Tanzania yatoa ruzuku ya Sh100 bilioni kupunguza maumivu bei ya mafuta
- Ruzuku hiyo itatokana na Serikali kujibana katika matumizi ya kawaida
- Pia, imeomba mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia na IMF kupunguza bei za nishati hiyo.
Dar es Salaam. Baada ya kilio cha kupanda kwa gharama za mafuta ya petroli Tanzania, Serikali imetoa ruzuku ya Sh100 bilioni zitakazosaidia kupunguza maumivu ya kupanda gharama za maisha kutokana kupanda kwa bei ya mafuta.
Ruzuku hiyo kwa mujibu wa Waziri wa Nishati, January Makamba itasaidia kutoa ahueni katika upatikanaji wa nishati hiyo muhimu nchini kuanzia Juni mosi mwaka huu.
Makamba amewaambia wabunge jijini Dodoma leo (Mei 10, 2022) kuwa uamuzi wa kutoa ruzuku hiyo ulifikiwa na Rais Samia Suluhu Hassan ikiwa ni moja ya hatua za kusaidia kupunguza gharama za maisha kwa Watanzania ambao siku za hivi karibuni wameshuhudia bei za bidhaa na huduma mbalimbali zikipaa na kutoboa mifuko yao zaidi.
Serikali kujibana kupunguza bei ya mafuta
“Ruzuku hii inatolewa kwa kupunguza matumizi ya Serikali katika kipindi kilichobaki cha mwaka 2021/22. Kutolewa kwa ruzuku hii hakutagusa miradi ya maendeleo ambayo inaendelea,” amesema Makamba katika hotuba yake bungeni.
Waziri huyo alikuwa amepewa wiki moja na Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson kueleza hatua zinazofanywa na Serikali kukabiliana na kuongezeka kwa gharama za maisha kulikosababishwa na kupaa kwa bei za mafuta ya petroli katika soko la Dunia.
Makamba anasema ruzuku hiyo ya Sh100 bilioni itaanza kutoa nafuu Juni mosi kwa sababu tayari wafanyabiashara wa jumla wameshalipia gharama ya mafuta ambayo imejumuishwa katika bei za Mei 2022 na wafanyabiashara wa mafuta katika vituo wameshanunua mafuta hayo kwa bei inayoendelea kutumika sasa.
Hata hivyo, haijawa bayana ruzuku hiyo itaenda kupunguza bei ya mafuta kwa kiwango gani kutoka bei ya sasa inayolalamikiwa na wengi kiasi cha kupandisha nauli na bidhaa nyingine.
Serikali yaomba mkopo Benki ya Dunia, IMF
Mbali na hatua hiyo, Makamba amesema Serikali imeomba mkopo kutoka Benki ya Dunia (World Bank) na Shirika la Fedha Duniani (IMF) kwa ajili ya kuleta ahueni kwenye bei za mafuta na bidhaa nyinginezo zinazogusa maisha ya watu.
“Mchakato wa kuchukua mkopo huo uko mbioni kukamilika na ahueni kwenye kupanda kwa bei za bidhaa itapatikana katika mwaka ujao wa fedha,” amesema.
Tangazo:

Mbali na mafuta ya petroli bidhaa na huduma nyingine zimeendelea kupaa pia Tanzania zikiwemo unga wa ngano, mafuta ya kupikia, nauli za usafiri wa abiria na mizigo na huduma mbalimbali zinazotegemea zaidi mafuta.
Jioni ya Mei 9, 2022 Rais Samia alilihutubia Taifa na kueleza kuwa kupanda kwa mafuta ni tatizo la dunia nzima kutokana na vita inayoendelea Ulaya Mashariki baada ya Urusi kuivamia kijeshi Ukraine.
Rais Samia: Serikali tujibane, tujiminye
Katika jitihada za muda mfupi baada ya kusikia kilio cha wananchi, Rais Samia alisema ameelekeza Serikali “tujibane na tujinyime ili kupata fedha katika matumizi ya kawaida ya Serikali ili kutoa nafuu ya bei za mafuta.”
“Kwa miezi 18 iliyopita bei imekuwa ikipanda kwa kasi,” amesema Rais Samia.
Bei za mafuta ya petrol, dizeli na mafuta ya taa yamekuwa yakipanda kwa kasi ndani ya mwaka mmoja kiasi cha kuongeza maumivu zaidi kwa watumiaji wa vyombo vya moto.
Mafuta ya petroli yamepanda kutoka Sh1,981 kwa lita Machi 2021 jijini Dar es Salaam hadi kufikia Sh3,148 kwa lita Mei mwaka huu ikiwa ni ongezeko la Sh1,167 kwa lita ndani ya miezi 14.
Oktoba 2021 Serikali ilipunguza tozo zinazotozwa na taasisi mbalimbali kwenye mafuta ili kushusha bei ya mafuta kiasi cha kuifanya ipoteze mapato ya Sh102 bilioni.