Corona ilivyowafungulia fursa za kibiashara wanamuziki Zanzibar

December 14, 2021 3:56 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni baada ya shughuli za muziki kusimama kwa muda.
  • Baadhi waliingia katika biashara za mavazi na nguo.
  • Serikali yaungana nao kuwainua kimuziki ikipambana na Corona.

Zanzibar. Ni kawaida kwa hoteli za Zanzibar kuwa na vipindi vya burudani kwa wageni wake. Mara nyingi huwa muziki wa “live” ambao huhusisha wanamuziki wa Taarab na miondoko mingine.

Vijana wenye vyombo vya muziki adimu kama filda, oud, magitaa, vinanda na dufu huhusika katika hafla hizo za kuwakaribisha watalii kwa muziki wa mwambao ambao umekuwa ni sehemu ya wasanii mashughuli akiwemo marehemu Bibi Kidude, Mzee Yusufu na wengine wengi.

Hata hivyo, kazi za muziki visiwani humo zilisimama kwa muda baada ya ugonjwa wa Corona (Uviko-19) kuingia Tanzania Machi 2020 na mipaka ya nchi mbalimbali kufungwa hivyo kuiziba mifereji iliyokuwa ikiingiza watalii nchini.

Kwa mujibu wa ripoti ya 16 ya hali ya uchumi Tanzania ya Julai 2021 ya Benki ya Dunia, kasi ya ukuaji uchumi visiwani Zanzibar ilishuka hadi asilimia 1.3 kutokana na kushuka kwa shughuli za kitalii ambapo kiwango cha utoaji huduma za malazi (Occupancy rate) kilishuka karibu kufikia asilimia 0 katika kipindi cha Machi hadi Septemba 2020.

Hali hiyo imeathiri wanamuziki wa Taarab na miondoko mingine visiwani humo kwa kuwa wengi hufanya kazi zao katika hoteli ambazo huendeshwa kwa uwepo wa watalii. 

Kati yao ni Jessica Mtoi mwanamuziki wa miondoko ya “soul”, “jazz” na “sweet reggae”.

Muziki unaofanya Jessica ni ule wa kuingia makubaliano maalum na baadhi ya hoteli na migawaha ili kutoa burudani mubashara kwa wateja wao hasa watalii wa kimataifa.

“Hoteli zilifungwa na mimi nilikosa kabisa kazi za muziki. Ningeweza kubaki Zanzibar kuendelea na shughuli zingine lakini niliamua nirudi nyumbani Dar es Salaam,” anasema Jessica ambaye kwa sasa amerejea tena Zanzibar kuendeleza maisha.

Baada ya kuona kazi yake ya muziki imeingia mchanga, binti huyo akiwa Dar es Salaam alikuwa anajishughulisha na biashara ya kuuza viremba, tai na nguo za malighafi ya kitenge kupitia biashara yake aliyoiita Vosso Designs.

Licha ya kurejea Zanzibar, anaendelea na biashara yake ikizingatiwa kuwa shughuli za utalii bado hazijaimarika kama ilivyokuwa awali. Ni sawa kusema Uviko-19 umemfungulia fursa nyingine ya kujiingizia kipato. 

“Imenibidi nianze kufanya matangazo zaidi ili niwafikie Wazanzibari na watu wa bara pia. Walau naona kuna muamko na wateja wapo,” amesema Mtoi akielezea biashara yake ya mavazi.

Baada ya Uviko kuathiri muziki wa Jessica Mtoi, aliamua kugeukia biashara ya kufunga viremba. Picha| Jessica Mtoi.

Shirika la Utalii la Umoja wa Mataifa (UNWTO), limeeleza kuwa idadi ya watalii wa kimataifa imepungua kwa asilimia 73 kwa mwaka 2020, huku kwa miezi mitano ya mwanzo ya mwaka 2021, watalii wamepungua hadi milioni 147 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2020.

Hata hivyo, UNWTO imesema sekta ya utalii duniani itaimarika kwa asilimia 60 ifikapo mwaka 2022, huku Afrika, sekta hiyo ikitarajiwa kuimarika kwa asilimia 73.

‘Fursa zaidi’

Wakati Jessica akigeukia biashara ya mavazi kujinusuru na athari za Uviko-19, wengine wameanzisha biashara za kuuza vyakula ikiwemo ubuyu ambayo ni tunu ya Zanzibar.

Ukipita baadhi ya mitaa ya Kariakoo, jijini Dar es Salaam utakutana na wauzaji wa “ubuyu wa Babu Issa”. Huo ni ubuyu kutoka Zanzibar.

Mwalimu wa ala kutoka Chuo cha Muziki Zanzibar, Tryphone Evarist Tryphone naye alikataa kubaki nyuma na sasa anajihusisha na uuzaji wa ubuyu ili kujipatia kipato kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya familia. 

Mbinu aliyokuwa akitumia Tyrphone kuuza ubuyu ni kupitia mitandao ya kijamii ya watu anaowafahamu na kisha kuwasambazia popote walipo visiwani humo.

“Nilikua nafunga ubuyu na nawauzia watu wangu wa karibu. Ilinisaidia kupata fedha ya kupeleka siku,” anasema Tryphone.

Mwalimu huyo wa muziki mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka miwili ameanza kurejea taratibu katika shughuli zake baada ya watalii ambao ndiyo wateja wake wakuu kuanza kuingia Zanzibar. 

Mambo bado hayajachanganya

Huenda kampeni ya utoaji chanjo ya Uviko-19 inayofanyika duniani kwa sasa itasaidia kuimarika kwa shughuli za muziki na kuwapatia kipato wasanii ambao maisha yao yanategemea muziki. 

Mpiga ala wa Taarab kutoka Chuo Cha Muziki Zanzibar, Hassan Abrahmani, kabla ya Corona alikuwa na uhakika wa kupata Sh270,000 kwa wiki na hayo ni mahesabu ya chini bila kujumuisha kazi ndogo ndogo za hapa na pale.

Mpiga violini huyo anasema zamani ilikuwa hauwezi kutazama barabarani na usione mgeni kabisa lakini kwenye kipindi cha Uviko-19, “wageni walikuwa hawaonekani kabisa.”

“Tulikuwa tunaandaa shoo lakini watu hawaji. Kwa sasa hivi kidogo tunashukuru Mungu, kazi zinakuja,” anasema.

Wanapotakiwa kurekebisha

Huenda hali ya ukata iliyowapata wasanii wa Taarab visiwani hapa ni kwa sababu hawakujiandaa au walikuwa hawana mbinu mbadala za kukidhi mahitaji yao ya maisha.

Mchambuzi wa muziki wa mwambao ambaye pia ni mwandaaji wa matamasha ya Taarab, Malick Mansoor anasema wasanii wa Taarab hawajawekeza vya kutosha katika muziki wao jambo linalowafanya washindwe kuhimili ushindani wa soko la muziki.

“Hakuna kizazi kipya cha Taarab ambacho kina watu branded na kizazi kinachoendeleza muziki wa Taarab kinajiendesha kwa njia zilezile ambazo walikuwa wanatumia miaka ya 90. Dunia inabadilika,” anasema Mansoor. 

Mdau huyo wa muziki wa mwambao anasema ikilinganishwa na muziki wa Bongo Fleva ambao uliendelea hata kipindi cha Uviko-19, muziki wa Taarab ulisimama kabisa bara na visiwani.

“Kuna nyimbo za Taarab ambazo nikikuuliza sasa hivi, hauwezi kuzipata kwenye majukwaa ya kidijitali siyo video wala sauti,” anasema Mansoor.

Kuepukana na hali hiyo, Mansoor anashauri wanamuziki wa Taarab wajitafakari na kuweka muziki huo katika majukwaa ya mtandaoni kwa ajili ya kupanua wigo wa wasikilizaji na pia kutengeneza pesa mtandaoni.

Ugonjwa wa Corona umeathiri wanamuziki wengi visiwani humo akiwemo Hassan Abrahman. Picha| Rodgers George.

Serikali pia inajitihada 

Licha ya kuwa watalii wanaanza kuonekana katika mitaa mbalimbali ya Zanzibar, Serikali pia ipo mbele katika kuhakikisha wananchi ambao wanategemea muziki hawaachwi nyuma.

Afisa Utalii wa Mkoa wa Mjini, Saidi Soud Said, ameiambia Nukta habari (www.nukta.co.tz) kuwa Serikali imetoa fursa za wasanii kufanya muziki katika ziara mbalimbali za kiserikali za kutangaza utalii ikiwemo “Royal Tour” ya Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.

“Kwa wanamuziki wa taarab wanapata nafasi kufanya maonyesho kwenye hafla mbalimbali kwa ajili ya kutangaza kama sehemu ya asili ya Zanzibar,” anasema Said.

Said anasema wataendelea kushirikiana na wasanii wa Taarab ili kuuendeleza muziki huo hata katika majanga makubwa kama Uviko-19.

Makala hii imefadhiliwa na Shirika la maendeleo ya habari la International Media Support (IMS) na Umoja wa Ulaya (EU).

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Nukta TV

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

Nukta TV

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Nukta TV