Wizi wa mafuta reli ya kisasa wamkera waziri

December 26, 2021 4:56 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni wizi wa zaidi ya lita 4,000 uliofanyika katika kituo cha Malampaka.
  • Naibu Waziri Waitara asema ni aibu kwa Taifa.
  • Aagiza waliohusika wachukuliwe hatua kali. 

Mwanza. Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara amekemea vitendo vya wananchi wanaozunguka eneo la mradi wa ujenzi wa reli ya Kisasa (SGR) kipande cha Isaka- Mwanza kituo cha Malampaka wilayani Maswa Mkoa wa Simiyu kuiba mafuta ya kuendeshea magari na mitambo ya mkandarasi anayetekeleza ujenzi huo.

Waitara ameuagiza uongozi wa wilaya hiyo kuhakikisha unakomesha wizi huo kwa kutoa elimu kwa wananchi, kukamata wahusika, kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria na kuwachukulia hatua kali ili wawe mfano kwa wengine wenye tabia hizo.

Naibu Waziri huyo ametoa maagizo hayo baada ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo Desemba 24, 2021 katika kituo cha Malampaka na kuelezwa kuwa zaidi ya lita 4,000 za mafuta zimeibwa. 

“Limejitokeza suala la wizi kwenye eneo la mradi katibu tawala simamieni hili ni aibu kusikia kuna wizi wa mafuta, watakaopatikana wawe mfano kwa sababu ni sifa mbaya kwa nchi fanyeni mikutano na wananchi, watafuteni wahusika na muwachukulie hatua kali,” amesema Waitara.

Aidha, ameonya tabia ya wafanyakazi wazawa kunyanyaswa kwa kucheleweshewa malipo yao na kuvunjiwa utu wakiwa kazini.

“Kuna matukio yameanza kujitokeza kuonea wafanyakazi, kunyanyaswa na kutoheshimiwa kama tumekubaliana huyu atalipwa kiasi fulani lazima izingatiwe na Watanzania wenzetu mliopo hapa hakikisheni mnasimamia hili, lazima haki za watu wetu ziheshimiwe na muwaambie msiwachekee tukija hapa mtu akilalamika na hamkusimamia basi lazima mtawajibishwa,” amesema.

Waitara alilitaka Shirika la Reli Tanzania (TRC) na idara ya ardhi kuhakikisha wananchi waliochukuliwa maeneo yao wanalipwa fidia kwa wakati na tathmini zifanyike mapema kuondoa malalamiko huku akiwataka wasimamizi wa mradi huo kuhakikisha kunakuwepo mpango wa kutunza mazingira katika maeneo ya kuchimba kokoto na kuweka udongo mchafu ili kutoacha mashimo tupu yatakayoleta hasara kwa wananchi. 

“Maeneo haya mengi yanatumika kwa kilimo ni huzuni kwa wananchi kutolipwa kwa wakati, tathmini zifanyike malipo yatoke mapema na haya ni maelekezo ya Rais na lazima yazingatiwe hatuhitaji tuwe na mambo makubwa halafu mambo madogo yawe yanalalamikiwa,” amesema.

Mradi huo umefikia asilimia nne huku ekari 2,213.75 zikiwa zimeshatwaliwa na Sh 2.7 bilioni zikilipwa kwa wafidiwa.

Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Swege Kaminyoge amesema hadi sasa watu wanne wanashikiliwa kwa tuhuma za wizi huo huku watatu wakiwa tayari wamefikishwa mahakamani ambapo wanaendelea kufanya msako kuhakikisha wanakomesha vitendo hivyo.

Naibu Meneja Mradi wa SGR kituo cha Malampaka, Alex Bunzu amesema ujenzi huo utagharimu Sh3.06 trilioni na utakamilika Mei 15, 2024 ambapo Watanzania 2,094 sawa na asilimia 19.05 ya ajira tarajiwa wakiajiriwa.  

Enable Notifications OK No thanks