Ufahamu mfumo wa kielektroniki wa kufuatilia ubovu wa barabara Tanzania

July 25, 2022 12:13 pm · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Unawawezesha watu kutoa taarifa za ubovu wa barabara katika maeneo yao.
  • Unatumia mfumo wa simu janja.
  • Utasaidia kuboresha miundombinu ya barabara nchini.

Mwanza.  Huenda umekuwa ukikerwa na ubovu wa barabara katika maeneo mbalimbali Tanzania lakini hujui ni wapi utoe taarifa ili uboreshaji ufanyike. Sasa hilo siyo tatizo tena.

Bodi ya Mfuko wa Barabara Tanzania imezindua mfumo wa kielektroniki wa kufuatilia kazi na hali ya barabara nchini ili kuongeza ufanisi wa matumizi ya barabara.

Meneja wa bodi hiyo, Eliud Nyauhenga amesema bodi iliamua kuunda mfumo huo ili kutoa taarifa kuhusu hali ya barabara ili kuwashirikisha wananchi hasa watumiaji wa barabara katika kusimamia na kutunza miundombinu hiyo. 

“Moja ya jukumu la bodi ya barabara ni kufuatilia matumizi ya fedha zinazopelekwa kwa wakala ili kujua thamani halisi ya fedha hizo kulingana na kazi zilizofanyika hivyo bodi iliaamua kuongeza ufanisi wa ufuatiliaji kwa kuunda mfumo (e-Monitoring) huo,” amesema Nyauhenga.

Nyauhenga aliwakuwa akizungumza leo Julai 25, 2022 jijini Mwanza katika warsha ya kujadili namna ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwenye miundombinu ya barabara.

Amesema kupitia mfumo huo taarifa za hali ya barabara kutoka kwa watumiaji wa barabara zitapelekwa kwa mameneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (Tarura) na Bodi ya Mfuko wa barabara ili hatua stahiki ziweze kuchukulia na kupeleka mrejesho kwa watoa taarifa.

“Mfumo huu umeandaliwa na wataalam wa ndani na kuidhinishwa na wakala wa Serikali Mtandao (eGA) inakadiriwa kuwa kama mfumo ungetenezwa na wataalam wa nje ungegharimu Sh300 milioni mbali ya gharama ya kulipia leseni pamoja na matenegenezo,” amesema.

Meneja huyo amesema mfumo umeshafanyiwa majaribio sehemu mbalimbali kwa kutumia makundi mbalimbali ya wadau na kuonyesha matokeo mazuri hivyo wananchi wanaweza kutumia simu-janja, au simu za kawaida kutuma taarifa kwa kutumia mfumo huo.

Taarifa zitakazotumwa kwenye mfumo huo ni pamoja na mashimo hatarishi, ujenzi mbovu, kuziba mifereji, kuibiwa alama za barabarani na uharibifu wa madaraja.


Tangazo


Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya ameipongeza bodi ya barabara kwa kubuni mfumo wa kielektroniki utakaotumiwa na wananchi na watumia barabara kufuatilia na kutoa taarifa kwa vyombo husika juu ya hali ya barabara katika maeneo yao.

Amesema amefurahishwa kwa kwa mfumo huo umetengenezwa na wazawa na kutoa rai kwa  taasisi za umma kuwatambua wataalamu wa ndani pale walipo, kuwaamini, kuwapa nafasi  na kuwajengea uwezo.

“Natoa rai kwa wakala wa barabara Tanroads na Tarura kuzifanyia kazi kwa wakati taarifa ambazo zitakuwa zinaletwa na watumiaji wa barabara na kutoa majibu kwa wakati,” amesema Mhandisi Kasekenya huku akitoa angalizo kwa wahusika ambao hawatazifanyia kazi kwa wakati taarifa hizo.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW