Rais Samia asitisha mikataba ujenzi meli tano Ziwa Victoria, vigogo matumbo joto

December 4, 2021 9:18 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni baada ya kubaini mkandarasi hana uwezo kujenga meli hizo.
  • Vigogo waliopitisha tenda ya ujenzi huo kuwekwa kiti moto.
  • Rais asema hatavumilia kuchezewa kwa fedha za Serikali.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesitisha utekelezaji wa mikataba mitano ya ujenzi wa meli tano katika Ziwa Victoria kutokana na mapangufu mbalimbali ikiwemo uwezo mdogo wa mkandarasi huku akiagiza hatua zichukuliwe kwa vigogo waliopitisha tenda ya ujenzi wa meli hizo.

Juni 15, 2021, Rais Samia Suluhu Hassan, akiwa jijini Mwanza alishuhudia utiaji saini wa mikataba mitano kwa ajili ya ujenzi wa meli mpya nne pamoja na ukarabati wa meli moja ya abiria uliofanywa na Serikali kupitia Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) na mkandarasi wa kampuni ya Yücel Tekin Shipbuilding Company (YÜTEK) kutoka nchini Uturuki.

Mikataba hiyo mitano iliyosainiwa ilikuwa ina thamani ya Sh438.8 ambayo ni mkataba wa ujenzi meli mpya ya mizigo yenye uwezo wa tani 2,800 itakayotoa huduma katika Bahari ya Hindi na meli mpya ya mizigo yenye uwezo wa tani 3,000 itakayotoa huduma Ziwa Victoria.

Mkataba mwingine ulihusu meli mpya ya mizigo yenye uwezo wa tani 2,800 itakayotoa huduma Ziwa Tanganyika, meli mpya itakayobeba abiria 600 na mizigo tani 400 itakayotoa huduma Ziwa Tanganyika pamoja na mkataba wa ukarabati wa Meli ya MV Umoja inayotoa huduma katika Ziwa Victoria.

Hata hivyo, leo Desemba 4, 2021, Rais Samia ameweka wazi mapungufu yaliyobainika katika mkataba huo na kuwa Serikali haiweze kutoa fedha hizo kwa sababu mashaka ni mengi juu ya utekelezaji wake.

Amesema katika kufuatilia utekelezaji wa mikataba ya ujenzi wa meli hizo mambo kadhaa yamejitokeza ambayo yanatia mashaka na kuna harufu ya ufisadi ambao unataka kufanywa na baadhi ya Watanzania kwa kushirikiana na makampuni ya nje. 

“La kwanza tuliona ndani ya mkataba ule tuliona huyu mkandarasi ana wakala yupo Tanzania ambaye wakala yule anatakiwa kulipwa Dola za Marekani milioni 2 (Sh4.6 bilioni) kwa kila meli tutakayoijenga. Meli ya chini ilikuwa dola milioni 1.9 (Sh4.4 bilioni) pamoja na vimalipo vidogo vidogo vinakwenda kwa wakala,” amesema Rais leo wakati akizindua maboresho ya gati namba 0 hadi 7 katika Bandari ya Dar es Salaam. 

Amesema kazi za wakala huyo ilikuwa kufuatilia tenda zitakazotoka Tanzania, kuomba tenda, kujaza nyaraka za tenda na mambo mengine huku malipo yake yakiwa na utata kwa yanayotokana na kila meli  inakayotengenezwa.

Hatua zilizochukuliwa ilikuwa kumtafuta wakala huyo ambaye hajatajwa jina pamoja na mkandarasi na baadaye walikubaliana wakala aondolewe kwenye majukumu ya mradi huo kwa sababu hana tija yoyote.

Rais  Samia Suluhu Hassan, akishuhudia utiaji saini wa mikataba ya ujenzi na ukarabati wa meli za Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), uliofanyika mkoani Mwanza Juni 15, 2021. Mikataba iliyosainiwa inahusisha ujenzi wa meli mpya ya abiria na mizigo Ziwa Tanganyika, ujenzi wa meli ya mizigo Ziwa Tanganyika, Ujenzi wa meli ya mizigo Ziwa Victoria, ujenzi wa meli ya mizigo Bahari ya Hindi na ukarabati wa meli ya MV Umoja. Picha| Ikulu.

Kiongozi huyo mkuu wa nchi amesema suala la pili walilobaini katika mkataba huo ni matayarisho ya ujenzi wa meli hizo yalikuwa yanatia mashaka kwa sababu mkandarasi hakuoneka kuwa yuko tayari kujenga meli hizo.

“Kutokana na wasiwasi uliotokana na Serikali tukaamua kuunda timu ya wataalam kutoka sekta mbalimbali kutoka Wizara ya Ujenzi, mjumbe kutoka Wakili Mkuu wa Serikali, Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), mjumbe mwingine tukamtoa jeshini kitengo cha meli,” amesema.

Timu hiyo ilikwenda nchini Uturuki kufuatilia hali na hadhi ya mkandarasi ambapo walibaini kuwa kampuni ya haina eneo la ujenzi wa meli badala yake imekuwa ikipata zabuni na wao ni madalali.

Rais amesema kampuni hiyo uwezo wa kifedha ni mdogo mno kwa sababu hadi timu hiyo inaondoka Uturuki haikotoa taarifa yao ya fedha walizonazo.

“Lakini jingine, wasifu wa kampuni na uwezo wake katika ujenzi ni wa mashaka kwani haipo hata kwenye orodha ya wajenzi wa meli inayotolewa na Umoja wa Wajenzi wa Meli nchini Uturuki,” amesema Rais.

Pia kampuni hiyo inadaiwa kuwa haina wafanyakazi wenye sifa za ujenzi wa meli na wala haina mitambo ya kujenga meli. 

Aidha, taarifa za Serikali zinaonyesha kuwa hadi sasa kampuni hiyo haijafanya jambo lolote tangu uliposainiwa mkataba zaidi ya miezi mitano iliyopita.

Rais Samia Suluhu Hassan akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari (TPA) Eric Hamissi kuhusu Ujenzi wa gati namba 0 – 7 kabla ya kuzindua rasmi kwa ajili ya matumizi katika hafla iliyofanyika katika Bandari ya Dar es Salaam leo Desemba 4, 2021. Picha| Ikulu.

Vigogo wa MSCL mashakani

Licha ya mkataba huo wenye mashaka, tenda ya kutengeneza meli hizo ilipitishwa na Bodi ya Tenda na Bodi ya Wakurugenzi ya MSCL ambayo ina wataalam wa masuala ya meli baada ya kujiridhisha kuhusu uwezo wa mkandarasi huyo.

“Sasa haya tumeyabaini hivi karibuni, huko nyuma yametokea mangapi?,” ameuliza Rais huku akimuagiza Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbalawa kulishughulikia suala hilo kwa kuchukua hatua stahiki kwa bodi zilizopitisha tenda na mkataba huo.

Aidha, tayari Raia Samia amesitisha mkataba huo ili kunusuru fedha zilizopangwa kutekeleza mradi huo ambazo zingeingia katika mifuko ya watu wachache.

“Kinachosikitisha ni mwananchi wa ndani anashikiliana na mtu wa nje kuchepusha fedha zote hizi ambazo zingekwenda kutekeleza maendeleo ya wananchi wanyonge kule chini,” amesema Rais.

Amemtaka Waziri Prof Mbalaw kufanya marekebisho makubwa ndani ya wizara yake hasa katika uwazi na ubora wa miradi inayotekelezwa ili kuepusha upotevu wa mapato.

Rais Samia alitengua uteuzi wa Waziri Mhandisi Dk Leonard Chamuriho Septemba 12, 2021 kwa kile kilichodaiwa kutoridhishwa na utendaji wake wa kazi na kumteua Prof Mbalawa.

Kutokana na changamoto hizo, wananchi ambao wangefaidika na ujenzi wa meli hizo watalazimika kusubiri mpaka mkandarasi mwingine atakapopatikana, jambo ambalo linaweza kuwafanya wakose huduma muhimu za usafiri wa majini zinazotumika katika shughuli mbalimbali ikiwemo biashara.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW