2025 mwaka wa hukumu kwa marais wastaafu
- Rais wa zamani wa Brazil, Jair Bolsonaro na Rais Álvaro Urib ni miongoni mwa walikubwa na hukumu hizo.
Dar es Salaam. Rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Joseph Kabila, amehukumiwa kifo na Mahakama ya Kijeshi nchini humo baada ya kumtia hatiani kwa makosa makubwa ikiwemo uhaini, uasi na uhalifu dhidi ya ubinadamu.
Hukumu hiyo ilitolewa jana Jumanne Septemba 30, 2025 na Luteni Jenerali Joseph Mutombo mjini Kinshasa bila Kabila mwenyewe kuwepo mahakamani.
Kabila (54) alipatikana na hatia ya kushirikiana na waasi wa kundi la M23, linalopinga Serikali ya Congo na kudhibiti maeneo mengi ya mashariki mwa nchi hiyo yenye utajiri mkubwa wa rasilimali, likisaidiwa na Rwanda.
Taarifa zinaonesha kuwa Kabila aliondoka nchini humo mwaka 2023, na alionekana tena Mei 2025 katika mji wa Goma unaodhibitiwa na waasi hao.

Wafuatiliaji wa mambo wanasema hukumu hiyo inalenga tu kuzuia azma yake ya kuunganisha upinzani, licha ya kwamba hajulikani aliko kwa sasa.
Hukumu ya Joseph Kabila inakuja kama muendelezo wa mfululizo wa matukio ya marais wastaafu kushtakiwa na kuhukumiwa kwa makosa yaliyotokea wakati wa uongozi wao au yale yanayohusiana na mienendo yao ya kisiasa.
Siku chache zilizopita Rais wa zamani wa Ufaransa Nicolas Sarkozy alihukumiwa kifungo cha miaka mitano jela baada ya kupatikana na hatia ya kula njama ya uhalifu katika kesi inayohusiana na mamilioni ya euro ya fedha kutoka kwa kiongozi wa Libya marehemu Kanali Muammar Gaddafi.

Mahakama ya jinai ya Paris ilimuondolea mashtaka mengine yote, ikiwa ni pamoja na rushwa na ufadhili haramu wa kampeni.
Septemba 12, mwaka huu Rais wa zamani wa Brazil, Jair Bolsonaro, alihukumiwa kifungo cha miaka 27 na miezi mitatu jela baada ya kupatikana na hatia ya kupanga njama za kufanya mapinduzi ya Serikali.

Hukumu hiyo imetolewa na majaji wa Mahakama ya Juu ya nchi hiyo baada ya kumtia hatiani kwa makosa matano, ikiwemo kosa la kujaribu kumuua Rais wa sasa, Luiz Inácio Lula da Silva, na jaribio la kubatilisha utaratibu wa kidemokrasia.
Rais wa zamani wa Georgia, Mikheil Saakashvili naye alihukumiwa kifungo cha nyongeza cha miaka tisa (9) Machi 2025 kwa kosa la matumizi mabaya fedha ya umma, miongoni mwa makosa mengine.

Nchini Colombia, Rais Álvaro Uribe alipatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo cha ndani (house arrest) kwa karibu miaka 12 mwezi Agosti 2025, kufuatia jaribio la kuharibu au kubadilisha ushahidi na kutoa rushwa kwa maafisa wa umma katika kesi iliyohisha uhusiano wake na wanamgambo wa zamani wa mrengo wa kulia.

Katika kesi iliyodumu kwa miaka 13, Uribe alipatikana na hatia ya mashtaka hayo mawili ambapo kesi yake ilitolewa hukumu na Jaji Sandra Liliana Heredia.
Dunia inashuhudia enzi mpya ambapo heshima na kinga za urais hazilindwi baada ya kuondoka madarakani, na viongozi wa zamani wanahesabiwa kwa makosa yao bila kujali hadhi waliyo nayo.
Latest



