Watatu mbaroni wizi vifaa vya ujenzi daraja la Magufuli
- Ni daraja la Kigongo-Busisi mkoani Mwanza ambalo ujenzi wake unaendelea.
- Wanatuhumiwa kuiba vifaa vya ujenzi zikiwemo nondo na nyaya.
- Daraja hilo litakuwa kiungo muhimu cha mikoa ya Mwanza na Geita.
Dar es Salaam. Jeshi la Polisi mkoani Mwanza linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za kuiba vifaa vya ujenzi katika mradi wa daraja la JPM Kigongo-Busisi.
Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Wilbroad Mtafungwa akizungumza na waandishi wa habari leo Disemba 10, amewataja watuhumiwa hao kuwa ni fundi nondo wa ujenzi wa mradi huo, Seif Yusuph na mfanyakazi wa kampuni ya ujenzi wa daraja hilo China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) Hamfrey William.
Mwingine ni mlinzi wa kampuni ya ulinzi Cops Security Tanzania Limited, Bwire Manyama.
Kamanda Mtafungwa amesema Disemba 8 mwaka huu, walipokea taarifa kutoka kwa kampuni ya CCECC kuwa kuna wizi wa vifaa vya ujenzi wa daraja la Dk John Pombe Magufuli (JPM) na kuanza kufanya ufuatiliaji.
“Walifika (askari) katika kitongoji cha Busisi madukani kwenye nyumba inayomilikiwa na Makona Samwel kupitia upelelezi huo Jeshi la Polisi lilifanikiwa kupata vitu mbalimbali vikiwa vimefichwa ndani ya nyumba hiyo na vyote vikiwa ni vifaa vinavyotumika kwenye mradi wa kimkakati wa daraja la JPM,” amesema Mtafungwa.
Vitu hivyo, ni pamoja na mashine saba za kuchomelea, Stick za kuchomelea vyuma aina ya THJ 422 Box 30, nyaya (Welding Cable, Drilling Bit) mbili ambapo bado thamani yake haijafahamika.
Uchunguzi wa awali umeonesha Samwel alishirikiana na Hamfrey William ambaye ni mfanyakazi pia wa kampuni ya CCECC kama fundi wa kuchomelea na mlinzi kwenye daraja hilo.
Jeshi la Polisi pia linashikilia Gari aina ya Toyota NOAH rangi nyeusi yenye usajili wa namba T 707 BPG inayosadikiwa kuhusika katika kubeba vitu hivyo vilivyoibwa baada ya kukutwa limetelekezwa eneo la Busisi madukani Wilaya ya Sengerema.
Daraja hilo ambalo limepewa jina la John Magufuli linalounganisha mikoa ya Mwanza na Geita na nchi za maziwa makuu likikamilika litakuwa na urefu wa kilomita 2.3 na upana mita 28.45 na ujenzi wake utagharimu Sh699 bilioni.
Daraja hilo linalotajwa kuwa refu kuliko yote Afrika Mashariki, na la sita kwa urefu barani Afrika litakuwa mbadala wa vivuko vya MV Misungwi, MV Sengerema na MV Mwanza vinavyofanya safari zake Ziwa Victoria.
Licha ya daraja hilo ambalo litakamilika 2024 kutatua tatizo la usafiri wa majini, pia litaufanya Mkoa wa Mwanza kuwa kivutio kikuu cha utalii na biashara kwa nchi za maziwa makuu.