Mabadiliko ya tabianchi: Kichocheo kipya moto wa msituni

February 25, 2022 4:26 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • UNEP yasema moto wa msituni utaongezeka kwa asilimia 50 mwishoni mwa karne ya 21.
  • Ukame, ongezeko la joto, upepo mkali kuchangia ongezeko hilo.
  • Serikali zatakiwa kujiandaa kiteknolojia, fedha na wafanyakazi.

Dar es Salaam. Huenda visa wa vifo vya watu, uharibifu wa mali na mazingira vikaongezeka siku zijazo baada ya ripoti mpya kueleza kuwa kutakuwa na ongezeko kubwa la moto wa msituni (nyika) mwishoni mwa karne ya 21 unaochochewa na mabadiliko ya tabianchi. 

Ripoti ya utafiti uliopewa jina la “Kuenea kama Moto wa Nyika: Kuongezeka kwa tishio la mioto ya ajabu ya mazingira,” ya mwaka 2022 inaeleza kuwa moto wa nyika unakadiriwa kuongezeka kwa asilimia 50 ifikapo mwisho wa karne hii kutokana na mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi na mabadiliko ya matumizi ya ardhi, 

Utafiti huo uliotolewa jana Februari 24 na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Mazingira (UNEP) na GRID-Arendal, shirika lisilo la kiserikali ambalo ni kituo cha mawasiliano ya mazingira kilichopo Norway umegundua kuwa hata maeneo ya Arctic na maeneo mengine ambayo hapo awali hayakuathiriwa na moto wa nyika, sasa yanakabiliwa na hatari kubwa. 

Miongoni mwa maeneo yaliyoathirika na moto wa nyika ni misitu ya Amazon nchini Marekani, Australia na maeneo ya Savanna ya Afrika.

Wazima moto huko California na maeneo mengine ya Pwani ya Magharibi ya Marekani wamejitahidi kuzuia moto wa nyika. Picha| Idara ya Moto ya San Francisco. 

Uhusiano wa moto huo na mabadiliko ya tabianchi

Ripoti imeeleza kuwa moto wa nyika unachochewa na mabadiliko ya tabianchi kupitia kuongezeka kwa ukame, joto la hali ya juu, unyevu, umeme, na upepo mkali na kusababisha misimu ya joto zaidi, hali kame na ya muda mrefu ya moto wa nyika.

“Wakati huo huo, mabadiliko ya tabianchi yanafanywa kuwa mabaya zaidi na moto wa nyika, hasa kwa kuharibu mazingira nyeti na yenye kiwango kikubwa cha hewa ukaa kama vile peatlands na misitu ya mvua. 

“Hii inageuza mandhari kuwa visanduku vidogo, na kuifanya kuwa vigumu kukomesha halijoto inayoongezeka.” imesema ripoti hiyo. 

Ripoti hiyo inasisitiza hitaji muhimu la kuelewa vyema tabia ya mioto ya nyika. Kuzuia kunahitaji mchanganyiko wa takwimu na mifumo ya ufuatiliaji inayozingatia sayansi na maarifa asilia, na kwa ushirikiano thabiti wa kikanda na kimataifa. 


Soma zaidi:


Athari za moto wa nyika

Moto wa nyika unaathiri kwa kiasi kikubwa mataifa maskini zaidi duniani, na athari ambazo hudumu kwa muda mrefu baada ya moto huo kupungua na hivyo kuzuia maendeleo endelevu na kuzidisha pengo la usawa wa kijamii. 

Moshi kutoka moto huo huathiri moja kwa moja afya za watu ikiwemo kupumua, moyo na mishipa, kuongeza gharama za maisha kwa watu kujenga upya makazi yaliyoungua. 

Wanyamapori, pamoja na makazi ya asili, pia hunusurika mara chache, imeeleza ripoti hiyo na kubainisha kuwa “moto wa nyika umesababisha baadhi ya wanyama na mimea kutoweka.”

Mioto ya nyika ya mwaka 2020 nchini Australia inakadiriwa kuwa iliangamiza mabilioni ya wanyama wa kufugwa na wa porini. 

Waandishi wa ripoti hiyo wanatoa wito wa mabadiliko makubwa katika hatua za serikali ambazo zinazingatia kuzuia na kujitayarisha kukabili hatari hiyo. 

Moto wa nyika ulionea katika eneo la Queensland na New South Wales nchini Australia. Picha| Ofisi ya Huduma za Dharura za Queensland

Suluhu ya tishio hilo la moto

Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP, Inger Andersen amesema kwa sasa uwekezaji zaidi wa pesa na nguvukazi unahitajika ili kujitayarisha kudhibiti moto huo. 

“Wale wafanyakazi wa huduma ya dharura na wazima moto walio mstari wa mbele ambao wanahatarisha maisha yao ili kupambana na moto wa nyika wanahitaji kuungwa mkono. 

“Tunapaswa kupunguza hatari ya moto wa nyika uliokithiri kwa kujitayarisha vyema, kuwekeza zaidi katika kupunguza hatari ya moto, kufanya kazi na jumuiya za wenyeji, na kuimarisha dhamira ya kimataifa ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi,” amesema Andersen mara ya ripoti hiyo kutoka jana.  

Ripoti hiyo imetolewa kabla ya kuanza kwa kikao cha Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa kitakachofanyika Nairobi, Kenya, wiki ijayo likihudhuriwa na wawakilishi kutoka nchi 193. 

Serikali ikiwemo ya Tanzania zinahimizwa kupitisha kinachojulikana kama “Mfumo uliotayari kwa ajili ya moto”, ambayo inataka theluthi mbili ya bajeti za kukabiliana a majanga ya moto itumike katika kupanga, kuzuia, kujitayarisha na kurejesha na theluthi moja kwa ajili ya kukabiliana na moto wa nyika. 

Waandishi hao wa ripoti hiyo wanatoa wito wa kuwepo kwa viwango imara vya kimataifa kwa ajili ya usalama na afya ya wafanyakazi wa zima moto na kupunguza vitisho vinavyowakabili kazini. 

Hii ni pamoja na kuongeza ufahamu wa hatari za kuvuta pumzi ya moshi, kupunguza uwezekano wa mitego ya kutishia maisha, na kuwapa ufikiaji wa hewa ya kutosha, lishe, na kupumzika kati ya zamu zao za kazi. 

Pia matumizi ya teknolojia za kisasa za kugundua viashiria vya moto zitumike kukabiliana na vitisho vya kila aina. 

Makala hii imefadhiliwa na Shirika la WAN-IFRA-Press Freedom. WAN-IFRA haihusiki kwa namna yeyote na maudhui haya. 

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Nukta TV

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

Nukta TV

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Nukta TV