Mitandao ya kijamii inavyochochea matumizi ya dawa za kulevya kwa vijana
- Wauzaji watumia njia za kidijitali ikiwemo mitandao ya kijamii kukuza biashara zao
- Sarafu za kidijitali, malipo ya simu na huduma za kielektroniki zatajwa katika biashara ya dawa za kulevya.
- Serikali zatakiwa kuongeza uthibiti wa janga hilo.
Dar es Salaam. Bodi ya kimataifa ya kudhibiti madawa ya kulevya (INCB), imezitaka Serikali kufanya jitihada zaidi kudhibiti mitandao ya kijamii ambayo inasifu tabia mbaya zinazohusiana na dawa zaa kulevya na ili kuwanusuru vijana wasiathirike na dawa hizo.
Katika ripoti yake ya kila mwaka, iliyotolewa Machi 10 2022, INCB imebainisha kuongezeka kwa ushahidi wa uhusiano kati ya umaarufu katika mitandao ya kijamii na matumizi ya dawa za kulevya.
Hali hiyo ambayo huathiri vibaya vijana, ambao ni watumiaji wakuu wa majukwaa ya mitandao ya kijamii, na kundi rika lenye viwango vya juu vya watumiaji wa dawa za kulevya.
Ripoti hiyo imeeleza kuwa pamoja na majukwaa ya mitandao ya kijamii, wahalifu wanatumia zana nyingine za kidijitali ikiwemo sarafu za kidijitali, malipo ya simu na huduma za kielektroniki, ambazo hurahisisha uhamishaji wa fedha kimataifa na kwa haraka zaidi, na kuwaruhusu kuficha chimbuko la fedha haramu na hivyo kujiongezea faida.
“Hali hiyo ina matokeo mabaya kwa jamii na maendeleo ya kiuchumi, kuanzia ufisadi na hongo, hadi kuongezeka kwa uhalifu wa kupangwa, vurugu, umaskini na ukosefu wa usawa.” inaeleza ripoti ya INCB.

Umaarufu katika mitandao ya kijamii na matumizi ya dawa za kulevya,huathiri vibaya vijana, ambao ni watumiaji wakuu wa majukwaa ya mitandao ya kijamii. Picha| North Jersey Recovery Center.
Ili kukabiliana na athari mbaya na gharama za biashara hiyo kwa binadamu, bodi hiyo iliyo chini ya Umoja wa Mataifa (UN) linapendekeza kuwa serikali zishughulikie hatua zote za ulanguzi wa dawa za kulevya kuanzia uzalishaji hadi uuzaji.
“INCB iliona mtiririko wa fedha haramu kuwa unastahili kuangaliwa mahususi na kuchunguzwa kwa sababu biashara ya madawa ya kulevya ni tasnia yenye faida kubwa kwa magenge ya uhalifu wa kupangwa,” amesema Rais wa INCB, Jagjit Pavadia.
Zinazohusiana:
-
Zingatia haya kuwa na afya bora ya akili
-
Fahamu haya kuhusu matumizi ya intaneti, mitandao ya kijamii duniani
Matumizi ya dawa za kulevya ambayo yana athari mbalimbali ikiwemo afya ya akili, yaliongezeka mwaka 2020 , ambapo takriban watu milioni 275 duniani walitumia dawa hizo kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa Juni 2021 na ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na madawa na uhalifu (UNODC ).
Hali ni mbaya katika nchi zinazoendelea
Katika nchi za Afrika, ripoti inasema gharama ya uhalifu wa kupangwa ni inakadiriwa kuwa Dola za Marekani bilioni 88.6, sawa na Sh205 trilioni, ikiwa ni takriban asilimia 3.7 ya pato la taifa la bara la Afrika ambazo hupotea kwa sababu ya mtiririko haramu wa kifedha kila mwaka.
INCB inahimiza kuboreshwa kwa udhibiti na kanuni zinazosimamia uuzaji wa vianzilishi, ikitolea mfano utafiti uliofanywa na shirika hilo mwaka 2021, ambao ulionyesha mapungufu makubwa katika udhibiti wa utengenezaji, biashara na usambazaji wa kemikali hizo