu nitoe taarifa kuwa ni halmashauri tisa ziko tayari ambazo maandalizi ya ramani husika yamekamilika,” amesema.
Latest