Maumivu ushuru wa mawigi kuanza leo
- Ni wa asilimia 35 kwenye nywele bandia zinazotoka nje ya nchi.
- Watumiaji wasema itaongeza gharama za maisha.
Dar es salaam. Tanzania inaanza kutekeleza makubaliano ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ya kutoza ushuru wa asilimia 35 katika nywele bandia (mawigi) yanayoagizwa nje ya nchi huku ukiacha maumivu kwa wafanyabiashara na watumiaji wa bidhaa hiyo.
Ushuru huo ambao umepanda kutoka asilimia 25 ya awali ulipitishwa katika Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2022/23
Waziri wa Wizara ya Fedha na Mipango Dk Mwigulu Nchemba wakati anawasilisha pendekezo hilo Bungeni Juni 16 mwaka huu alisema ushuru huo makubaliano ya EAC ambayo inaundwa na nchi saba ikiwemo Tanzania.
“Nchi wanachama za Jumuiya ya Afrika Mashariki zimekubaliana kuongeza ushuru wa forodha kutoka asilimia 25 mpaka asilimia 35, kutoka kwenye nywele bandia,” alieleza Waziri Nchemba na kubainisha kuwa hatua hiyo itaongeza mapato ya Serikali.
Waziri huyo alisema lengo ni kulinda na kuviongezea uwezo viwanda vya ndani kuzalisha na kujipatia soko la uhakika la bidhaa hiyo kutoka kwa watumiaji.
Hata hivyo, ushuru kwa bidhaa hiyo inayozalishwa na viwanda vya ndani haujabadilika imebaki asilimia 10 ya awali ambayo ilianza kutumika mwaka 2019/20.
Baadhi ya watumiaji wa mawigi waliambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa amesema kupandisha ushuru ni kuwaumiza zaidi Wananchi kwani bidhaa nyingine zimekwisha panda bei.
“Kila mtu ana uchaguzi wa kutumia wigi analopenda, wengine wanapenda yanayotoka nje ya nchi, hivyo kupandisha ushuru inaweza kuwanyima haki ya kuchagua,” alisema Getrude John mkazi wa Bunju jijini Dar es salaam.
Wakati waagizaji wa nje watalazimika kutoboa zaidi mifuko yao,kutokana na ongezeko la tozo huenda itakuwa kicheko kwa wazalishaji wa ndani wa bidhaa hiyo kwa sababu watafaidika na wateja ambao wataachana na mawigi ya nje, hivyo kuwaongezea faida.
Latest