Kilimo, biashara: Kutawala bajeti ya Serikali 2022-23

April 4, 2022 7:04 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Serikali yasema itawekeza fedha nyingi katika sekta hizo.
  • Hiyo itasaidia kuongeza uzalishaji na fursa za ajira.
  • Wahisani waahidi kutunisha bajeti ya Serikali.

Dar es Salaam. Wakati vikao vya Bunge vikitarajia kuanza kesho, Serikali imesema bajeti ya mwaka 2022/23 na zijazo zitajikita zaidi katika kilimo na uboreshaji wa mazingira ya biashara ili kuongeza uzalishaji na fursa za ajira.

Vikao hivyo vitakavyoanza Aprili 5, 2022 ni mahususi kujadili bajeti za wizara na Serikali Kuu kwa mwaka 2022/23 ambao unaanza rasmi Julai moja mwaka huu.

Katika mwaka wa fedha wa 2022/23, Serikali inakadiria kutumia bajeti ya Sh41.1 trilioni. Kati ya kiasi hicho kitakachotumika mwaka ujao, Sh25.5 trilioni zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida ikiwa ni asilimia 62.2 ya bajeti yote, ikijumuisha Sh11.3 trilioni kwa ajili ya ulipaji wa deni la Serikali.

Wakati Wabunge wakijiandaa kwa majadiliano ya kina na kupitisha bajeti hiyo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amesema Serikali imejipanga kikamilifu kuhakikisha kuwa sekta muhimu za uzalishaji ikiwemo kilimo zinaongezewa fedha ili kuongeza tija katika sekta hizo.

“Katika Bajeti ya mwaka 2022/23, na zijazo, tutawekeza fedha nyingi kwenye maeneo ya uzalishaji ikiwemo kilimo kwa kuongeza huduma za umwagiliaji na uzalishaji wa mbegu bora, uhifadhi wa mazao, mifugo bora, uvuvi na kuboresha mazingira ya biashara kwa wamachinga,” amesema Dk Nchemba.

Dk Nchemba ametoa msimamo huo alipokutana na kufanya mazungumzo na Ujumbe wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) ukiongozwa na Mwakilishi wake Mkazi Christine Musisi, Jijini Dodoma mwishoni mwa wiki.

Amesema kuwa sekta hizo ni kipaumbele cha Serikali na inakwenda sambamba na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya mwaka 2025 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano.


Zinazohusiana: 


Kilimo kimeendelea kuwa na umuhimu mkubwa katika kuchangia pato la Taifa (GDP) na uchumi wa nchi hususan katika kuhakikisha usalama wa chakula, upatikanaji wa ajira na malighafi za viwanda. 

Kwa mujibu wa Wizara ya Kilimo, katika mwaka 2019, mchango wa kilimo katika pato la Taifa ulikuwa ni asilimia 26.9 na sekta hiyo imechangia kwa asilimia 58.1 katika kutoa ajira na zaidi ya asilimia 65 ya malighafi za viwanda nchini.

Nchemba, ameipongeza UNDP kwa kuchangia maendeleo ya nchi katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii na kuliomba shirika hilo kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za kuwaletea wananchi maendeleo.

Mwakilishi Mkazi wa UNDP, Christine Musisi, ameihakikishia Tanzania kuwa shirika lake litaendelea kuchangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii kupitia miradi mbalimbali iliyowekeza fedha nchini ikiwemo kilimo, uchumi wa bluu na kuboresha sekta nyingine za uzalishaji.

Ameahidi kuwa shirika lake litaendelea kutoa fedha katika maeneo ya uzalishaji na uwekezaji yatakayochangia kuondoa umaskini na kutatua changamoto zote za uzalishaji mali kupitia sekta binafsi na wajasiriamali.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW