Majaliwa: Nyongeza ya mshahara ni kwa wafanyakazi wa kada ya chini

July 29, 2022 1:40 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Amesema nyongeza ilikuwa siyo ya watumishi wote.
  • Asema lengo ni kupunguza pengo kubwa la mishahara ya Serikali.
  • Aahidi Serikali kuendelea kuongeza mishahara ya wafanyakazi.

Dar es Salaam. Baada ya kuwepo kwa mjadala mpana kuhusu nyongeza ya mshahara ya asilimia 23.3 kwa watumishi wa umma, Serikali imesema nyongeza hiyo iliwalenga zaidi wafanyakazi wa kada ya chini ili kuwaboreshea maisha yao na kupunguza pengo la viwango vya mishahara. 

Mjadala huo umekuja baada ya baadhi ya wafanyakazi wa Serikali kudai kuwa kiwango kilichongezeka katika mishahara ya Julai mwaka huu ni kidogo na hakiendani na matarajio waliyokuwa nayo awali.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyekuwa akizungumza leo Julai 29, 2022 jijini Dodoma ametolea ufafanuzi sintofahamu hiyo na kueleza kuwa nyongeza ya mishahara iliwalenga zaidi wafanyakazi wanaopokea kima cha chini cha mshahara na siyo wafanyakazi wote.  

“Ni kweli asilimia 23 iliyotamkwa haijalipa watu wote, na hii ni kwasababu ya formula inayotumika katika kutamka viwango vya Mshahara. Inapotamkwa wanaonufaika si wote mpaka wa mishahara mikubwa, bali ni wale wa kada ya chini,” amesema Majaliwa.

Amesema wanaonufaika ni wale wa kada ya chini, ambao kwa tangazo la mwaka huu wanufaika ni asilimia 75 hadi 78 ya watumishi wote.

Amesema nyongeza hiyo itawafaidisha zaidi wafanyakazi wa kada ya chini ili wawezesha kuboresha maisha yao katika kipindi hiki ambacho karibu kila bidhaa imepanda bei, jambo linaloongeza ukali wa maisha.

“Ile asilimia iliyotamkwa iliwalenga zaidi wa kima cha chini sio tu wale wanaoanza kazi hata wale waliotangulia lakini kwa lengo la kuinua kiwango chao ili waweze kupata fedha inayowawezesha kukidhi mahitaji yao kwenye mazingira ya mabadiliko ya uchumi nchini,” amesisitiza waziri mkuu.


Soma zaidi: 


Mara ya mwisho kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa Serikali kilitangazwa mwaka 2015 ambacho kilikuwa Sh300,000 ambapo wafanyakazi wamekuwa wakitaka kiongezwe ili kuendena na hali ya uchumi wa sasa ikiwemo kupanda kwa bei za bidhaa.

Kiongozi huyo mkuu wa shughuli za Serikali amesema pia nyongeza hiyo itasaidia kupunguza pengo la mishahara ya wafanyakazi wa Serikali lisiwe kubwa sana kuhakikisha kila mtu anafaidika na rasilimali zilizopo nchini.

“Huku juu watumishi wenye mapato makubwa hawapati asilimia ile kama ilivyotamkwa kwa sababu ukiwalipa ile watakuwa wameenda mbali zaidi kuliko walioko chini. Kwa hiyo pengo la mishahara ya Serikali litakuwa kubwa,” amesema Majaliwa.

Amefafanua kuwa asilimia za nyongeza ya mishahara inapungua kwa kadri ya ukubwa wa kiwango cha mshahara anachopata mfanyakazi.

Amesema Serikali itaendelea kuongeza mishahara ili kuboresha maisha ya Watanzania kutegemea hali ya uchumi. 

Enable Notifications OK No thanks