Akamatwa na shehena ya dawa za mifugo Mwanza
- Mmiliki wa dawa hizo, Nixon Thobias akamatwa.
Mwanza. Mamlaka ya Dawa na vifaa Tiba (TMDA) kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi mkoani Mwanza imefanikiwa kukamata shehena ya dawa za mifugo zenye thamani ya zaidi ya Sh99 milioni zilizoingizwa nchini na kuhifadhiwa kwenye ghara bubu kinyume cha sheria.
Akizungumza na wanahabari leo Februari 10, 2022, Meneja wa TMDA Kanda ya Ziwa, Sophia Mziray amesema dawa hizo ambazo hazikuthibithishwa na mamlaka hiyo na wamemkamata mmiliki wa dawa hizo, Nixon Thobias.
Mziray amesema taratibu za kisheria zinakamilishwa ili mtuhumiwa aweze kufikishwa mahakamani.
“Baada ya kufanya uchunguzi tumebaini kuwa bidhaa zilizokuwemo hazijasajiliwa na mamlaka ya dawa lakini pia TMDA haijathibitisha ubora, usalama na ufanisi wa dawa hizo na hata namna mfanyabiashara huyo alivyoziingiza nchini hazikufuata taratibu,” amesema Mziray.
Mbali na kosa hilo, pia TMDA ilibaini kuwa mfanyabiashara huyo ameingiza dawa zingine ambazo mamlaka hapa nchini imezisajili lakini yeye hajapewa kibali cha kuziingiza kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.
“Kwa mantiki hiyo amevunja sheria ya uingizaji wa bidhaa za dawa hivyo atashitakiwa kwa makosa hayo,” amesema Mziray.
Soma zaidi:
-
Miili ya wanawake watatu waliouawa yazikwa Mwanza
-
Watano mbaroni mauaji ya ndugu wa familia moja Mwanza
Licha ya kukiri kuwepo kwa mianya ya njia za panya kwenye mipaka yote ya Kanda ya Ziwa, Meneja huyo pia amesema njia wanazotumia kuwakamata wafanyabiashara wasiofuata kanuni na sheria ni kukagua kwenye maeneo yao ya biashara pamoja na kupokea taarifa mbalimbali kutoka kwa raia wema.
“Mfano mfanyabaishara huyu alitengeneza ghala lake nyumbani, eneo ambalo ni sehemu ya geleji kwahiyo ni vigumu watu kubaini kama hapa kuna ghala kubwa la dawa za mifugo, lakini pia ni hatari kwa afya za watu wanaokaa karibu na ghala hili,” amesema meneja huyo.
Kwa upande wake Mkaguzi wa TMDA Kanda ya Ziwa, Agrey Mwabuki amewataka wafanyabaishara kuwa waadilifu na kufuata kanuni na taratibu za uingizwaji wa dawa hizo nchin.
Pia amewataka kuhakikisha maghala yote yawe yamesajiliwa ili kulinda afya za watumiaji.
“Mfano kuna dawa zingine ambazo muda wake unawahi kuisha na kusababisha madhara kwa binadamu,” amesema Mwabuki.
Latest