Mahindi yachangia kupaisha mfumuko wa bei Agosti

September 8, 2022 2:19 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link


  • Umepaa hadi kufikia asilimia 4.6.
  • Mfumuko wa bidhaa za vyakula na vinywaji nao wapaa.
  • NBS yasema kupanda kwa bei ya baadhi ya bidhaa za vyakula zimechangia mfumuko huo.

Dar es Salaam. Huenda maumivu ya kuongezeka kwa gharama za maisha yakaendelea kushika kasi nchini  mara baada ya mfumuko wa bei  za bidhaa na huduma kuendelea kupaa na kuvunja rekodi kwa mwaka unaoishia Agosti kufikia asilimia 4.6.

Mfumuko huo wa bei umeongezeka kutoka asilimia 4.5 iliyorekodiwa mwaka ulioishia Julai  2022 huku hali hiyo ikichagizwa zaidi na kupanda kwa bei ya baadhi ya bidhaa za vyakula ikiwemo mahindi.

Kiwango hicho cha Agosti kilichotangazwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) leo Septemba 8, 2022 ni kiwango cha juu zaidi kuwahi kurekodiwa nchini tangu Oktoba 2017.

Kwa mujibu wa tovuti ya Trading Economics. Oktoba 2017 mfumuko ulikuwa asilimia 5.1.

Mfumuko wa bei wa Taifa hupima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya binafsi nchini.

“Kuongezeka kwa mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwaka ulioishia mwezi Agosti, 2022 kumechangiwa hasa na kuongezeka kwa mfumuko wa bei wa baadhi ya bidhaa za vyakula ikilinganishwa na kipindi cha mwaka ulioishia mwezi Julai, 2022,” imeeleza NBS katika taarifa yake.


Soma zaidi:


Baadhi ya bidhaa za vyakula zilizochangia mfumuko wa bei ni pamoja na ngano ambayo bei imeongezeka kutoka asilimia 3.7 hadi asilimia 6.0, unga wa mahindi (kutoka asilimia 19.3 hadi asilimia 37.2), na nyama kutoka asilimia 4.3 hadi asilimia 5.1.

Bidhaa nyingine zilizopaisha mfumuko huo ni mboga mboga kutoka asilimia 1.0 hadi asilimia 2.7, maharagwe (kutoka asilimia 1.9 hadi asilimia 2.7), mihogo mikavu (kutoka asilimia 8.0 hadi asilimia 8.4) na unga wa muhogo kutoka asilimia 9.5 hadi asilimia 10.9.

Mfumuko wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi umeongezeka kwa asilimia 1.3 zaidi kuliko ile iliyorekodiwa mwezi Julai.

“Mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwaka ulioishia mwezi Agosti, 2022 umeongezeka hadi asilimia 7.8 kutoka asilimia 6.5 kwa mwaka ulioishia mwezi Julai, 2022,” imesema taarifa hiyo.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW