Tanzania, Congo DRC kujadili mwelekeo mpya wa kibiashara
- Nchi hizo zitafanya mkutano hivi karibuni kuhusu mahusiano ya kibiashara.
- Mkutano huo utajadili changamoto na suluhu za kibiashara kwa mataifa hayo.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (Congo DRC) zimepanga kuandaa mkutano mkubwa wa pamoja kati ya wafanyabiashara wa nchi hizo ili kuzungumzia mwelekeo wa kibiashara ili kuimarisha uchumi wa nchi hizo mbili.
Amesema kuwa mkutano huo ambao utajadili changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo wafanyabiashara na namna ya kuzitatua utasaidia kuchochea uchumi wa kitaifa na wa mtu mmoja mmoja.
“Tuna fursa katika ziwa Tanganyika ambapo Tanzania tumejenga bandari tano muhimu zinazoweza kutumiwa na DRC, pia tuna barabara tunayoitumia kutoka Tunduma kwenda Kaprimposhi-Kasumbalesa, tunataka kubadilisha “route” ipite kwenye daraja la Kasenga barabara ambayo ni fupi sana inapunguza zaidi ya kilomita 2000 kwenda na kurudi,” amesema.
Amesema hayo Februari 25, 2022 baada ya mazungumzo yake na Waziri Mkuu wa Congo DRC, Sama Lukonde yaliyofanyika ofisini kwa Waziri Mkuu huyo jijini Kinshasa.
Majaliwa amesema wamekubaliana kutembeleana ili kuimarisha utendaji na ufutiliaji pamoja na kuimarisha uhusiano.
Awali, Waziri Mkuu alikutana na watumishi katika ubalozi wa Tanzania nchini DRC na aliwataka kuongeza ubunifu ili kukuza diplomasia ya uchumi kati ya nchi hiyo na Tanzania.
“Tunapozungumzia ubalozi maana yake tunawataka muimarishe diplomasia yetu , ongezeni ubunifu ili tuweze kunufaika na mahusiano haya,” amesema Majaliwa.
Waziri Mkuu amerejea nchini baada ya kumalizika kwa mkutano wa 10 wa wakuu wa nchi na serikali kuhusu Mpango wa Amani, Usalama na Ushirikiano na DRC pamoja na Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu uliofanyika jijini Kinshasa, ambapo alimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan.
Latest
