Mwili wa Mtanzania aliyefia vitani Ukraine wasafirishwa kuja Tanzania
- Waziri tax asema mwili wake umeondoka Urusi asubuhi ya leo.
- Nemes Tarimo aliuawa Oktoba 24, 2022 wakati akipigana kuisaidia Urusi katika vita hiyo.
- Serikali yahoo tahadhari Watanzania waishio nje ya nchi.
Dar es Salaam. Wakati mwili wa Mtanzania, Nemes Tarimo aliyefariki dunia katika vita nchini Ukraine, ukiondoka Urusi kuja Tanzania kwa ajili ya maziko, Serikali imewataka Watanzania waishio nje ya nchi kuzingatia sheria na taratibu ili kulinda taswira nzuri ya kimataifa.
Mtanzania huyo aliuawa Oktoba 24, 2022 wakati akipigana kuisaidia Urusi katika vita hiyo iliyodumu tangu Februari 2022.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Stergomena Tax akizungumza na waandishi wa habari Januari 24, 2023 amesema Serikali inaendelea na taratibu kuhakikisha mwili wa Mtanzania huyo unarejeshwa nchini kwa ajili ya kuzikwa na familia yake.
“Wizara inaendelea kuwasiliana na Serikali ya Urusi kuhakikisha mwili wa marehemu Tarimo unarejeshwa nchini na kukabidhiwa kwa familia husika ili taratibu za mazishi ziweze kufanyika kwa kuzingatia mila na desturi za Kitanzania.
“Mwili umeondoka Urusi asubuhi hii,” amesema Dk Tax.
Taarifa zinaeleza kuwa Tarimo alikwenda Urusi na kujiunga na Chuo Kikuu cha Moscow Technological University (MIREA) mwaka 2020 kwa masomo ya shahada ya uzamili katika fani ya “Business Informatics”.
Hata hivyo, Machi 2022, alihukumiwa kifungo cha miaka saba jela kwa mujibu wa Sheria za Urusi kwa vitendo vya uhalifu.
Akiwa gerezani, Tarimo alipewa nafasi ya kujiunga na kikundi cha kijeshi cha Urusi kiitwacho Wagner kwa ahadi ya kulipwa fedha na kuachiwa huru baada ya kumalizika kwa vita hiyo, ameeleza Dk Tax kuwa wamepokea taarifa hizo kutoka Serikali ya Urusi.
Watanzania zingatieni sheria
Serikali imewataka Watanzania kuzingatia na kufuata sheria, kanuni na taratibu za nchi walizopo ili kulinda taswira nzuri ya nchi ya Tanzania.
Dk Tax amefafanua kuwa kwa mujibu wa sheria za Tanzania, Mtanzania yeyote haruhusiwi kujiunga na Jeshi la nchi yoyote duniani zaidi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania kwa kufuata taratibu zilizopo.
“Nitoe rai kwa watanzania kuhakikisha wanazingatia sheria kanuni na taratibu za nchi walizopo, na pia wawe mabalozi wazuri wa kulinda taswira ya Tanzania. Ikumbukwe kuwa kwa mujibu wa sheria zetu, Mtanzania yoyote haruhusiwi kujiunga na jeshi la nchi yoyote isipokuwa Jeshi la Tanzania na kufanya hivyo ni kuvunja sheria”, amesema.
Hata hivyo, amesema diaspora wa Kitanzania wikiwemo wanafunzi walioko masomoni nchini Urusi kuwa Serikali kupitia ubalozi wake uliopo nchini humo itaendelea kuwapa ushirikiano na kuhakikisha Watanzania hao wako salama wakati wote.
Latest