Dk Saqware arudishwa tena TIRA baada ya kuondolewa mwaka 2019

January 4, 2022 2:57 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni yule aliyefutwa kazi na Hayati Rais John Magufuli mwaka 2019.

Dar es Salaam. Miongoni mwa watu waliouanza mwaka kwa bahati ni Dk Baghayo Saqware ambaye ameteuliwa na Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) nafasi aliyowahi kuwa nayo miaka miwili iliyopita.

Dk Saqware ambaye uteuzi wake umetangazwa leo Januari 4, 2022, anashika nafasi hiyo kwa mara nyingine ndani ya kipindi cha miaka mitatu baada ya kufutwa kazi na Hayati Rais John Magufuli Juni 2019. Kabla ya uteuzi wa leo, Dk Saqware alikuwa ni Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo cha Uhasibu Tanzania (TIA). 

Katika uteuzi huo, Dk Saqware anachukua nafasi ya Dk Mussa Juma ambaye aliipokea mikoba yake miaka miwili iliyopita. Dk Juma kabla ya nafasi yake alikuwa Mkuu wa Idara ya Bima katika Kitivo cha Bima na Hifadhi ya Jamii cha Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM).

Mara ya kwanza Dk Saqware aliteuliwa na Dk Magufuli mwaka 2017 kama Kamishna wa Bima au Mkurugenzi Mkuu na kuhudumu kwa miaka miwili. 

Mbali na Dk Saqware, Rais Samia, kwa mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, amewateua viongozi wengine ambao ni Charles Itembe kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Eneo Maalum la Mauzo ya Nje(EPZA) pamoja na Ernest Mchanga kuwa Katibu wa Tume ya Pamoja ya Fedha(JFC).

Uteuzi huo umeanza Januari 1, 2022. 

Dk Baghayo katika moja ya mikutano na wanahabari. Picha| https://hakipensheni.blogspot.com.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW