Wabuni mfumo kuwawezesha wanafunzi kujifunza kwa vitendo masomo ya sayansi
- Ni teknolojia ya uhalisia pepe na uhalisia ghushi.
- Mwanafunzi anaweza kutumia teknolojia hizo kwa simu au kompyuta yenye intaneti.
- Zinamsaidia kujifunza kwa vitendo na uhalisia masomo ya sayansi.
Dar es salaam. “Kutokana na ugumu wa kujifunza niliachana na masomo ya sayansi na uinjinia, nikaenda kusoma masomo ya biashara.”
Ni mbunifu katika sekta ya elimu, Aginiwe Kusiluka akielezea namna ilivyo vigumu kuelewa masomo ya sayansi katika mazingira yasiyo na miundombinu rafiki kama maabara, vifaa vya maabara na walimu wa masomo husika.
Kusiluka ni mfano tu wa vijana wengine waliokatisha ndoto zao kutokana na kutokuwepo kwa mazingira rafiki ya kusoma masomo ya sayansi hasa katika shule za Serikali.
Kwa mujibu wa uchambuzi wa matokeo ya kidato cha nne ya mwaka 2021 uliofanywa na Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) unaonesha wanafunzi 52,514 sawa na asilimia 44.6 ya waliofanya mtihani wa fizikia mwaka jana walifeli somo hilo kutokana na kutokuwa na uelewa wa kutosha na kushindwa kutumia vifaa wakati wa majaribio.
Kwa kutambua hilo baadhi ya vijana Watanzania wamebuni mfumo rahisi unaoitwa ‘Smart Darasa’ unaowawezesha wanafunzi kusoma na kuyaelewa masomo ya sayansi kwa vitendo, jambo linalotarajiwa kuchochea ufaulu wa masomo hayo.
Mfumo huo unaotumia teknolojia ya uhalisia pepe (Virtual reality) na uhalisia ghushi (augmented reality) unalenga kumwezesha mwanafunzi wa sekondari kuyaelewa masomo ya sayansi ya Kemia, Bailojia, Fizikia na Hisabati.
Unafanyaje kazi?
Kupitia Smart Darasa, mwanafunzi ana uwezo wa kusoma dhana za kisayansi zilizofafanuliwa, kuona kwa uhalisia vitu mbalimbali. Mfano, mfumo wa upumuaji au wa mmeng’enyo pamoja na kufanya majaribio ya kisayansi katika masomo husika ikiwemo upasuaji.
Kusiluka ambaye ni Mtendaji Mkuu wa shughuli za Smart Darasa ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) walibaini kuwa wanafunzi wengi wanakariri badala ya kuelewa masomo ya sayansi hivyo, mfumo huo utarahisisha uelewa wao.
“Itakuwa rahisi kuyaelewa masomo ya sayansi, kujifunza kwa vitendo, kufanya majaribio yaliyopo kwenye masomo yao kwa kutumia dijitali mahali popote na muda wanaoutaka kwa gharama nafuu,” anasema Kusiluka.
Soma zaidi:
Inapatikana vipi?
Kwa sasa huduma hiyo inapatikana bure katika njia mbili: tovuti ya smartdarasa.com ambako mwanafunzi anaweza kujipatia maudhui yaliyo katika uhalisia pepe yanayofafanua maada za masomo husika pamoja maswali yaliyo katika picha jongevu.
Huduma hiyo pia inapatikana kupitia programu tumishi inayoitwa Smart Darasa ambayo inamsaidia mwanafunzi kuviona vitu katika uhalisia (Augmented Reality) kwa kutumia simu yake.
“Kwa hali ya kawaida mwanafunzi anatakiwa aende maabara ili kuona kiunzi lakini kupitia programu tumishi mwalimu au mwanafunzi anaweza kutizama kiunzi cha mwili wa binadamu kama kilivyo mahali popote alipo,” anasema Kusiluka.
Kwa kutumia teknolojia ya uhalisia pepe huduma hiyo inapatikana kupitia kadi zenye picha mgando ambazo kwa kutumia programu maalumu picha hizo hugeuka kuwa picha jongevu (video) inayoelezea mada fulani.
“Kwa sasa Smart Darasa ni bure kabisa, kitu pekee kinachouzwa ni hizi kadi za masomo mbalimbali ambazo zipo 24, boksi zima tunauza Sh10,000 na kadi moja Sh500,” anasema.
Baadhi ya dhana (concept) za somo la Fizikia zilivyofafanuliwa katika tovuti hiyo. Picha|Smart Darasa.
Viunzi vya kuvuka
Tangu kuanzishwa kwake mpaka sasa Smart Darasa imewafikia zaidi ya wanafunzi 1,000 pamoja na walimu 70 ambao wamekuwa wakirejesha mwitikio chanya.
Pamoja na mapokezi hayo mazuri bado wale ambao hawana uwezo wa kumiliki simu janja na kupata huduma za intaneti, kwa sasa hawafaidiki na huduma hii.
“Kwa sasa tumelenga maeneo ambayo simu janja na huduma ya intaneti zinapatikana kwa urahisi, huduma yetu itakuwa inakua kulingana na ukuaji wa huduma hizo,” anasema mbunifu ambaye wanaendesha mfumo na wenzake watano.
Wanatarajia kuiweka huduma hiyo katika vitabu vyote vya masomo ya sayansi ambapo picha mgando zilizopo katika vitabu hivyo zitakuwa na uwezo wa kugeuka kuwa picha jongefu kwa kutumia programu maalumu.
Smart darasa ni mfumo wa elimu ulioasisiwa mwaka 2016 kama wazo la kusaidia wanafunzi kuyaelewa masomo ya sayansi kwa urahisi na mwanzilishi wake Elias Elisante ambapo ulianza kufanya kazi rasmi mwaka 2019.
Miongoni mwa malengo yao ni kuongeza kiwango cha wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi kuingia kwenye taaluma za masomo husika.