Majaliwa akemea wizi vifaa ujenzi reli ya kisasa

October 17, 2022 10:16 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali inaendelea kutekeleza miradi yote ya kimkakati nchini na kwamba hakuna mradi wowote utakaokwama. Picha| Ofisi ya Waziri Mkuu.


  • Asema kuna tatizo ambalo wameanza kuliona katika mradi huo la wananchi kudokoa vifaa vya ujenzi.
  • Alitaka Jeshi la Polisi kuchukua hatua kali kwa watakaohusika.
  • Ataka mkandarasi alindwe ili akamilishe kazi yake. 

Mwanza. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameliagiza Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza kuhakikisha hakuna vifaa vitakavyoibwa katika mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), kipande cha tano kutoka Mwanza hadi Isaka (Shinyanga) ambao umefikia asilimia 14.

Majaliwa aliyekuwa akizungumza baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo katika kituo cha Fela wilayani Misungwi jana Oktoba 16, 2022 amesema kuna tatizo ambalo wameanza kuliona katika mradi huo la wananchi kudokoa vifaa vinavyotumika katika ujenzi huo ikiwemo nondo, saruji na mafuta ya magari.

Waziri Majaliwa ameliagiza Jeshi la Polisi kuhakikisha mkandarasi wa mradi huo hakwamishwi kwa sababu ya wizi wa vifaa.

“Natoa wito kwa Jeshi la Polisi Mkoa na Wilaya hakikisheni kampuni hii inayotekeleza mradi huu haipotezi mali zao wanapotujengea reli yetu Watanzania, na yeyote atakayeingia kwenye wimbi la wizi wa vifaa vya ujenzi hatua kali za kisheria zichukuliwe,” amesema Majaliwa.

Amesema Serikali imeridhia  kutoa pesa kwa ajili ya kukamilisha mradi huo hivyo haitegemei kutengeneza hasara na kuwataka wananchi wa wilaya hiyo kuhakikisha kila mmoja anakuwa mlinzi wa mwenzake.

Pia amewataka mafundi wote ambao wameshiriki katika mradi wa ujenzi huo pindi utakapokamilika wawe mahili katika ufundi kulingana na kitengo alichokuwa anafanyia kazi.

Waziri Majaliwa amemtaka mkandarasi wa mradi huo kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi huo kwa kufanya kazi kwa saa 24 na kuongeza nguvu kazi ili mradi huo ambao unapaswa kukamilika Mei 24, 2024 ukamilike mapema.

Pia amewataka wananchi wa Misungwi kutumia fursa ya eneo la kituo cha reli cha Fela ambacho kitakuwa bandari ya nchi kavu baada ya kukamilika kwa ujenzi wa reli hiyo ya kisasa kufanya uwekezaji kwa kujenga hoteli na nyumba za kulala wageni ili kujiinua kiuchumi.

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya, amesema hadi sasa ujenzi huo umefikia asilimia 14 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Mei mwaka 2024.

Amesema kipande hicho cha tano kina urefu wa kilomita 1,219 na kitagharimu zaidi ya Sh3.12 trilioni.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Amina Lumuli amesema katika kipande hicho watalaza reli takriban 500,000 hadi kukamilisha ujenzi  wa mradi huo  na kutakuwa na vituo (station) 10 ikiwemo ya Fela ambacho kitakuwa bandari ya nchi kavu.

“Katika vipande vyote vitano mradi utatumia kiasi cha Sh16.17, na Serikali kwa ujumla imeishalipa kwa kazi zote ambazo zimeishafanyika kwenye mradi mzima kiasi cha zaidi ya Sh6 trilioni na utapunguza muda wa safari kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza kutoka masaa 20 hadi 8 pia utapunguza gharama za usafirishaji wa mizigo kwa asilimia 30-40,” amesema Lumuli. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW