Magazeti manne kufunguliwa: Ushindi kwa vyombo vya habari Tanzania
- Watetezi wa haki za binadamu waipongeza Serikali.
- Waishauri kuimarisha zaidi uhuru wa kujieleza, vyombo vya habari.
Dar es Salaam. Shirika la haki za binadamu la Amnesty International limeipongeza Serikali ya Tanzania kuyafungulia magazeti manne likiwemo la Mseto huku likiitaka kufanya zaidi ili kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari nchini.
Magazeti manne ya Tanzania Daima, Mawio, Mwanahalisi na Mseto yalifungiwa kuchapishwa kwa makosa mbalimbali chini ya Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari iliyoanza kutumika Novemba 2016 na Sheria ya Magazeti ambayo sasa imefutwa.
Kuondolewa kwa marufuku kwa magazeti hayo ambayo yalikuwa yamezuiliwa kuchapishwa tangu 2016 na 2017 kumetajwa na shirika hilo kama hatua kubwa katika kuendeleza uhuru wa kujieleza na vyombo vya habari.
Naibu Mkurugenzi wa Amnesty International kwa Afrika Mashariki, Pembe na Maziwa Makuu, Sarah Jackson amesema katika kipindi cha miaka sita iliyopita, magazeti yaliyokuwa yakifuchua ufisadi na ukiukaji wa haki za binadamu yalilengwa na kupata misukosuko mbalimbali.
“Sasa zuio la magazeti haya limeondolewa, mamlaka za Tanzania zifute Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ili kuhakikisha vyombo huru vya habari vinafanya kazi zao kwa uhuru, na kufanya kazi zao bila kuogopa.
“Hii ni muhimu kwa kufurahia haki za uhuru wa kujieleza na kupata habari,” amesema Jackson.
Agosti 10, 2016, Serikali ililifungua gazeti la Mseto kwa miezi 36 kutokana na kuandika habari yenye nyaraka zilizodaiwa ni za kughushi.
Mwaka uliofuata, Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo wa wakati huo, Harrison Mwakyembe, alifungia magazeti manne Mawio, Mwanahalisi, Raia Mwema na Tanzania Daima kwa kuchapisha habari zinazohusu tuhuma za rushwa.
Zinazohusiana:
- LHRC yazungumzia adhabu ya vituo vitatu vya televisheni mtandaoni.
- Waziri Nape ayafungulia magazeti manne yaliyofungiwa
- CCM yazidi kuongeza umiliki wa vyombo vya habari Tanzania
Juni 23, 2020, Serikali ilizuia uchapishaji na usambazaji wa gazeti la Tanzania Daima ndani na nje ya nchi kwa muda usiojulikana kwa uvunjaji wa sheria na kushindwa kuzingatia maadili ya taaluma, lakini halikutaja sheria au maudhui mahususi.
Awali gazeti hilo lilifungiwa kwa siku 90 mwaka 2017 kwa madai ya kuchapisha habari za uongo.
Agosti 11, 2021, Serikali ilisimamisha gazeti lingine la Uhuru, kwa siku 14 kwa kuchapisha habari iliyodai kuwa Rais Samia Suluhu Hassan hana nia ya kuwania wadhifa huo katika uchaguzi wa 2025.
Mnamo Septemba 5, 2021, Idara ya Huduma ya Habari ililifungia gazeti la Raia Mwema kwa siku 30 kwa madai ya kukiuka viwango vya taaluma ya uandishi wa habari mara kwa mara na kuvunja sheria kwa kuchapisha ripoti za “kupotosha” ambazo zinachoche “uchochezi wa vurugu.”
Waziri wa Habari, Teknolojia ya Mawasiliano, Nape Nnauye, alitangaza kuondoa marufuku ya magazeti hayo manne Februari 10, 2022 katika mkutano na wahariri wa vyombo vya habaei jijini Dar es Salaam.
Nape alikuwa anatekeleza agizo la Rais Samia alilolitoa Aprili 6, 2021 ambapo aliagiza vyombo vya habari vilivyofungiwa vifunguliwe viendelee kufanya kazi huku vikizingatia sheria za nchi.
Latest
