Chaneli za bure zarudishwa DStv

January 31, 2022 10:46 am · Maria
Share
Tweet
Copy Link
  • Kuoneshwa kwa chaneli zisizo za kulipia katika kisimbuzi cha DStv ni matokeo ya mabadiliko ya kanuni za mawasiliano.
  • Hali hiyo itaongeza wigo wa upatikanaji habari kwa wananchi na soko la sanaa duniani.
  • Idadi ya visimbuzi vinavyoonesha chaneli za bure yafikia tano.

Dar es Salaam. Wigo wa wananchi kupata habari mbalimbali nchini huenda ukaongezeka baada ya kampuni ya Multichoice Tanzania (DStv) kuanza kuonesha chaneli zisizo za kulipia kutokana na mabadiliko yalifanywa na Serikali katika kanuni za miundombinu ya utangazaji kidijitali.

Agosti 2018, visimbuzi vya kampuni za Multichoice Tanzania (DStv), Simbanet Tanzania (Zuku) na Azam  vilizuiwa kuonyesha chaneli zisizo za kulipia za ndani ya nchi kutokana na masharti ya leseni zao kukidhi mfumo wa soko la kimataifa na maudhui yake huwa ni ya kulipia. 

Baadaye Mei, 2019 kisimbuzi kinachomilikiwa na kampuni ya Azam kilipatiwa leseni ya kuonyesha chaneli zisizo za kulipiwa na wakati huo huo DStv na ZUKU walipeleka maombi TCRA ili waweze kuonesha chaneli zisizo za kulipia bila mafanikio.

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema kutokana na mabadiliko waliyoyafanya kwenye kanuni za mawasiliano ya kielektroniki na posta kufuatia maagizo ya Rais wa Tanzania, chaneli zisizo za kulipia zitaanza kuonyeshwa katika kisimbuzi cha DStv.

Mabadiliko ya kanuni hayo yameanza kutumika kuanzia jana Januari 30, 2022.

“Tumefanya mabadiliko kwenye kanuni zetu ikiwemo namba 18 ya mwaka 2018 ambayo inahusiana na miundombinu ya utangazaji wa kidijitali, kanuni hii tumeifanyia mabadiliko ili kuruhusu chaneli ambazo hazilipiwi ziweze kuonekana kwenye king’amuzi cha DStv,” amesema Nnauye alipotembelea ofisi za DStv leo jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya ziara yake kwa wadau wa wizara hiyo.

Kwa mabadiliko hayo ya kanuni, inaongeza idadi ya kampuni zinazotoa huduma ya kuonyesha chaneli zisizo za kulipia na kufikia tano ukiachilia mbali Azam, kampuni ya Basic Transmission Ltd inayomiliki visimbuzi vya Continental na Digitek; Star Media (Startimes); na Agape Associates (Ting). 

Chaneli za ndani  zisizo za kulipia hujumuisha TBC 1, ITV, Star TV, Channel TEN, East Africa TV, Safari Channel na Clouds TV. 


Zinazohusiana:


Hata hivyo, Nnauye amesema baadhi ya faida zinatakazoletwa na uamuzi huo wa kubadilisha na kufanyia maboresho baadhi ya kanuni ni pamoja na kuongezeka kwa wigo wa kupata habari kwa Watanzania.

“Tunaamini kwamba uamuzi huu utazipeleka hizi chaneli duniani, nilikua nauliza hapa wigo wa Multichoice unakwenda nchi 36 Afrika maana yake ni kwamba pamoja na Watanzania waliopo huko wataona chaneli za nyumbani kupitia hiki king’amuzi lakini pia tutakua tumezifungulia hizi chaneli milango ya kwenda duniani,” amesema Nnauye.

Aidha, amesema kupitia mabadiliko hayo, soko la kazi za sanaa litaongezeka kwa kuwa chaneli hizo zitatumika kutangaza kazi za sanaa za hapa nchini na kukuza utamaduni wa Tanzania ikiwemo lugha ya Kiswahili kimataifa.

Wito kwa chaneli zilizoruhusiwa kuonyeshwa DStv

Waziri Nape amezika chaneli zilizoruhusiwa kuonyeshwa katika king’amuzi cha DStv ambazo ni chaneli zisizo za kulipia kuongeza ubora wa maudhui wanayotengeneza na kuyarusha.

“Kwa chaneli tulizoziruhusu kwenda kwenye ving’amuzi vingine ni kuongeza ubora wa maudhui (content) mnayotengeneza, wasanii wetu mfanye kazi nzuri ili zikionekana zivutie,” amesema Nnauye.

Amesisitiza uamuzi huo utaongeza wigo wa biashara kwa vyombo vya habari, ambapo biashara hizo zitawaongezea mapato yatakayotumika kuboresha sekta hiyo ya habari na mawasiliano.

“Ni matumaini yangu uamuzi huu utapokelewa vizuri, utatimizwa na kuona namna ambavyo tutasonga mbele pamoja,” amesema Nnauye

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW