Wananchi walalamikia pendekezo kupandishwa kwa ushuru wa mawigi
- Waomba Serikali ifikirie upya suala hilo kunusuru biashara zao.
- Ushuru wa mawigi yanayoagizwa nje ya nchi unakusudia kupanda kutoka asilimia 25 hadi asilimia 35 mwaka fedha ujao.
- Lengo ni kuongeza mapato ya Serikali na kulinda wazalishaji wa ndani.
Dar es Salaam. Kufuatia tamko la Serikali ya Tanzania kupendekeza kuongeza ushuru kwenye nywele bandia (mawigi) yanayoagizwa nje ya nchi hadi asilimia 35 katika mwaka ujao wa fedha, watumiaji na wauzaji wa bidhaa hiyo wameiomba Serikali kutoongeza ushuru huo ili kunusuru biashara zao.
Waziri wa Wizara ya Fedha na Mipango Dk Mwigulu Nchemba aliyekuwa akiwasilisha Bungeni mapendekezo ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2022/2023, Juni 14 Bungeni jijini Dodoma alisema ushuru katika bidhaa hiyo unakusudia kuongezeka kutoka asilimia 25 ya sasa.
Pendekezo hilo la kuongezeka kwa ushuru huo, Nchemba alisema ni makubaliano ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambayo inaundwa na nchi saba ikiwemo Tanzania.
“Nchi wanachama za Jumuiya ya Afrika Mashariki zimekubaliana kuongeza ushuru wa forodha kutoka asilimia 25 mpaka asilimia 35, kutoka kwenye nywele bandia,” alieleza Waziri Nchemba na kubainisha kuwa hatua hiyo itaongeza mapato ya Serikali.
Waziri huyo alisema lengo ni kulinda na kuviongezea uwezo viwanda vya ndani kuzalisha na kujipatia soko la uhakika la bidhaa hiyo kutoka kwa watumiaji.
Hata hivyo, ushuru kwa bidhaa hiyo inayozalishwa na viwanda vya ndani haujabadilika imebaki asilimia 10 ya awali ambayo ilianza kutumika mwaka 2019/20.
Soma zaidi:
- Nukta | Madhara ya matumizi ya dawa za nywele, mawigi kwa wanawake
- Nukta | Maumivu kwa wanawake, Serikali ikipendekeza kutoza ushuru mawigi
“Pendekezo litaua biashara”
Baadhi ya watumiaji wa mawigi wameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa ikiwa Serikali itapitisha pendekezo hilo la kupandisha ushuru litawaongea gharama za maisha.
“Bidhaa zote zimepanda bei, sasa wanataka wapadishe na ushuru wa kodi, hii itatuumiza zaidi, waliangalie tena kabla ya kufanya maamuzi,” amesema Getrude John, mkazi wa Bunju, jijini Dar es Salaam.
John amesema kila mtu ana uchaguzi wa kutumia wigi analopenda, wengine wanapenda yanayotoka nje ya nchi, hivyo kupandisha ushuru inaweza kuwanyima haki ya kuchagua.
Wauzaji wa bidhaa hiyo nao wameliomba Bunge kutopitisha pendekezo hilo kwani litaua biashara zao za saluni na kuongeza ugumu wa maisha.
“Nawashauri wabunge wasipitishe tu hizo tozo kwasababu wakituongezea na huku biashara zinazidi kudoda,” amesema Mwajabu Hamisi, Msusi wa Mwanayamala jijini hapa.
Madhara ya nywele bandia kwa afya ya binadamu
Mwajuma Tuwano, mtumiaji wa mawigi na mkazi wa mwananyamala Dar es Salaam amesema hata sasa bei ya mawigi iko juu.
Kwa mujibu wa Tuwano, wigi orijino unaweza kupata kwa Sh400,000 au Sh500,000 yasiyo origino ni Sh10,000 au Sh20,000, hali ambayo ni tofauti sana na zamani.
“Kipindi cha nyuma ilikuwa haya yasiyo origino ulikuwa unapata kwa Sh5,000 au Sh3,000 na haya origino unayapata kwa Sh300,000, la chini kabisa unalipata kwa Sh350,000,” amesema Tuwano.
Nywele bandia maarufu kama mawigi ni bidhaa pendwa inayotumiwa na wanawake na wasichana kufunika vichwa na kuongeza urembo kwa muhusika.
Licha ya kuwa watumiaji watalazimika kutoboa zaidi mifuko yao, huenda itakuwa kicheko kwa wazalishaji wa ndani wa bidhaa hiyo kwa sababu watafaidika na wateja ambao wataachana na mawigi ya nje, hivyo kuwaongezea faida.