Serikali ya Marekani yafungwa baada ya Bunge kutopitisha muswada wa bajeti

October 1, 2025 12:15 pm · Esau Ng'umbi
Share
Tweet
Copy Link

Serikali ya Marekani yafungwa baada ya Bunge kutopitisha muswada wa bajeti 

  • Kwa sasa hakuna mwelekeo wa wazi wa kutatua mgogoro huu, kwa kuwa pande zote  mbili bado zinatofautiana  juu ya namna gani ya kuukwamua mkwamo huo.

Dar es Salaam. Serikali ya Marekani imefungwa rasmi usiku wa kuamkia leo Oktoba Mosi mara baada ya Bunge na Ikulu ya Marekani kutokukubaliana juu ya muswada wa bajeti ya marekani uliopendekeza  kuongeza fedha za uendeshaji wa shughuli za serikali kuu.

Licha ya kwamba Chama cha Republican cha Rais Donald Trump ndicho  kinadhibiti mabaraza yote mawili ya Bunge la Marekani yaani Baraza la Seneti na Baraza la wawakilishi, bado kinahitaji msaada wa chama cha Democratic ili muswada upitishwe katika Seneti ambako kura 60 zinahitajika.

Hata hivyo, pande hizo mbili zimeshindwa kuandaa muswada unaokubalika na wote, baada ya Seneti kukataa mapendekezo ya Republican na pia ya Democratic saa chache kabla ya muda wa kufungwa kwa Serikali kumalizika.

Kikawaida Mwaka wa fedha wa Marekani huanza Oktoba Mosi na humalizika Septemba 30. Hii ni kusema kwa sasa Serikali ya Marekani haina bajeti ya kuendesha shughuli za Serikali kuu.

Hii ni mara ya kwanza serikali inafungwa tangu mwaka 2018, katika muhula wa kwanza wa Trump, kufungwa kwa Serikali  kulidumu kwa siku 34 ambao ni  muda mrefu zaidi katika historia  hadi mwanzoni mwa mwaka 2019. 

Kwa sasa hakuna mwelekeo wa wazi wa kutatua mgogoro huu, kwa kuwa pande zote  mbili bado zinatofautiana  juu ya namna gani ya kuukwamua mkwamo huo.

Wafanyakazi wa Serikali kuu watakosa mishahara kipindi chote cha kufungwa kwa serikali, huku wabunge na Rais Trump wakiendelea kulipwa mishahara yao.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Bajeti ya Bunge (CBO), takribani wafanyakazi 750,000 watasitishwa kazi kila siku, huku wengine wanaofanya kazi muhimu kama maafisa wa Usalama wa Usafiri wa Anga (TSA), waelekezaji ndege, maafisa wa usalama wa shirikisho na wanajeshi watalazimika kuendelea kufanya kazi bila malipo.

Hata hivyo, Kwa mujibu wa sheria za Marekani wafanyakazi wote watalipwa mishahara ya nyuma mara Serikali itakapofunguliwa tena, hata kwa muda ambao hawakufanya kazi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks