Tanzania inavyodhibiti migogoro ya binadamu na wanyamapori
- Inafanya doria za mara kwa mara katika maeneo yenye migogoro.
Dar es Salaam. Wizara ya Maliasili na Utalii imesema itaendelea kudhibiti migongano baina ya binadamu na wanyamapori katika maeneo ya kinga ya hifadhi na mtawanyiko wa wanyamapori mkoani Simiyu ili kupunguza athari ikiwemo uhalibifu wa mali na vifo vya watu.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja amesema wizara yake hufanya doria za mara kwa mara kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu na pia vituo viwili vya askari vitajengwa katika maeneo ya Busega na Meatu mkoani humo.
Masanja ameyasema hayo Aprili 5, 2022 Bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Minza Mjika aliyetaka kufahamu mikakati ya Serikali kupunguza migogoro ya wanyamapori na binadamu.
Pia, wizara inatarajia kuajiri askari 600 na mafunzo ya mbinu za kujilinda na kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu yametolewa kwa Halmashauri za wilaya 17 nchini.
Aidha, Wizara imetoa namba maalum za simu kwenye kila kanda za kiutendaji ili kuwezesha wananchi kutoa taarifa za matukio ya wanyamapori bila malipo.